Wengi
wetu tunatumia kipasha chakula (microwave) kwa ajili ya kupasha chakula, lakini
je unajua kuna kazi nyingi unazoweza kufanyia ndani ya microwave zaidi ya huu
ulimwengu wa kupasha chakula tu? Nimetafiti kazi mbalimbali zinazoweza kufanyika
ndani ya microwave na hakika zitakurahisishia maisha yako! Hata hivyo tukumbuke
kuwa
microwave imekuwa maarufu kwa ajili ya kufanya kazi kwa haraka zaidi.
Kwahivyo zaidi ya kupasha chakula, microwave inaweza kufanya yafuatayo:
·
Kuzuia
machozi wakati wa kukata kitunguu. Kikate eneo la juu na chini (kuondoa mizizi)
halafu kipashe kwenye microwave kwa sekunde 30. Kitoe na ndipo unaweza kukikata
bila tone la chozi!
·
Unaweza
ukaondoa kirahisi karatasi zilizobandikwa kwenye vyombo na vikontena kwa kupaka
maji eneo lenye karatasi halafu unakiweka chombo ndani ya microwave kwa sekunde
20. Gundi yote inayeyuka na unaondoa hiyo karatasi/lebo bila usumbufu wowote
tena bila kuacha alama kama ambavyo ungetoa kwa maji, sabuni na sponji wakati
wa kuosha.
·
Wote
tunajua kuwa asali inakuwa ngumu ikitulia. Ifanye irudi kuwa kimiminika chepesi
tena kwa kuiweka ndani ya microwave ikiwa wazi bila mfuniko kwa dakika moja.
·
Unaweza
kupika baadhi ya vyakula moja kwa moja kwenye microwave mara baada ya kuvimenya
maganda yake. Jaribu kwa viazi mviringo. Vilevile pika bisi ndani ya microwave kwa
dakika nne tu.
·
Kama
unataka kupika maharage na hukukumbuka kuyaloweka usiku kucha – jaribu mbinu
hii. Yaweke kwenye bakuli yakiwa yamefunikwa na maji na ongezea magadi soda
halafu yapashe kwenye microwave kwa dakika 10 yatoe yaache yapoe kwa muda wa
dakika 40, baada ya hapo yatakuwa tayari kwa kuunga mboga.
·
Unapata
shida ya kupata juisi kutoka kwenye hizo ndimu au limao? Lipashe kwa sekunde 15
utashangaa itakavyokuwa rahisi kukamulika.
·
Unachukia
kumenya vitunguu swaumu? Vitie maji
halafu vitoe viweke kwenye microwave kwa sekunde 20. Hali ya mvuke inasaidia ngozi
kavu ya nje itoke haraka.
·
Unaweza
kukausha viungo na mitishamba kwa ajili ya kuvihifadhi kwa muda mrefu kwa
kuvikausha kwenye microwave. Anza na dakika 3, vitoe viangalie hadi ufikie
kiwango cha ukavu unachohitaji.
·
Unateseka
kuondoa maganda ya nyanya kwa kisu wakati unapotaka kupika? Ziweke ndani ya
maji halafu pasha kwenye microwave kwa dakika tano. Zitoe ziache zikae kwa muda
wa dakika mbili. Ngozi itaanza kusinyaa na kutoka kirahisi.
·
Unaweza
kuyeyusha nyama na samaki zilizoganda kwa kutumia microwave. Chagua pale
palipoandikwa defrost. Muda wa kuyeyusha unategemeana na uzito wa chakula, kama
huna mizani kisia uzito wa unachotaka kuyeyusha. Microwave moja kwa moja
itaseti muda baada ya wewe kuchagua kiasi cha uzito.
·
Matumizi
mengine ya microwave ni pamoja na kuua vijidudu. Unaweza kuua vijidudu kwenye
sponji la kuoshea vyombo kwa kuliweka kwenye macrowave likiwa limeloa. Litoe
baada ya dakika 2.
Sina
shaka kuwa hakika utakuwa unafurahia matumizi yako mapya ya microwave. Kama
kuna ambayo unajua lakini sijaorodhesha hapa, tafadhali nijulishe nitapenda kusikia
toka kwako.
No comments:
Post a Comment