Huenda unajiuliza ni kwa namna gani unaweza kutengeneza
muonekano wa kuvutia ndani ya nyumba yako. Dondoo hizi zitakuwezesha kupamba
kama vile wewe ni mtaalam wa mapambo ya ndani.
Pamba kwa jinsi ambayo unataka wewe, ni nyumba yako na ni
mahali unapoishi wewe. Hakikisha kuwa kila kitu unachoweka ndani ya nyumba yako
ungependa kukiona kila siku.
Weka makabati na shelfu katika hali ya usafi na yapambe
kwa ama sanaa au mimea hai midogogodo ya kwenye vyungu vigododogo. Sanaa za
mapambo zinaweza kuwa kwenye mfumo wowote hata kama ni michoro ya kwenye
sahani. Uamuzi ni wako
Baki kwenye mpangilio. Kama huna nafasi za kutosha za
kuhifadhia, weka vitu unavyovipenda peupe kama vile navyo ni mapambo. Kwa mfano,
unaweza kuweka vitabu vyako unavyovipenda juu ya meza ya kahawa au shelfu na
vikakaa vizuri tu kama vile ni mapambo na hapohapo umevihifadhi.
Chagua fenicha ambazo zinakidhi hitaji zaidi ya moja. Kwa
mfano, meza kubwa ya kuvalia inaweza kukidhi hitaji la droo za kuhifadhia
vilevile. Na kitanda chenye droo mvunguni kinakuwezesha kuhifadhia shuka, taulo
na mablanketi ya ziada badala ya mvungu kukaa bure.
Valisha kuta za nyumba yako kwa picha ambazo fremu zake
unaweza kutoa na kubadilisha picha ya ndani.
Weka vihifadhio vya kutosha kila mahali. Chumba chenye
tenga la nguo chafu kitafanikisha nguo zisitupwe sakafuni au kurundikwa kwenye
kiti.
Vilevile kabati la luninga lenye droo za kuhifadhia litawezesha mikanda
ya filamu isasambae sebule nzima.
Tumia vyema kona za chumba. Kona mara nyingi
zinasahaulika na kuachwa wazi, zijengee vishelfu ambavyo unaweza kuweka picha
au maua juu yake. Wapo pia wanaoweka hapo taa za urembo.
Sanaa ndogo inaleta matokeo makubwa. Kama huna ukuta
mkubwa kwa ajili ya kuweka mchoro mkubwa (kumbuka ukuta mkubwa unapendeza kwa
michoro mkubwa) usife moyo.
Tundika sanaa ndogondogo lakini ziwe karibukaribu
kwenye eneo moja kwa ajili ya kuleta mvuto. Wengi wanatumia mbinu hii kupamba
kuta zao.
Endapo unaweka fenicha mpya sebuleni anza na kubwa zikifuatiwa
na ndogo. Ukishakuwa na zile kubwa mahali pake (sofa, meza ya kahawa, viti,
vimeza vya kando na media), anza kuongeza vitu vya mapambo. Hii itasaidia
chumba kuwa na mshikamano. Hii ni kwa uzoefu wa kazi zangu za mapambo ya ndani.
Ongeza vitupio vya rangi kuchangamsha chumba. Unataka
kuleta matokeo makubwa ya mapambo yako? Ni rahisi: Ongeza rangi kwa kutumia
vitu kama mito, mitandio na vesi za maua ambavyo unaweza kuvibadili kirahisi
mara kwa mara.
Nawe msomaji wangu usisite kunishirikisha jinsi unavyopamba mahali unapoishi ili tuelimishe na wengine piga/whatsapp 0755 200023
No comments:
Post a Comment