Hata uwe na maji mengi kiasi gani ya
kumwagilia bustani, ni ukweli kuwa kiangazi kinatesa bustani nyingi. Watunza
bustani wanatumia muda mwingi kuitunza kuliko majira mengine ya mwaka. Sasa
majira yanabadilika tunategemea mvua za vuli na ni
fursa nzuri ya kuirudisha
bustani yako kwenye uhai wake.
Zifuatazo ni dondoo za namna ya
kutunza bustani katika majira ya vuli, ili ianze tena kung’aa kwa kile kijani
ambacho kimepotezwa na kiangazi kirudi.
Kwanza kabisa ni vyema ufahamu
wakati wa kukata majani na kukatia maua. Hii ni muhimu kwa ajili hata wakati wa
kiangazi hupaswi kukata majani kila mara au pia kuyakata yawe mafupi sana!
Nimewahi kuona bustani nyingi ambazo zinakatiwa chini kiasi kwamba unaogopa
kama majani yatachipua tena.
Maadam vuli inakuja na mvua kiasi
japo sio kama masika, kwa bustani inatosha tofauti na mazao mengine. Majani
bila shaka yatachipua na muonekano mzima utakuwa wa kuvutia.
Kumbuka kuweka mbolea. Kipindi cha
mvua za vuli ni kizuri kwa ajili ya kuweka tena mbolea bustanini. Mbolea ya
wanyama hasa kuku inafaa sana kurutubisha majani yashamirishe kijani chake
ambacho kilipotezwa na majira ya nyuma.
Kupunguza au kuacha kabisa
umwagiliaji. Kuendana na mkoa uliopo huenda mvua za vuli zikakurahisishia sana
kazi ya umwagiliaji wa bustani. Kwa sababu mvua zitanyesha hutapaswa kumwagilia
kivile. Kama uko mikoa ya baridi ni kwamba hutamwagilia kabisa kipindi cha
majira ya vuli wakati wale wa mikoa ya joto (ukanda wa pwani) wanapaswa
kumwagilia kwa kiwango kidogo sana.
Zalisha
mboji. Vuli ni wakati mzuri wa kuzalisha mbolea ya mboji ambayo ni mbolea
inayotokana na majani. Wakati wa kiangazi majani yanakauka na hayawezi
kutengeneza mbolea, kwahivyo kama kuna majani makavu ulikusanya wakati wa
kiangazi sasa ni wakati muafaka wa kuyatandaza kwenye vitanda vya maua ili
yapigwe na mvua yaoze kutengeneza mbolea.
Zuia mbu. Hili
ni jambo ambalo wengi wanasahau wakati wakiandaa bustani zao kwa mvua za vuli.
Kama tujuavyo mbu wanazaliana kwenye maji yaliyosimama. Tembea ndani ya bustani
yako na nje ya nyumba kwa ujumla kuhakikisha kuwa hakuna kitu ambacho
kitasimamisha maji na kusababisha mbu kuzaliana.
Kitu chochote ambacho ni chanjo cha
maji kusimama ni tatizo kwani mbu wanaweza kuzaliana hata kwenye maji
yaliyosimama katika mfuniko wa chupa ya soda (kisoda).
Kuwa makini na mabadiliko ya tabia
nchi. Ingawa tunasema ni ujio wa kipindi cha mvua za vuli lakini sio lazima
ziwepo kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya tabia nchi.
Kutunza bustani ni zaidi ya kuifanya
ivutie. Dondoo hizi zitakusaidia kuwa na busatani yenye afya ambayo inaweza
kuitunza yenyewe na hatimaye kupunguza kazi kwa upande wako. Utaifurahia vuli
huku ukisubiri kiangazi kije tena.
Nifuate instagram @vivimachange
No comments:
Post a Comment