Monday, June 6, 2016

Njia sita za kuifanya nyumba iwe nyumbani

Msemo kuwa nyumbani ndipo moyo ulipo una ukweli usiopingika. Nyumbani ni mkusanyiko wa maisha, kumbukumbu na upendo. Kama unatafuta njia za kufanya nyumba yako iwe nyumbani, kuna vitu virahisi na
vidogodogo unavyoweza kufanya. Na hii haihusiani na kununua vitu vingi vya gharama kubwa. Fuatilia njia hizi ili uanze leo:

Pamba kwa picha
Wanasema picha inaongea maneno elfu moja. Kuongeza kumbukumbu ya picha kwenye mashelfu, juu ya meza na kuta za nyumba yako kutaifanya iwe nyumbani. Hii inaipa nyumba muonekano na hisia kuwa mtu fulani anaishi hapo, badala ya kuonekana kama nyumba tu. Pia ni njia nzuri za kuondoa hizo picha kutoka kwenye simu yako au kamera ili kuzipa lengo halisi.

Weka eneo la kukaa
Nyumba inageuka nyumbani pale kunapokuwa na eneo na viti vizuri vya kukaa kwa wenyeji na wageni. Kuwa na eneo la kutosha kwa ajili ya kukaa kutaleta mvuto wa mahali pa kuishi.

Fanya chumba cha kulala kiwe kama mahali patakatifu
Usingizi mzuri wa usiku ni kipaumbele kwa watu wa kila umri. Hakikisha usingizi mwororo kwa kuwa na kitanda na godoro linalofaa kwa kadri iwezekanavyo. Hii ni pamoja na malazi na mwanga wa chumba.

Usafi
Kila nyumba ina upekee wake na mahitaji tofauti kuendana na wakaaji wake. Nyumba safi ni ile ambayo hakuna vyombo vinavyoachwa vichafu iwe ni kwenye sinki, karo, beseni, ndoo, popote pale pa kuoshea vyombo kuendana na maisha unayoishi na nguo chafu hazijazagaa kila mahali sakafuni. 
Ni kujitahidi kupambana na uchafu palepale unapotokea ikiwa ni pamoja na kusafisha sakafu na kushughulikia madoa hasa palepale yanapotokea. 
Nyumba safi ni nadhifu nje na ndani na kuna kanuni mlizojiwekea hapo nyumbani ili kuiwezesha kuendelea kuwa safi.

Kuweka mapambo ya msimu
Kwenda na wakati kwa kuiweka nyumba katika hali ya wakati uliopo kwa mfano wakati wa sikukuu kuweka mapambo yanayoendana na wakati huo ambapo pia inaifanya nyumba igeuke kuwa nyumbani na kuwapa hisia waliomo juu ya sikuuku hiyo.

Jiko litumike
Hapa ina maana kuwa ndani ya nyumba kupikwe. Kuna baadhi ya nyumba ambazo hakupikwi ni watu wa kula barabarani tu. Ili nyumba yoyote ile igeuke kuwa nyumbani ni muhimu sana kuwe na chakula kila wakati. Jiko linapotumika kuandaa vyakula na harufu yake nzuri inaifanya nyumba kuwa na uhai wa kuitwa nyumbani.



No comments:

Post a Comment