Wednesday, October 12, 2016

Dondoo za kupendezesha pembeni mwa luninga

Kupendezesha pembeni mwa luninga inaweza kuwa changamoto na pia baadhi wanadhani kwamba wakishaiweka iwe ni ukutani au juu ya kabati basi inatosha. Bahati mzuri ni kwamba ujio wa luninga za vioo flati na nyembamba yaani zisizo na kichogo kama zile za zamani, unafanya kazi ya kupendezesha pembeni mwake iwe rahisi.
Hapa hebu tuangalie dondoo tano za
namna ya kupamba  pembeni mwa luninga.

Kuificha
Usishange kwani kuficha nako ni njia ya kupendezesha. Kuna wakati ukitaka kupendezesha pembeni mwa kitu inakupasa kukificha kitu hicho. Unaweza kuificha luninga kwa kuiwekea kabati ambalo lina mlango wa kufunguka kwa kuteleza ambapo ukiwa ni muda unataka kutazama/kutumika unafungua huo mlango ambapo unafunguka kwa kuzama ndani ya kabati aidha kwa upande wa juu au pembeni. Na wakati haitumiki mlango unafunguka na kuificha isionekane na eneo kubaki kama lina kabati tuu. Njia hii ni rahisi kwa zile nyumba ambazo luninga inatizamwa katika muda maalum tu yaani haitizamwi kila wakati ndani ya masaa ya siku.

Iweke juu ya stendi rahisi lakini yenye mvuto.
Unapoamua kuangalia luninga yako ikiwa juu ya fenicha, epuka kwenda na makabati makubwa ya kawaida na badala yake uchague fenicha ambayo ni ya kipekee ili kutendengeza kitovu cha sehemu luninga ilipo na kuleta mvuto wa kipekee. Unaweza kupata wazo la fenicha hiyo kupitia majarida na mitandao inayoelimisha namna ya kupendezesha eneo la luninga na ukapeleka kwa fundi seremala au chuma wa mtaani akakutengenezea kwa mfano huo au hata kuboresha zaidi. Bila shaka inawezekana kuwa ni gharama nafuu kuliko hata makabati ya luninga ya kawaida na hivyo  kuongeza mvuto zaidi mahali luning ilipo.

Weka shelfu za kuwekea mapambo
Unaweza kuweka shelfu za wazi chini au pembeni mwa ilipo luninga yako ili kuweka mapambo na sanaa ndogo ndogo kwenye hizo shelfu. Hii ni njia nzuri endapo itafanyika kwa usahihi.

Tundika picha na fremu kuizunguka
Nadhani kati ya dondoo zote hii ndio nzuri na inayotumiwa na watu wengi zaidi. Kuifanya luninga yako ilipo pawe na mvuto unachotakiwa kufanya ni kutundika picha na sanaa kuizunguka ambapo mapambo hayo yanatakiwa kuendana na muonekano wa luninga. Kwa mfano luninga nyingi zina fremu nyeusi, hakika itavutia ikizungukwa na picha zenye fremu nyeusi na nyeupe. Picha hizi unaweza kuzitundika juu na pembeni kwa luninga, na ikiwa ni ile ya kupachikwa ukutani hakuna shaka muonekano utavutia zaidi.

Izungushie fremu
Kuizungushia luninga yako fremu ni njia nzuri ya kuiongezea utambulisho na kuifanya imvutie mtazamaji kuangalia eneo lile.

Ehe msomaji wangu, je unatumia njia

mojawapo kati ya hizi kupendezesha 

eneo ilipo luninga yako? Nitafurahi

kusikia toka kwako.

No comments:

Post a Comment