Tuesday, November 1, 2016

Namna ya kuchagua mapambo ya ukutani

Inapofikia wakati wa kutoa nje ubunifu ulio ndani mwetu, wa namna ya kupendezesha nyumba zetu, basi sehemu nzuri ya kuonyesha kipaji chako ni kwenye kuta. Onyesha utambulisho wako wa sanaa kupitia kuta.

Mapambo ya kisasa ya
kupendezesha kuta ni pamoja na vitu kadhaa kama vile picha, fremu, michoro, saa, vioo, shelfu, vitundikio, stika, wallpaper na mengine mengi. Kutokana na wigo huo mpana wa mapambo unayoweza kutumia ukutani, ubunifu wako ndio kikomo chako. Unaweza ukachanganya kila moja ya mapambo haya katika eneo lolote la nyumbani kwako  iwe ni sebuleni, korido, chumba cha mtoto, cha wageni bafuni na kadhalika.

Baada ya kuyafahamu mapambo unayoweza kupendezeshea kuta za nyumbani, unachotakiwa kufahamu ni namna ya kuyachagua huko yanapouzwa au hata kutoa oda ya kutengenezewa.

Chagua sanaa kwa ukubwa utakaotosha ukuta fulani. Pambo ambalo ni kubwa sana litauzidi nguvu ukuta na lile ambalo ni dogo sana litamezwa na ukuta. Chagua pambo ambalo litaleta uwiano na mahali unapotaka kulitundika. Pambo linapokuwa kubwa ndivyo linavyohitaji ukuta mkubwa na kinyume chake pia ni sahihi. Pima eneo unalotaka kutundika pambo na kuacha nafasi ya kutosha kati ya moja na lingine ili yasionekane kurundikana.

Chagua pambo ambalo linaendana na madhari ya chumba kwa kuangalia rangi kuu mbili ambazo zimeshamiri (zinachomoza zaidi ya nyingine hata kama haziko eneo kubwa) katika chumba na uchague pambo la ukuta ambalo lina rangi hizo. Kumbuka kuwa lengo sio saresare hapana, ila kuchagua pambo lenye rangi moja kati ya rangi kuu chumbani inatoa ujumbe kwamba hilo pambo linatakiwa kuwa katika mazingira hayo.

Kama pambo ni picha ya ukutani ni vyema ujue kuwa fremu pana na yenye rangi ya kuwaka inaficha picha ya ndani yake, na kinyume chake pia ni sahihi. Kwahivyo fahamu lengo lako kama ni je, unataka picha ya ndani ionekane zaidi au unataka fremu iliyozungushia picha ndio ionekane zaidi.

Utaweza kufikia suluhisho la kununua pambo fulani baada ya kuona mapambo ya mitindo na miundo mingi tofauti tofauti. Angalia kwenye majarida, mitandao, madukani, makumbusho  na kwa wachoraji aina mbalimbali ya sanaa za ukutani kabla ya kufikia uamuzi wa unayoihitaji.

Jambo lingine la kufahamu ni kiasi cha mwanga kilichopo mahali unapotaka kutundika pambo. Hakikisha mwanga ni wa kutosha kuliwezesha pambo lako lionekane. 

Chagua sanaa yenye kuonekana vizuri kama ni picha iwe angavu vya kutosha toleo la mwanzo na sio iliyorudufishwa mara kadhaa.

Kama unatengenezesha saana yako kwa msanii hakikisha kuwa ni ambaye unaamini kazi zake ili ukae mkao wa kula ukisubiri pambo ambalo hakika ukuta wa nyumbani kwako utapendeza!

No comments:

Post a Comment