Wakati Watanzania wakiendelea kufuatilia kwa shauku kubwa
msururu wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaojitosa kwenye mbio za
kusaka ridhaa ya chama chao kuteuliwa kugombea kiti cha urais Oktoba 25, mwaka
huu, mitandao ya kijamii imevamiwa na mafundi wa kutunga na kuumba habari na
sasa hata Umoja wa Ulaya na Dk. Harrison Mwankyembe wamechomekewa mambo dhidi
ya Edward Lowassa.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Ofisa
Habari wa EU, Susanne Mbise, juu ya taarifa za kuwako kwa kauli ya Balozi wa EU
kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Lowassa na nia yake ya kuusaka urais, alisema
wamesikia taarifa hizo, lakini ukweli wa jambo hilo upo kwenye taarifa
waliyoweka kwenye mtandao wa Face Book ya Umoja huo.
Kadhalika, alituma kwa NIPASHE taarifa hiyo kwa njia ya
mtandao wa intaneti.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa
anayeshughulikia Siasa na Habari, Luana Reale wa kitengo cha habari, Balozi
huyo hajafanya mkutano wowote na mwandishi yeyote na kwa maana hiyo hajatoa
taarifa yoyote kwa vyombo vya habari.
Reale alisema kuwa tangu Juni mosi mwaka huu Balozi huyo
hayuko nchini kwani alisafiri kwenda makao makuu ya Umoja huo na hajarejea
nchini.
Alisema kuwa EU ina uhusiano mzuri wa muda mrefu na
Tanzania ambao umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana na kuaminiana.
EU inatoa taarifa hizo baada ya watu wasiojulikana
kusambaza taarifa za uzushi na uongo kwenye mitando ya kijamii wakidai kuwa
Rais Kikwete ameonywa kwamba Lowassa akipitishwa kuwania urais uhusiano wa
Tanzania na EU utaingia shakani na kwamba hawataisaidia katika miradi ya
maendeleo.
Wazushi hao walidai kuwa Lowassa ni mtuhumiwa namba moja
wa rushwa nchini na kutaja kuwa anahusika katika kadhia ya Richmond na NIC.
Wakati EU ikijiweka kando na uzushi huo, Dk. Mwakyembe
ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naye alijiweka kando na
taarifa za uzushi zilizokuwa zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimnukuu
kwamba ametoa taarifa kuhusu Richmond na kumwandama Lowassa.
Akihojiwa na redio moja nchini jana, Dk. Mwakyembe
aliwataka wanasiasa kuacha kujificha mgongoni mwake kwa lengo la kumshambulia
Lowassa.
“Taarifa ile haikuwa ya kwangu, ni upuuzi. Mnanijua
kwamba huwa sikurupuki. Mimi ni waziri wa Serikali ambaye naheshimu wadhifa
wangu, hivyo siwezi kuandika mambo kama hayo. Nilipigiwa simu hata na wenzangu
wakiniuliza mbona nimeandika maneno makali,”alisema.
Dk. Mwakyembe alisema kuwa hana sababu ya kuendelea
kujadili suala la sakata la Richmond kuhusu Lowassa na kuongeza:
“Kama ni suala la kashfa ya Richmond, jamani mbona
tulimtanguliza Mungu? Tulifanya kazi yetu kwa haki na ripoti ya Bunge ipo. Sasa
hakuna haja ya unafiki…unafiki wa watu kutaka kumsema Lowassa halafu
wanajificha mgongoni kwangu.”
Alisema kuwa amekwisha kukamilisha hatua za awali za
kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika ikiwamo Polisi Makao Makuu Kitengo
cha uhalifu wa kimtandao (Cyber Crime), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
ili waweze kubaini mtandao huo ambao ulianza harakati zake tangu Lowassa
atangaze nia.
“Siyo uungwana kuchezea majina ya watu wanaokosa ujasiri
wa kuelezea hisia zao hadi watumie majina ya watu wengine, mtandao huo nauona
kuwa ni hatari,” alisema na kuongeza kuwa huenda kwa sababu ya joto la uchaguzi
ndiyo maana suala hilo likapewa msukumo.
Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa amedhamiria kukomesha
tabia ya kuchafuana kupitia mitandao ya kijamiina ndiyo maana amekwenda Polisi
Kitengo cha Cyber Crime (Mkosa ya Jinai ya Mtandao) na TCRA, kulalamikia mchezo
huo mchafu wa kihuni na tayari.
Tangu Mei 30, mwaka huu Lowassa alipotangaza nia ya
kuwania urais kupitia CCM, limeibuka wimbi la mashambulizi dhidi yake.
Mashambulizi mengine yamekuwa yakitolewa ama moja kwa
moja au kwa kuzunguka makada wengine wa CCM waliotangaza nia ya
kutaka kuteuliwa na CCM kuwania kiti hicho.
Mbali na Lowassa makada wengine ambao wametangaza nia ni
pamoja na Stephen Wasira, Profesa Mark Mwandosya, Dk. John Magufuli, Frederick
Sumaye, Dk. Titus Kamani, Mwigulu Nchemba, Luhaga Mpina, Samuel Sitta na
Profesa Sospeter Muhongo.
Wengine ni Balozi Amani Karume, Balozi Amina Salum Ali na
Amos Siatemi. Msururu huo unatarajiwa kuongezaka kwani wengine wanatarajiwa
kutangaza nia na kuchukua fomu leo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment