Wednesday, October 14, 2015

Namna ya kuleta mvuto getini




Hapo kwenye lango kuu la kuingilia nyumbani kwako almaarufu getini bila shaka ndio mbele ya nyumba yako. Ni eneo ambalo mgeni wako anapata hisia za mwanzo kabisa juu ya nyumba yako, kwa hivyo pafanye pavutie. Elimika kwa dondoo hizi za namna ya kuongeza mvuto kwenye eneo la mbele la lango kuu kwa kuboresha kile kilichopo na kuondoa muonekano wa nyumba iliyochoka:

·       Weka paa juu ya geti. Paa juu ya geti lina faida kama pambo na matumizi vilevile.
Faida kuu ya paa ni ulinzi wa geti lenyewe kutokana na maji ya mvua na jua kali. Jua kali linaharibu rangi kwa kuzipausha au kuzimomonyoa na wakati huo huo maji ya mvua yakisababisha geti kupata kutu ndani ya miaka michache hasa maeneo ya chini. Kwa kuweka paa inasaidia eneo la chini liwe kavu na mvua isiloanishe geti moja kwa moja. Faida nyingine ya paa getini ni kumpa kivuli mgeni wa miguu baada ya kugonga kengele nawe ukitafuta funguo kwenda kumfungulia. Pamoja na kivuli vile vile paa getini linamkinga mgeni wakati wa mvua. Kwa upande wa mapambo ni kwamba zipo paa za mitindo mingi na pia rangi ya paa la getini inaoana na ya paa la nyumba na hivyo kuvutia.
·       Njia nyingine ya kuleta mvuto getini ni kuweka taa, au hata kama taa zipo ni kwamba wenye nyumba wengi wanakuwa na mtindo mmoja wa taa kwa miaka mingi wakati mitindo mipya inakuwa ipo sokoni. Mbali na ulinzi na usalama taa za getini zinaleta mvuto pale mwanga unapomulika kwenye miti, maua, nyumba na hata njia iliko.
·       Ongeza mvuto wa mbele ya lango kuu kwa kuweka urembo wa mawe yawe ni ya asili ama ya kutengenezwa viwandani. Mawe haya ndio sanaa pekee unayoweza kuweka kwenye ukuta wa getini mbele ya nyumba na kuwa na amani kuwa mwizi hawezi  kuyaiba kwakuwa yanajengewa mlemle ukutani tofauti na sanaa nyingine ambayo ungeweza kuitundika na ikaibiwa. Chagua mawe au urembo ambao unaendana na sehemu nyingine ya nyumba.
·       Mara kwa mara tunza geti kwa kulipaka rangi ili lisionekana kukukuu, kwakuwa eneo lililopo  bila shaka linapatwa na shurba nyingi ambazo ni pamoja na upepo mkali. Usiruhusu muonekano wa geti uwe na rangi yenye mikwaruzo. Kama kanuni nyingine zozote za rangi, paka rangi inayotakiwa kwa eneo hilo iwe ni geti la mbao au chuma au mchanganyiko wa mbao na chuma. Rangi ya geti inavyokuwa mpya na ya kupendeza moja kwa moja nyumba nzima inavutia. Na rangi ipakwe baada ya matengenezo yoyote yanayohitajika kukamilika kwanza.
·       Endapo eneo linaruhusu pandikiza ukanda wa maua getini kwako, huku ukitengeneza ukuta mfupi wa kuvutia kuzunguka kitanda cha maua hayo. Ukuta huo unaweza kuwa wa mawe ya asili ama wa saruji tupu na kupakwa rangi. Kwenye maua yako changanya makubwa kwa madogo. Vilevile kama kuna uwezekano wa kutundika vyungu vya maua basi fanya hivyo
·       Weka kengele yenye hadi ya nyumba yako.
·       Tengeneza sakafu ngumu getini kwenye njia ya kuingilia nyumbani. Hii sio tu itasaidia eneo lisiwe chepechepe na tope wakati wa mvua bali pia italeta mvuto kwani mawe ya kutengeneza sakafu ngumu ni mengi ya maumbo na rangi mbalimbali.


Kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment