Sunday, January 24, 2016

KUTOKA KWANGU.....Unapohitaji fundi mzuri wa TILES, zingatia dondoo hizi

Kosa dogo tu katika uwekaji wa marumaru sakafuni au ukutani kwa jikoni na bafuni linaleta ukakasi machoni. Marumaru moja tu inapokuwa imewekwa vibaya ,  inaweza kuharibu mtiririko mzima na kufanya muonekano wa kupinda. Mbaya zaidi kufanya marekebisho baadaye, inaweza kuwa
gharama, usumbufu na kuchafua maeneo mengine. Gharama inahusika hasa pale inapotokea toleo lile limeisha madukani na kuweka “kiraka” hutaki.

Ndio maana ni muhimu ukiwa na kazi ya kusimika marumaru uwe na fundi sahihi anayeweza kufanya kazi iliyotukuka toka mwanzo, kwa maana ya kusionekane makosa baadaye.

Nimeongea na mkandarasi Sood Domwa na akatoa dondoo zifuatazo za jinsi ya kuweza kumpata fundi marumaru mzuri. Bwana Sood anasema marumaru ni bidhaa ngumu sana kwamba huwezi kuifanya kwa namna yoyote ile ibonyee. Hata hivyo pamoja na ugumu wake ni rahisi mno marumaru kuvunjika. Hivyo basi ili kuzuia marumaru zilizokwisha simikwa sakafuni zisifanye mipasuko ni muhimu kuhakikisha hakuna nafasi kati ya marumaru na sakafu iliyo chini yake. Yaani marumaru inatakiwa ishikane kabisa na eneo lililoibeba. Nafasi wazi chini ya marumaru itasababisha marumaru kukunjika pale ambapo uzito wa mwili unakaa juu yake mtu anapoikanyaga akitembea na hivyo kuifanya ivunjike.

Kutokana na haya yote ndipo tunasema ni muhimu kupata fundi wa viwango kwa kutumia dondoo hizi:

Uliza wakandarasi
Kuna uwezekano mkubwa wa kumpata fundi mzuri wa kuweka marumaru kutoka kwa wakandarasi. Hii ni kwasababu kazi kubwa za kuweka marumaru ziko kwenye majengo makubwa ya biashara, na wakandarasi wanavutiwa zaidi na kazi za namna hiyo kuliko hizi ndogondogo za nyumba za kuishi. Kwahivyo kuongea na mkandarasi kwako wewe unayejenga nyumba ya kuishi kutakupa uwezekano mkubwa wa kukupatia fundi mzuri wa marumaru. Pia kama utafanikiwa kupata mkandarasi aliyeko tayari kufanya kazi yako ndogo itafaa zaidi, sababu ikiwa ni ile ile kuwa wana uzoefu mkubwa wa kuweka marumaru kwenye majengo ya biashara. Na sikuzote mwenye nyumba kataa kuchukua fundi wa kuweka marumaru kutoka vibarua.
Fundi marumaru wa kufanya kazi yako anatakiwa kuwa na uzoefu wa kazi hiyo usiopungua miaka mitatu, muulize akuonyeshe kazi zake. Na kuangalia picha tu ya kazi za nyuma hakutoshi- picha zinaweza kudanganya. Sisitiza kuona angalau eneo moja alilosimika marumaru.

Uliza kwa Wauzaji
Wauzaji wengi wa marumaru wanawajua mafundi wazuri na kuna wengine wanao mafundi wao kabisa. Pia mafundi wengi wanapenda kutengeneza urafiki na wauzaji ili wawe wanawaitia wateja kwa maana ya wao mafundi wapate kazi.

Hakiki Ubora
Wakati unapoangalia kazi za fundi alizofanya kabla, fahamu kwamba uwekaji marumaru hautofautiani kuendana na ukubwa. Angalia ulingano wa  ile nafasi kati ya marumaru moja na nyingine na pia hakikisha ile mistari ya grauti imelingana na kunyooka vizuri kabisa.

Angalia jinsi marumaru zilivyotandazwa. Je, kuna uwiano? Fundi mzuri anaanzia kati kati ya chumba ili vile vipande vya kuweka maeneo ya mwisho ya ukutani vikae vizuri na kwa ukubwa sawa. Pia tazama nyuma ya milango kwenye kona na kona zozote za kipekee zinazoweza kuwa kwenye chumba. Kwa ajili marumaru za kukata ni changamoto kwenye maeneo hayo, ni kielelezo kizuri cha ujuzi wa fundi. Hakikisha kuwa marumaru zinazozunguka fremu ya milango zimekaa vizuri laa zitafanya bonde au kuacha nafasi maji yasimame. Kama ni za ukutani angalia yale maeneo yenye bomba. Hakikisha kila mahali pamezibwa vizuri.

Usafi wakati wa uwekaji
Njia nyingine ya kupata fundi sahihi ni kwa kumuuliza  mwenye nyumba aliyefanyiwa kazi na fundi husika juu ya swala la usafi. Fundi anayefanya kazi ya marumaru kwa uchafu anachangia kuacha alama za kudumu sakafuni. Kwa mfano saruji ikishakaukia juu ya kioo cha marumaru zenye vishimoshimo huwa haitoki tena.

Gharama
Mafundi wengi wa kuweka marumaru wanapendelea kuchaji kwa mita za mraba. Na endapo wakianza kufanya kazi na ukajikuta kuwa muonekano uliotokea sio uliokuwa nao kichwani, utakuwa hujachelewa kama utabadili wazo mapema. Ila huenda ukaishia kulipa gharama mara mbili za kuondoa hizo ambazo zilishaanza kuwekwa tayari. Na ndio sababu ni muhimu kufikiria mapema kuhusu michoro na maeneo zinapochanganywa za rangi tofauti  ili kuondoa kadhia ya kurudia.

Mwishoni mkandarasi anasema  usitembee eneo lililowekwa marumaru kwa walau masaa 24 na kama ni bafu subiri hadi baada ya masaa 48 ndipo litumike. Hii ni muhimu ili kuacha grauti ikauke kabisa. 

No comments:

Post a Comment