Inawezekana
umepanga nyumba yenye chumba kidogo cha kulala. Na kama tujuavyo nyumba nyingi
za kupanga hazina ile mifumo ya kukuwezesha kupangilia vitu vyako kama vile
makabati ya nguo na kadhalika. Hata hivyo unaweza kuishi vizuri mno kwenye
chumba hicho kidogo endapo utafahamu jinsi ya kukiweka katika muonekano sahihi.
Kuna
mbinu nyingi ya kukipanga chumba cha
kulala kikaonekana kuwa na nafasi kubwa
endapo ndicho unachojaribu kwa sasa. Nimebahatika kutembelea nyumba nyingi na kwa kadri ninavyojua kuna njia kuu nne
muhimu zinazoweza kukupa matokeo mazuri ya kuwa na nafasi ya kutosha ndani ya
chumba kidogo cha kulala bila chumba hicho kuonekana kuwa na mrundikano.
Njia
ya kwanza ni kuweka kitanda karibia na ukuta halafu unakamata fursa ya huo
ukuta wa kichwani mwa kitanda. Ni ukuta ambao unakaa tu bila kazi yoyote na
unafaa kuwekea shelfu au kabati (endapo utaweka na milango) kwa ajili ya
kuhifadhia baadhi ya vitu kwani sio sehemu ambayo wala unapita kwamba shelfu
zitakukera. Hakikisha kuwa vitu vya kuhifadhi kwenye shelfu hizi ni vile
ambavyo hata kwa bahati mbaya vikikudondokea ukiwa umelala havitakuumiza, kwa
mfano nguo, shuka na taulo.
Njia
ya pili ni kwa kuwa na stendi rahisi kwa ajili ya kutundikia pochi, tai,
mikanda, skafu na vingine vingi vinavyowezekana kutundikwa kwa mtindo huu.
Stendi hii huwa ina uwezo wa kusimamishwa kwenye kona na kutundikwa vitu vingi sana na huku ikichukua eneo dogo
tu. Na kwa upande wa nguo za kutundika jipatie stendi nyingine kwa kazi hiyo.
Maana zile za kukunja tayari una shelfu za kichwani mwa kitanda.
Ukipiga
mahesabu ya haraka utakuwa umebakiwa na vitu kama masanduku na viatu ambavyo
pengine huna pa kuvihifadhi. Ukisema uongeze raki ya viatu inaweza kusababisha
muonekano wa mrundikano kwani tayari kuna stendi ya nguo na ya pochi. Habari
njema ni kwamba kuna mvungu wa kitanda ambapo pako tu wazi. Tumia mvungu
kupanga viatu na kule kwa mbali kabisa hifadhi masanduku na boksi za vitu
usivyotumia mara kwa mara. Kama utakuwa umefikiria toka mwanzo unaweza kuagiza
kitanda chenye miguu mirefu ili kufanikisha zaidi ongezeko la nafasi mvunguni.
Kwa
ufupi ni kwamba unavyokuwa na maeneo mengi ya kuhifadhi vitu ndivyo nafasi ya
chumba inavyoonekana kubwa. Tumia eneo la nyuma ya mlango kutundika mfuko
(mithili ya ile ya viatu) wenye
vyumba vingi vidogodogo kwa ajili ya kuwekea vitu kama vile chanuo vipodozi na
vibanio huku kioo cha kujitazama ukiwa umekichimbia ukutani kwahivyo unajikuta
wala huna haja ya dressing table itakayokumaliazia nafasi bure.
No comments:
Post a Comment