Haishangazi
jokofu kutoka kuwa katika hali ya usafi na mpangilio na mara moja kuhamia
kwenye mvurugano na harufu mbaya za vyakula vilivyoharibika ambavyo hata
havijulikani.
Lakini
ni kwa namna gani katika maisha ya nyumbani unavyoweza kuanza mchakato wa
kuweka mpangilio kwenye jokofu na friza? Kabla hatujaangalia hilo ni vyema
tukakubaliana katika mambo matatu ambayo ni; si kila familia inanunua vyakula vingi
vya
kuhifadhi kwa muda mrefu, ukubwa wa
familia unatofautiana kati ya moja na nyingine kwahivyo wingi wa vyakula kwenye jokofu nao ni
tofauti na jambo la tatu ni kwamba haya majokofu na friza yana miundo tofauti
tofauti. La kwako linaweza kuwa tofauti kabisa na la yule.
Baada ya kukubaliana hayo, sasa tuangalie dondoo hizi
kadhaa nilizokuandalia ili kuwezesha na pia kuendeleza hali ya mpangilio ndani
ya jokofu kwa ujumla, huku tukizingatia mambo hayo matatu hapo juu.
Sio kila chakula
ni cha kuhifadhi kwenye jokofu
Ni
vyema tutambue kuwa kuna vyakula ambavyo tunaweka kwenye jokofu kutokana tu na
mazoea lakini kiuhalisia vinafaa kuhifadhiwa katika halijoto ya kawaida iliyopo
hapo jikoni au stoo. Kuweka vyakula kwenye jokofu ambavyo havina sababu ya
kuwekwa humo inaweza kuwa ni chaguo binafsi kutokana na kwamba jokofu lako lina
nafasi ya kutosha kwasababu pengine una familia ndogo lakini jokofu ni kubwa,
kwahivyo unaona tu kwanini usiweke na chakula fulani ndani yake.
Hifadhi pamoja
vyakula vinavyofanana
Hii
ni kanuni ya msingi ya mpangilio wowote ule, ili uweze kupata unachohitaji kwa
haraka. Pale unapohitajika kuhifadhi chakula fulani ndani ya mfuko hasa kama ni
kwenye friza iandike mifuko hiyo majina ya vyakula vilivyomo ndani. Weka ndani
ya mifuko vyakula vya mbogamboga vilivyogandishwa. Wapo ambao wanagandisha
mbogamboga kama vile nyanya, njegere mchicha na nyinginezo. Wakati huo huo
ukikumbuka ukikumbuka kutenga sehemu ya nyama na mikate (ndio mikate
ikigandishwa inakaa muda mrefu zaidi, unaitoa muda mfupi pale unapotaka kuanza
kuitumia ndipo unahamishia kwenye jokofu yani sehemu isiyogandisha).
Vyakula
vya maboksi na makopo vinafaa kuwekwa eneo la mashelfu wakati mbogamboga zisizogandishwa
kama vile hoho, karoti, biringanya na kabichi vikipendeza kuwa kwenye droo
ambazo kwenye miundo ya majokofu mengi ziko eneo la chini.
Vyakula
vidogodogo kama vikopo vya maziwa mgando vinapendeza vikiwa ndani ya kikontena
kwani inasaidia visianguke anguke au kusambaa kila mahali. Pia inakuwa rahisi
kuchukua mara moja wakati ukihitaji kufanya hivyo na vilevile kugundua
vilivyopita muda wa kutumia. Kama wewe na familia yako mnapendelea kununua maziwa yaliyo kwenye
vikopo utakubaliana na mimi kuwa mara kadhaa kwenye kona nyuma ya jokofu
umeshakutana na ambayo yamepita muda wa
kutumiwa. Unapokuwa umeyahifadhi pamoja inakuwa rahisi kung’amua. Sasa basi, huenda wewe ni mpenzi wa vikontena katika kuweka mpangilio, ni muhimu
kuwa makini kuchagua ni wapi kwa kuvitumia kwa sababu vikiwa vingi vinaweza
kuzuia nafasi ndani ya jokofu hasa kama jokofu hilo ni dogo.
Kila kiporo kiingize
kwenye orodha ya mlo unaofuata
Ili
kuzuia mrundikano wa viporo ndani ya jokofu, kabla ya kuandaa mlo mpya ni vyema
kushirikisha kiporo cha mlo uliopita.
Tumia vyumba
vidogovidogo jinsi ilivyokusudiwa
Watengenezaji
wa majokofu wamefanya tafiti za kutosha na ndio maana wameweka vyumba mbalimbali
vikubwa kwa vidogo kwa mfano sehemu za kuweka mayai, dawa, vinywaji vilivoko
kwenye chupa na vingine nyingi. Kila kitu kinapokuwa eneo lake kwa
mpangilio jokofu linakuwa nadhifu.
Weka majina ya
vyakula kwenye mashelfu
Unaweza kutumia
zile kalamu za kuandika na kufuta baadaye kuweka majina kwenye mashelfu hasa
pale unapokuwa na friza refu kwenda juu lenye mashelfu juu mpaka chini. Mpishi
atakapofungua kuchukua nyama ya ngombe, kuku au samaki majina yatamrahisishia
shelfu la kwenda.
Je msomaji wangu ni zipi dondoo zako muhimu za kuweka mpangilio ndani
ya jokofu au eneo lingine lolote ndani ya nyumba yako? Nishirikishe!
Nifuate instagram @vivimachange
No comments:
Post a Comment