Sunday, June 7, 2015

Mtoto wa Makongoro Nyerere anusurika kifo kwenye ajali...Chanzo cha ajali ni vumbi lililomzuia dreva

Julius Makongoro mtoto wa kada wa  CCM Makongoro Nyerere, aliyetangaza nia ya kugombea urais ni miongoni mwa watu watano walionusurika kifo wakiwa kwenye msafara wa mgombea huyo, kufuatia ajali ya  gari iliyotokea mkoani Kigoma.

Makongoro Nyerere hakuwepo
kwenye gari hilo lililopinduka  jana saa 4:30 asubuhi eneo la Mwilanvya wilayani Kasulu na kuwajeruhi  Julius aliyeumia kichwani, waandishi Evance Magige (30) wa magazeti ya Habari Corporation, Cyprian Msiba (35) wa  Chanel Ten aliyeumia mabega.

Wengine ni  Fikiri Marumba (35) Katibu Mwenezi wa CCM,  aliyejeruhiwa  sikio la  kushoto, dereva Ally  Tesha (37) mkazi wa Arusha. Julius ndiye alikuwa dereva wakati wa ajali.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Kigoma, hali za majeruhi  ni nzuri baada ya kutibiwa katika hospitali ya wilaya ya Kasulu na wanatarajiwa kuendelea na safari.

Kamanda Frednand Mtui, alisema gari lililopata ajali ni Toyota Land Cruiser hadtop na kwamba liliacha njia na kupinduka eneo hilo lililoko Mwilanvya barabara ya Kasulu- Kibondo.

Aidha alisema chanzo cha ajali ni vumbi lililomzuia dereva  kuona kikamilifu linalosababishwa na  magari hayo ya msafara kukaribiana kwenye njia hiyo yenye  vumbi jingi. Gari lililopata ajali lina  namba T188 BXG.

Mtui alisema msafara huo ulikuwa na magari matatu Alisema majeruhi baada ya kutibiwa na kuruhusiwa waliazimia kuendelea na safari yao ya kwenda Kigoma mjini.

Kamanda Mtui aliwataka madereva wageni wanapoingia mkoani Kigoma  kuwa makini  kwa sababu  barabara zake nyingi ni za  vumbi na zenye kona. Aliwashauri kupeana nafasi wasikaribiane  ili kila mmoja  aweze kuona nyuma na mbele pia.

Alisema hali ya gari hilo ni nzuri na wataendela na safari yao hadi Kigoma mjini kama walivyokusudia.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI


No comments:

Post a Comment