Monday, October 3, 2016

Grauti za rangi zinavyopendezesha eneo lenye marumaru




Sio siri kuwa marumaru imekuwa ni malighafi ambayo inapendwa na wengi kwenye sakafu na kuta kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhimili uchafu na unyevu. Kile kinachounganisha marumaru moja na nyingine kinahusika sana kwenye muonekano na usafi wa sakafu au ukuta wa marumaru.

Mhandisi David Sembuyagi wa kampuni ya Ujenzi Bulk Build simu 0715 630 073 anatuelezea jnsi malighafi ya
grauti ambayo ni kiunganishi cha marumaru moja na nyingine inavyoweza kuwa ya rangi na kuchangamcha eneo lililowekwa marumaru hizo.

Japo ni ukweli kuwa wengi hawaweki umuhimu wa rangi ya grauti (aidha kwa kutokujua kwamba zipo za rangi mbalimbali) hadi pale inapokuwa mbaya kwa mfano kuwa na doa, kuwa na mpasuko au kubadilika rangi kutokana na uchafu ndipo wanaanza kuona ukakasi.  Grauti inatakiwa kuheshimiwa, zaidi ya kuunganisha marumaru inafanya sakafu, ukuta au kauta kuwa imara. Ni lazima ichaguliwe kwa umakini kuendana na mtindo na rangi ya marumaru unazotaka kuweka, na vilevile maeneo ambayo zinawekwa na muonekano mzima wa mwisho uliokamilika wa eneo hilo.

Kama nilivyosema kuwa wengi hawana habari kuwa kuna grauti za rangi mbalimbali, ukienda kwenye duka la vifaa vya ujenzi na kuulizia grauti, bila shaka utapewa ile iliyozoeleka ya rangi ya kijivu inayokaribiana na saruji. Ukweli ni kwamba ulimwengu wa grauti umepanua rangi na malighafi nyingi za grauti ambapo sasa kuna wigo mpana mno wa rangi za marumaru na za grauti vilevile. Unaweza kupata grauti ya rangi yoyote ile unayotaka.

Kama unaweka marumaru zenye rangi ya jiwe au saruji, unaweza kuoanisha na rangi ya grauti ili kutengeneza muonekano wa kufanana. Ila pia kama unataka kuonyesha muundo wa marumaru zako, au umbo la kipekee na kona za marumaru chagua rangi ya grauti ambayo haifanani na ya marumaru hizo.

Njano ni moja kati ya rangi za kuwaka ambazo mara nyingi hazitiliwi maanani tunapopendezesha nyumba. Grauti ya rangi ya njano na marumaru za rangi nyepesi zinavutia bafuni na vilevile zinasaidia kuongeza mwanga. Usikariri dhana kwamba rangi za kuwaka zinaonekana za kitoto, kwani sio kila mahali inakuwa hivyo.

Kama marumaru ni za rangi iliyofifia una uwezo wa kuzichangamsha kwa grauti ya rangi nzito.

Grauti ya rangi ya silva inaweza kudhaniwa haina mashiko lakini imetulia mno hasa ikichanganywa na marumaru nyeupe.

Chagua grauti ya rangi sahihi kuendana na chumba, mahali kama ni sakafuni, ukutani au kaunta na pia mlazo, rangi na muundo wa marumaru husika.

Grauti ina matokeo makubwa katika muonekano wa kazi ya marumaru iliyokamilika.

No comments:

Post a Comment