Saturday, October 22, 2016

Uzuri wa zulia lenye michoro kama ya kwenye ngozi ya wanyama

Kupendezesha nyumba kwa vitu vyenye rangi kama za michoro iliyopo kwenye ngozi za wanyama hakujawahi kupitwa na wakati. Kama unapenda mazulia lakini hujui namna ya kupamba kwa kutumia yale yenye michoro kama ya kwenye ngozi za wanyama, kwenye makala hii utazijua mbinu zote.

Mazulia haya kwa muonekano wake tu yana uzuri wa
asili hasa kwa msisitizo wa rangi zake za wanyama kama vile pundamilia, chui, twiga na duma ambapo rangi hizo ni nyeusi, nyeupe na udongo. Rangi hizi ni rahisi kushirikiana na zingine zozote zilizopo kwenye chumba au sebuleni. Bila shaka utakubaliana na mimi kuwa mazulia yenye michoro ya pundamilia ndio yako mengi na yanayopendwa zaidi yakifuatiwa na yale ya kichuichui. Wakati huohuo yakiwa ni ya maumbo mbalimbali ambayo ni pembenne, duara na yale ya umbo kama ngozi ya mnyama iliyochunwa na kuwambwa.

Kutokana na wigo huu mpana wa maumbo, rangi na michoro, inawezekana kabisa kupata ambalo ni sahihi kuleta ushirikiano kati ya rangi na staili ya chumba.

Kwanza kabisa ni lazima ufahamu ni katika muonekano au hali ipi unaweza kutumia zulia lenye michoro kama ya kwenye ngozi za wanyama niliowataja hapo juu.

·        Ni katika hali ile ambayo chumba fulani kinaonekana kupoa. Fenicha na rangi za kuta na vitu vingine zinahitaji kuchangamshwa zaidi.

·        Ni katika muonekano ambao sebule yako inahitaji miguso ya kumalizia ambapo itaifanya ionekane kuwa na ushirikiano na timilifu.

·        Ni katika muonekano ambao umeweka zulia la ukuta kwa ukuta au lolote kubwa lakini la rangi moja kwahivyo unahitaji mengine madogo ya kutupia ili kuongeza rangi

·        .Ni katika muonekano ambao mtindo wako wa maisha unahitaji alama ya kukuongezea nguvu na tumaini.

Katika hali hizi nilizoainisha hakuna zulia lenye michoro na rangi nyingine litakaloweza kukidhi hitaji lako. Kwahivyo sahau mazulia yenye maua ambayo utakutana nayo madukani au ambayo umeshaona kwenye nyumba za wengine. Unahitaji zulia changamfu, nalo ni lenye michoro kama ya kwenye ngozi za wanyama.

Sebule yako inahitaji zulia la namna hii litakalosisimua watu pale wanapoliona au kuweka miguu yao juu yake. Wigo mpana wa mazulia ya wanyama yaliyopo yanakupa uchaguzi katika kila eneo la nyumba yako. Kwahivyo unaweza kupeleka hiyo hisia ya msisimko kutoka chumba kimoja hadi kingine.

Iwe unahitaji lililo pana kujaza chumba kizima, au dogo tu la kuongeza mguso wa rangi  kwenye eneo dogo fikiria zulia la rangi kama ya kwenye ngozi za wanyama kuongeza kiungo, mvuto na nguvu katika kupendezesha ndani mwako. Mazulia haya yanaendana na aina yoyote ya fenicha na vinyago na hata staili ya upambaji iwe ni ya kiutamaduni, ya kisasa au mchanganyiko. Yanaweza kutandikwa juu ya mazulia mengine, sakafu za marumaru, tarazo na hata ya mbao.

No comments:

Post a Comment