Tuesday, October 25, 2016

Fimbo nzuri za kutundikia pazia zina vigezo hivi

Kwa takriban miaka 10 iliyopita matumizi ya fimbo au wengine wanaita bomba imekuwa ni njia ya kawaida zaidi ya kutundikia pazia. Zinafanya utundikaji uwe rahisi na uvutie.

Unapotaka kununua fimbo nzuri za pazia zingatia vigezo hivi.

Malighafi
Zipo fimbo zilizotengenezwa kwa plastiki, chuma, aluminiam na miti.
Kwa uimara na kudumu muda mrefu, fimbo nzuri za pazia zinatakiwa zile za
jamii ya chuma (ni pamoja na aluminiam). Imeshathibitika kwamba fimbo za miti zina tabia ya kujikunja baada ya kipindi laa sivyo uwe unazigeuzageuza kila wakati. Je, ungependa kujiongezea kazi hiyo? Bila shaka hapana.

Muundo wa pazia
Uchaguzi wa fimbo unategemea na aina ya utundikaji kama vile pini, bangili na pia uzito wa kitambaa kilichotengenezea pazia hizo.
Aina karibia zote za fimbo zinauzwa pamoja na vitundikio vyake. Hii inamaanisha ni lazima ujue muundo wa utundikaji wa pazia zako kabla hujanunua fimbo.

Rangi
Jambo lingine la kuangalia kwenye fimbo nzuri za pazia ni rangi. Angalia rangi nzito zilizopo chumbani unapoenda kuchagua rangi ya fimbo za pazia. Ila kwa upande mwingine kama unataka pazia zishamiri zaidi kuliko fimbo basi cha kufanya ni kununua fimbo ambazo rangi yake inafanana na ya kuta. Kwa mfano kama rangi ya kuta ni nyeupe na ukanunua fimbo nyeupe na ukaweka pazia za bluu bila shaka pazia ndio zitakuwa kitovu cha chumba.
Pia yawezekana una viti au fenicha zenye finishing za rangi ya brasi au dhahabu. Unaweza kununua fimbo za pazia zenye finishing ya rangi hizo ili kutengeneza ujirani wa rangi.
Fimbo nyeusi za chuma hazitapendeza kwenye pazia nyepesi za rangi za mwanga.

Vishikizo
Ni vyema kuwa makini na vishikizo vinavyoshikilia fimbo na ukuta. Kuna fimbo ambazo vishikizo vyake ni vyembamba sana kiasi kwamba baada ya muda wa kufunga na kufungua pazia mara kwa mara, fimbo inainama na hatimaye eneo la kishikizo kukatika. Kwa hivyo pamoja na kujali muonekano wa fimbo ni vyema uwe makini pia na muundo wa eneo la kishikizo.

Zisizopitwa na wakati au zilizo kwenye fasheni?
Fimbo nzuri ni zile zisizopitwa na wakati kuliko zilizo kwenye fasheni. Fimbo zisizopitwa na wakati ni simpo na nyembamba sizizo na madoido mengi. Zile ambazo zina mbwembwe nyingi zinakuwa ni za kwenye fasheni na hazikawii kupitwa na wakati kama fasheni nyingine zozote.

Za eneo moja zifanane
Kama uko kwenye eneo au chumba ambacho unaona madirisha yote kwa wakati mmoja basi inapendeza fimbo zikiwa zinafanana. Na hasa kama eneo kubwa la nyumba liko wazi (kwa mfano hakuna ukuta unaotenganisha sebule na chumba cha chakula au jiko) basi wazo la fimbo na pazia za kufanana ni zuri. Na kwenye maeneo haya wapo pia wanaopenda kuonisha rangi za fimbo na za majumba yanayobebea taa.


Ehe, hebu niambie kuhusu fimbo za pazia za nyumbani kwako. Je ulijuaje kwamba ndio nzuri zinazokufaa? Najua una vigezo ambavyo sijavisema hapa.

No comments:

Post a Comment