Wednesday, October 19, 2016

Namna ya kupendezesha nyumba ionekane ya gharama ila kwa bajeti ndogo

Wengi tunapenda ndani ya nyumba tunamoishi kuwe kuna mvuto. Ila bado tunajiuliza kama itawezekana kwa bajeti iliyopo ambayo bila shaka ni ndogo. Wala isikupe shaka! Katika makala hii nitakuonyesha njia tano ambazo zitapafanya nyumbni kwako paonekane kwa gharama bila bajeti ya
kutisha. 

Paka kuta rangi za mwanga
Rangi kama nyeupe, krimu na nyingine nyingi ambazo ni nyepesi na safi zinaipa nyumba muonekano wa kiwango cha juu. Mbali na hilo ni kuwa pia rangi za namna hii zinakuwezesha kukua na nyumba yako. Maana yake ni kwamba pale utakapotaka kukipa chumba muonekano mpya itakugharimu kazi ndogo tu aidha ya kubadilisha fenicha au kuongezea mapambo madogo ambayo huwa nayaita vitupio.

Fahamu thamani ya unapowekeza hela yako
Hebu fikiria wakati unaponunua vitu vya kuuvika mwili kama vile nguo, viatu na mapochi kwa wewe mwanamke. Vitu ambavyo unahitaji kuwekeza hela ya maana ni vile vyenye viwango, visivyoharibika ndani ya muda mfupi. Vivyo hivyo kwa kwa ajili ya nyumbani kwako unapoishi! Wekeza kwenye vitu vile vya thamani ambavyo vina haki ya kutumia hela yako ya nyongeza kwa mfano sofa, meza ya chakula (na viti vyake) na kitanda.

Vichache ni vingi
Ni muhimu sana kuwa na filosofia hii kichwani wakati unapohitaji kununua vitu kwa ajili ya nyumbani kwako. Ama kiwe ni kwa matumizi au kwa kupendezesha au vyote hakikisha kuwa kila kitu unachoweka ndani ya nyumba yako umekichagua kwa umakini na kinapaswa kuwepo.
Tunapoondoa vile vitu ambavyo havihitajiki, tunavipa vile ambavyo ni muhimu nafasi ya kung’ara.
Kwa mfano huna haja ya kubandika wallpaper zenye maua na michoro lukuki badala yake pamba ukuta (kwa mfano ule wa nyuma ya sofa) kwa kutundika picha moja kubwa. Au pia badala ya taa nyingi nyingi weka chandalia moja kubwa ya kuning’inia katikati ya chumba.

Tafiti kwa kina
Kabla hujanunua kitu cha nyumbani iwe ni kitanda, kochi, pazia na kadhalika hakikisha kuwa umepata kilicho bora na kwa bei nafuu. Kwa mfano, gharama ya kitanda cha chuma cha ukubwa wa futi 5 kwa 6 ni tofauti kwa kila mtengenezaji japo bidhaa ni ile ile. Au pia gharama inaweza kupungua kutokana na muundo wa kitu japo ukubwa unakuwa ni ule ule unaohitaji na pengine badiliko la muundo haliathiri matumizi ya bidhaa hiyo. Tukirudi kwenye mfano huo huo wa kitanda cha chuma yawezekana muundo fulani unahitaji vyuma vingi wakati mwingine hauhitaji kiasi hicho, kwahivyo moja kwa moja unakuta bei yake inakuwa chini na ukiangalia dhumuni lako la kupata kitanda cha kulalia linakuwa limetimia bila kujali muundo. Unapopendezesha nyumba yako ni vyema ukaangalia kila upande wa namna ya kupata kitu chenye ubora lakini kwa bei nafuu.

Jaladia vyema

Ili nyumba yoyote ionekane ya gharama au kifahari hata kama sio, na imekamilika ni lazima uwe umejaladia kila eneo. Jaladia zulia sebuleni, vyumbani na koridoni, mito kwenye sofa na vitanda na hata madirisha kwa pazia ndefu.

Namna hii nyumba inaonekana imekamilika na ya kifahari.

No comments:

Post a Comment