Thursday, May 19, 2016

Achana na vitu hivi kwani vinakusababishia mrundikano


Moja ya sababu za kuwa na mrundikano ni kutokujua wakati wa kuachana na baadhi ya vitu. Vitu vingi haviji na tarehe ya mwisho wa matumizi, na mara tunapopeleka kitu nyumbani, tunajitahidi kuwa tunakitumia hata pale ambapo kuna ukweli huwa hatukihitaji. Nimeandaa orodha ya
vitu ambavyo kuanzia sasa unaweza kuachana navyo aidha kwa kutupa, kugawa au kuuza ili uiweke nyumba yako huru na mrundikano.

Miwani ya ziada
Iwe ni miwani ya macho au ya kuzuia jua unapokuwa  na ambayo huvai tena kwa kufikiri tu kuwa ipo siku utaivaa ni kusababisha mrundikano. Unachotakiwa ni kuigawa au kuitupa mara moja.

Kalamu zisizoandika
Wino umeganda au umeisha kwahivyo hazifai tena, zitupe.

Vyombo usivyotumia
Ni ukweli kuwa ni ngumu kutumia vyombo kama sufuria, vikontena au mabakuli hadi viishe kwa kuchakaa kabisa ndipo ununue vingine. Tunajikuta tukinunua vyombo vipya tungali tunavyo vile vya zamani. Badala ya sufuria na vyombo vya zamani kukusababishia mrundikano jikoni, vigawe. Vile vikontena visivyo na mifuniko au ipo lakini haifungi vizuri navyo vigawe. Hatimaye na mwingine ashukuru kwa msaada uliompa.

Maboksi, makopo na chupa zilizoisha vyakula na vinywaji.
Kuna watu wana kawaida wakinunua kifaa chochote kinachouzwa na boksi wakishakifungua hawatupi boksi lake. Mmoja akaniambia ameyapambia maboksi hayo jiko lake. Jiko zima juu ya makabati ni maboksi matupu yameshamiri pamoja na chupa tupu zilizoisha mivinyo na viungo vya vyakula.

Mitandio usiyovaa
Kwa wamama na wadada wengi hasa mijini sherehe za kumfunda mwali (kitchen party) zimegeuka kiwanda cha kuzalisha mitandio. Tunaipenda ila unapokuwa nayo 20 kwa kukisia tu angalau unatumia mitano pekee. Gawa hiyo ambayo hujawahi na wala huivai maana sherehe bado zipo na zinaendelea kuja kwahivyo mitandio nayo itaongezeka.

Magazeti ya zaidi ya siku 2
Si kweli kuwa magazeti unayorundika ya siku 2 na zaidi nyuma kwamba utayasoma tena.

Vifaa vilivyobaki baada ya sherehe
Huenda ulikuwa na sherehe nyumbani lakini bado uma na glasi za plastiki na sahani za karatasi zilizobakia tokea kipindi hicho ambapo labda ni zaidi ya mwaka sasa bado unazo. Endapo wewe sio mtu wa kualika wageni nyumbani na kuburudisha mara kwa mara huna haja ya kuhifadhi vitu hivi, vichukue nafasi bure wakati tayari una vyombo vyako vizuri vya kawaida vya silva na udongo vya kutumia kwa maisha ya kila siku. Vipeleke ofsini watu watumie kulia lanchi viishe.

Rimoti za zamani
 Kila kitu hadi feni kinakuja na rimoti siku hizi. Ambayo huihitaji tena, itupe.

Soksi ambazo hazina mwenzie
Ukiwa na soksi iwe ni yako au ya mtoto lakini huoni mwenzie ipe muda kama wa mwezi mmoja. Baada ya hapo kama mwenzie akikosekana itupilie mbali.

Nyaya
Ulimwengu wa elektroniki umesababisha nyaya kusambaa kila mahali ndani ya nyumba zetu. Kumekuwa na nyaya nyingi ambazo nyingine hujui hata unachomeka wapi au zimeshakufa lakini bado zimerundikana mezani.

Kiporo cha zaidi ya siku 3

Vipodozi vya zamani
Si kweli kwamba unaweza kutumia tena kipodozi ulichonunua miaka miwili iliyopita. Hauwezi, hata kama hakijaandikwa tarehe ya mwisho kutumika, kama hukumbuki ni lini mara ya mwisho kukitumia kitupe.

Viatu na nguo
Hasa za watoto wadogo nyingi zinakuwa ndogo kuliko wao baada ya muda mfupi. Viatu ambavyo hujavaa kwa miaka zaidi ya mitatu vigawe.

Kadi, majarida na kalenda za zamani
Kama unadhani una sababu maalum ya kuhifadhi kadi au majarida mbalimbali uliyonayo aidha tafuta boksi uhifadhi pamoja. Vinginevyo ni vya kutupa. Kadi uliyopewa ya hongera kumaliza masomo miaka 10 iliyopita hadi leo unayo, jiulize je unaowapongeza nao wanazihifadhi miaka yote hiyo?

Simu za zamani
Hakuna sababu ya maana ya kuhifadhi simu hizi kwa ajili zimepitwa na wakati na hivi karibuni zitakapozimwa zile feki ndio itakuwa kifo chake kabisa.


Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment