Monday, May 23, 2016

Zijue rangi 5 zenye mvuto kwa mlango wa mbele

Njia ya haraka ya kuleta mvuto wa nyumba ni kupitia mlango wa mbele. Mlango huu ni utambulisho wa mwenye nyumba na pia unasema mengi kuhusu nyumba. Usishangae pia wengi wanapenda kupigia picha kwenye mlango wa mbele.

Kwanini uridhike na mlango wa mbele wenye rangi ile ile ya
mbao toka ulipoijenga nyumba hiyo hadi sasa? Huenda ni wakati wa  kutazama upya swala la rangi ya mlango wa mbele wa nyumba yako.
Rangi huwa zinacheza na macho na saikolojia ya anayeitazama.  Fundi rangi Dani David anatufahamisha rangi 5 zinazoweza kuleta mvuto kwenye mlango wa mbele:

Nyeusi
Nyeusi ni rangi yenye hisia na mvuto wa aina yake kwa ajili ya mlango wa mbele, inaendana vyema na nyumba za kisasa. Kama unaichagua kwa ajili ya mlango wa mbele ni muhimu kuamua ni nyeusi ipi. Tofautisha rangi ambayo ni nyeusi pekee na ile nyeusi inayotokana na uzito wa rangi nyingine ambapo unaipeleka rangi hiyo kwenye weusi. Kwa mfano rangi ya bluu nyeusi au udongo nyeusi ni tofauti na nyeusi ya asili ambayo tokea awali ni nyeusi na haijatokea kwenye rangi nyingine yoyote. Kuanisha aina ya nyeusi unayotaka ni muhimu ili kupata iliyo sahihi.

Kijani
Huenda hukuwahi kufikiria kijani kama rangi ya mlango wa mbele wa nyumba yako. Lakini kama tulivyosema rangi inacheza na saikolojia ya mtazamaji, nyumba inapokuwa na bustani ya uoto asili halafu ikawa na mlango wa kufanana na uoto huo inaleta picha nzuri ya ujirani wa rangi kati ya mlango na bustani.

Zambarau nzito
Je zambarau nzito inaweza kuwa ni jibu la rangi ya kuleta mvuto kwenye mlango wa mbele wa nyumba yako? Kwa siku za karibuni zambarau nzito imeanza kujipatia umaarufu sio tuu kama rangi ya mlango wa mbele bali pia kama rangi ya vyungu vya maua vya kuweka karibia na mlango wa mbele. Zambarau nzito inaendana na majani yaliyonyauka aidha yakiwa bado kwenye mti au yameshadondoka bustanini.

Kuchagua zambarau nzito sahihi inaweza kuwa changamoto kwa ajili ina wigo mpana toka zambarau ya zabibu hadi kuelekea damu ya mzee. Rangi ya ukuta itakuongoza vyema kwenye kuchagua zambarau ya mlango wa mbele, hakikisha unazilinganisha pamoja kabla hujafanya uamuzi.

Bluu ya mawingu
Unapochagua rangi za nje ya nyumba ni vyema ukumbuke kuwa zile zinazoendana na mazingira yanayozunguka nyumba zinakuwa na mvuto zaidi. Mazingira hayo yako katika makundi matatu ambayo ni sakafuni/ardhini, hewani na angani unapokuwa nje ya nyumba yako. Rangi ya bluu ya mawingu ina tabia ya kumpa mtazamaji hisia ya ukubwa na hewa ya kutosha pale ambapo hata eneo la mlango wa mbele wa nyumba si kubwa.

Dhahabu
Kwa asili dhahabu inapendwa toka enzi na enzi. Wenye nyumba wamekuwa wana vitu vya dhahabu lakini wanasahau kuwa rangi hii inafaa sana kwenye mlango wa mbele pia. Dhahabu inapendeza ikiwa maeneo jirani na vioo vya madirishani vina rangi nyeusi. Ni mantiki ileile ya ngozi nyeusi kupendeza wenye dhahabu kuliko ngozi nyeupe.


Wapenzi, kama uko instagram usisahau kunifuata @ vivimachange

No comments:

Post a Comment