Friday, June 26, 2015

Jinsi ya kuhifadhi mvinyo kwa kutumia susu za kuhifadhia (wine racks)

Susu ya mvinyo ni njia rahisi na ya gharama nafuu kabisa ya kuhifadhi chupa za mivinyo na wakati huohuo zikiweka mivinyo yako katika muonekano wa kimapambo. Susu hizi ni kwa ajili ya muonekano ila sio kwamba zinakuja na jokofu hapana. Katika kuandaa makala hii nimefanya mazungumzo na Jack ambaye ni mtaalam wa kuhifadhi mvinyo na afisa mauzo katika duka la mivinyo. Anasema kuwa kama wewe
huna shauku ya kunywa mvinyo haraka haraka na kuumaliza huna haja ya kuhifadhi mvinyo wako kwenye jokofu. Susu ya kuhifadhia mivinyo ni kwa wale watumiaji na wakusanyaji wa mivinyo bila kujali muda au kipindi na hivyo wanapendelea kuwa na hifadhi ya mivinyo mbalimbali muda wote nyumbani kadri wanavyoipata.

“Kwa lengo lolote kama wewe ni mtu wa kukusanya mivinyo na unaenda kuitumia polepole nyumbani, haiharibiki pale inapokuwa imehifadhiwa kwenye susu yake ndani ya miaka mitatu  hadi mitano,” anasema Jack.
 
Kuwa na eneo la kuhifadhi mivinyo kwenye nyumba yako inasikika vizuri, na kwa maana hiyo hutajali kuwa na susu ya kuihifadhia. Kimsingi susu za kuhifadhia mivinyo ni kwa wale wanaofurahia kuwa na mivinyo kila wakati nyumbani, anasema Jack. Kwa hawa wanaopenda kunywa mvinyo wakati wowote watakapo, susu ya mvinyo sio tuu itasaidia kufanya kaunta ziwe safi, yaani kutorundikana hizo chupa, lakini pia kufanya muonekano wa kuvutia hapo mahali utakapoamua kuweka susu yako, iwe ni jikoni, sebuleni au chumba cha chakula. Na wakati huo huo kuzuia ajali ya chupa kugongana na kuvunjika

“Eneo lenye susu za mvinyo limekuwa kitovu cha jicho kwenye nyumba za wapenda mvinyo,” anasema Jack. Na unapoamua kuburudika au kuburudisha nyumbani usitanie, zile nyakati za kuwa na kisusu cha mivinyo kidogo ndani ya kabati la sebuleni zinaishia. Sasa kuna susu za kusimama peke yake na ambazo zinatengenezwa kama pambo la ndani vilevile, kama hupendi mambo haya huwezi kuelewa. Na pia kuna zile ndogo za kuweka juu ya kaunta au meza.

Jack anasema kama unataka susu ya mivinyo yenye vigezo vyako ni vyema ukatengenezesha. Kutoa oda ya susu ya namna hii itasaidia kupata mtindo ule unaotaka na wa kuweza kuenea kwenye eneo unalotaka kuiweka; wakati ambapo zile zilizotengenezwa tayari zinapatikana kwenye vipimo maalum tu.

Kwenye kuchagua susu za mvinyo kuna aina nyingi. Zipo za maumbo mbalimbali na pia zenye visehemu vya kutumbukiza chupa kwa uwingi mbalimbali, hivyo hutabanwa na aina na mtindo wa susu unayotaka.
Kwa ajili susu za mivinyo zinatumika kuhifadhi mivinyo kwa miaka mitatu hadi mitano baada ya kuinunua, kuamua ni ukubwa gani unahitaji ni lazima ujue ni mivinyo mingapi utanunua/utakunywa kwenye kipindi hicho, hivyo unaweza kukisia ni chupa ngapi za mivinyo utahifadhi kwenye susu yako. Je susu yako utaiweka juu ya meza, kaunta, unaitundika ukutani ama inasimama peke yake.

Susu za mvinyo zimetengenewa kwa malighafi  mbalimbali kama vile chuma cheusi, chuma cha silva, mbao zilizopakwa rangi na mbao zilizoachwa asilia bila rangi. Ni ipi unapenda? Susu inayopendeza ni ile ambayo kila chupa ina kisehemu chake cha kuhifadhiwa.

Kuna vitu vinavyoambatana na susu za mvinyo, kama vile kimeza, sehemu ya kutundikia glasi za kunywea,  droo au shelfu. Fikiria kama utavihitaji pamoja na susu yako.

Sasa, kumbuka kuwa susu za mvinyo zinauweka mvinyi kwenye joto la chumba susu ilipo, kwa ajili tumeshasema hii susu haina jokofu. Hii ina maana mvinyo wako unaweza kuwa na hali ya uchungu baada ya miaka mitatu hadi mitano –hii haina maana kuwa utashindwa kuunywa. Ila sasa baada ya hapo unatakiwa  kufikiria mara mbili kabla ya kuuweka kwenye jokofu. Nilipokuwa na Jack nimemuuliza kuwa kama hilo ni wazo zuri ama laa. Jack ametoa changamoto hii kwa suala la kuweka  mvinyo kwenye jokofu.

“Kuweka mvinyo wako kwenye jokofu kunahusu kila kitu kwenye jokofu ambacho kinatoa harufu,” anasema Jack. “Mfuniko wa mvinyo ni kitu cha asili, kwa hivyo kinapitisha vitu kuingia na kutoka. Maana yake ni kama kuna kipande cha sangara au kitunguu kwenye jokofu, ni ukweli kuwa mvinyo wako unaenda kuchukua harufu au ladha za kitunguu au sangara”
Ukifikiria ni ladha ipi mvinyo wa kitunguu utakuwa nayo, unaweza kuepuka kuweka mvinyo wako kwenye jokofu. Badala yake amua kuweka kwenye chombo chenye barafu. Au kuwa na jokofu dogo la kuhifadhi mwinyo pekee, hapo ni kama miaka imeenda na mivinyo yako imeanza kuwa michungu. Mvinyo ambao haujafunguliwa unaweza kudumu hadi miaka 100, anasema Jack.

Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment