Thursday, October 31, 2013

My article for newspaper: Fenicha za chumba cha chakula

Kuwa na chumba cha kulia chakula katika eneo lolote la nyumba yako ni baraka. Kuwa na chumba cha kulia chakula chenye ukubwa wa kutosha kuweka fenicha zinazotakiwa kuwa kwenye chumba hiki ni ukweli kuwa itakuwezesha na kukuongezea ubunifu wa kupamba ndani mwako.

Fenicha za muhimu zaidi zinazotakiwa kuwa katika chumba cha kulia chakula ni meza na viti vyake, lakini hata hivyo kama una nafasi ya kutosha unaweza kuweka kabati la vyombo kwa ajili ya matumizi na mapambo.  Mapambo kwenye chumba cha kulia chakula yawe machache sana ili kuondoa mrundikano na kuacha sehemu kubwa ya familia.

cha chumba cha kulia chakula ni meza, ichague kwa uangalifu kutoka za pembe nne, duara au yai. Amua kama unataka ya viti vinne, sita au nane. Kimsingi umbo na nafasi ya chumba cha kulia chakula lazima itizamwe kabla ya kuamua umbo la meza inayotakiwa kuwa hapo. Isiwe kubwa kiasi ambacho itadumaza eneo la chumba wala isiwe ndogo kiasi ambacho itazama ipotelee.

Fikiria ni viti vingapi unahitaji kwenye meza ya chumba chako cha kulia chakula, mara nyingi ukweli huu utategemea na aina na ukubwa wa meza utakayonunua. Kama unajisikia kuwa viti vinne vitakidhi hitaji lako, fikiria meza ya duara au pembe nne. Pia fikiria kama utahitaji vile viti vyenye mikono kwenye meza yako ama laa; unaweza hata ukaamua kuchanganya hapa; weka viti vya mikono kwenye pande zile fupi za meza zinazotizamana halafu vile visivyo na mikono weka pande ndefu. Pia fikiria urefu na uzito wa viti, vinatakiwa kuwa na urefu na upana wa kutosha kwa ajili ya kukaa na kujisikia burudani na wakati huo huo visiwe vyepesi ili visisogee sogee kila mara.

Kama umebahatika kuwa na nafasi ya kutosha kwenye chumba chako cha kulia chakula weka kabati la vyombo. Makabati ya vyombo ya kwenye chumba cha chakula yako ya aina nyingi mno, lakini karibu yote yana milango ya vioo na mashelfu kwa ajili ya kuona kirahisi vilivyomo.  Kabati la vyombo katika chumba cha kulia chakula lina faida tatu ambazo ni sehemu ya nyongeza ya kuhifadhia vyombo vyako hasa vile ambavyo ni maalum na vinatolewa kwa matukio maalum na kwa wageni maalum. Pili, ni mahali pa nyongeza pa  kupakulia chakula hasa wakati unapoburudisha, unaweza ukahifadhia vinywaji na pia nafasi ya kuweka bufee na saladi na hata baadhi ya vitafunwa. Tatu ni mahali utakapoweza kuweka mapambo yako. Unaweza kuonyesha mapambo yako ya kichina, vyombo vya glasi na hata kuhifadhia vitambaa vya meza ambavyo havitumiki kwa wakati huo. Kumbuka kuwa makabati haya yanaweza kubuniwa kuendana na eneo unalotaka kuweka na matamanio yako.

Wakati hakuna njia mbaya au nzuri ya kupanga vilivyomo ndani ya kabati la vyombo la kwenye chumba cha kulia chakula; kuna njia za kimkakati za kupamba ambazo zinaleta mvuto. Kusanya vifaa vyote unavyotaka kuweka kwenye kabati na vipange mbele yako sehemu tambarare. Nyanyua kimoja kimoja upange vifaa vinavyovutia zaidi iwe ni vya glasi, kioo au seramiki kwenye shelfu la kabati lililo usawa na macho yako. Vifaa vikubwa vianze kwa ndani karibia na kuta na vile vidogo vipange karibia na mlangoni.
Vifaa vilivyobakia vipange kwenye mashelfu mengine kwa mtiririko huo huo wa hapo juu. Ongeza baadhi ya vifaa ambavyo kwa namna fulani vipo nje ya kawaida, lakini bado vina mvuto. Hii itafanya muonekano wa kabati lako uvutie. Kwa mfano, picha ya fremu ya wanafamilia inafaa, au mpira au mdoli wa kuvutia, utafanya ule mpangilio wako uwe na mvuto. 

Ongezea vifaa vya msimu kulingana na majira ya mwaka. Kwa mfano, kama ni karibia na krismasi weka mapambo machache kwenye shelfu au karibia na siku ya wapendanao weka kadi nzuri za valentine kuongeza mguso wa rangi kwenye kabati lako.

Sanaa chache za maonyesho zilizochaguliwa, na mwanga wa kuvutia vinaweza kuwa ndio mapambo machache tu ambayo chumba chako cha kulia chakula kinahitaji. Kama kuta zinaonekana kuwa tupu zivalishe kwa fremu za picha za maakuli lakini hakikisha unaweka chache sana kuondoa mrundikano kwenye chumba hiki. Zaidi ya yote chumba chako cha kulia chakula ni kijiwe chako na familia yako kutumia muda wenu wa thamani pamoja.

Kumbuka ili utumie hela yako kwa busara, wakati wa kuchagua fenicha za chumba cha kulia chakula, unapaswa kuwa makini na vigezo vikuu vitatu. Kwanza ni zingatia umbo, ukubwa na vipimo vya chumba au hapo mahali pa kulia chakula, na pili mandhari unayotaka kutengeneza kwamba ni ya kimapumziko, kitamaduni, rasmi na orodha inaendelea, tatu ni idadi gani ya viti unayotaka meza iwe navyo na mwisho ni aina ya mapambo ambayo unadhani chumba kinahitaji. Kutegemea na nafasi na pia mahitaji binafsi, amua ni fenicha zipi hasa unahitaji kwa ajili ya chumba chako cha kulia chakula.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk



No comments:

Post a Comment