Kama sofa zako zinaonekana kuchoka,
lakini bado hujakata tamaa kwamba uachane nazo jaribu kuzifufua kwa kutumia
njia moja au zaidi ya hizi tano. Unaweza
kushangaa ni kwa namna gani utapata matokeo makubwa na ya kuridhisha.
Tupia mito mipya
Njia rahisi na nyepesi kuliko zote
ya kufufua sofa ni kuweka
mito mipya. Mito ina nguvu ya kubadilisha muonekano
kwa njia zisizo na kikomo. Unaweza ukacheza na rangi, michoro, maumbo na hata
malighafi iliyotengenezea foronya za mito. Kama sofa unazotaka kufufua zina
rangi nyeusi au isiyoegemea upande wowote tupia mito ya kuwaka kama vile rangi za
chungwa, nyekundu au kijani cha ndimu na pia mito yenye doti doti za polka.
Kama hizo sofa ni za maua tupia mito ya rangi moja na kama zina kitambaa cha
rafu tupia mito ya kitambaa laini. Mito ya sofa inakuja kwa kila staili
kwahivyo huwezi kukosa unayotaka.
Shonea kitambaa kipya
Vipo vitambaa vingi vya sofa vyenye
maua, vya rangi moja au hata vya michoro mbalimbali ambavyo unaweza kumpelekea
fundi akashonea upya kwenye sofa zako. Pia uzuri wa sofa nyingi za kisasa zina
kava za kuvulika. Fundi sofa Adam Kajembe anasema, ni eneo dogo sana kama vile
zile sehemu za kuwekea mikono na mgongoni ambapo itamuhitaji fundi kushughulika
nayo moja kwa moja kwenye sofa . Na hasa kama sofa zenyewe ni za kutengeneza
hapahapa nchini basi una bahati maana itakuwa ni kazi rahisi zaidi.
Badilisha miguu
Ndio, ni kweli! Unaweza kufufua
muonekano wa sofa zako na kuzipa muonekano mpya kwa kubadilisha miguu yake.
Uzuri wa sofa zinazotengenezwa siku hizi zimeunganishwa miguu tofauti na fremu
la sofa yaani miguu sio muendelezo wa moja kwa moja toka eneo la kukalia. Mara
nyingi mgongo, kiti na eneo la kuweka mikono zimetengenezwa kama kitu kimoja na
baadaye miguu ndio inafungwa, anasema Adam. Kwa hivyo kama unataka kufanya
mabadiliko ni rahisi sana. Aidha unaweza kufunga miguu mipya au unaweza
kupulizia upya rangi miguu ya zamani na kuifunga tena na utashangaa tofauti
utakayoona.
Jazia kusheni zilizosinyaa
Kusheni hapa tunaongelea ile mito
inayokuja/inayotengenezwa na sofa ili kulikamilisha. Kusheni zinachukua nafasi
kubwa zaidi kwenye muonekano wa sofa. Mito hii ni muhimu na hatuwezi
kuilinganisha kiutendaji na ile ya mapambo ya kutupia. Bila kusheni ni ngumu
mgongo wa mkaaji kuwa na uwiano mzuri na sofa hilo. Sasa basi, kuendana na malighafi
zilizojazwa ndani kutengeneza kusheni hizo, kuna wakati zinakuwa zimesinyaa.
Fundi Adam anashauri tengeneza foronya jipya la kitambaa kinene (mithili ya mablanketi
na maduveti) halafu uchukue malighafi iliyosinyaa (bahati nzuri kusheni nyingi
zina zipu) na kuongezea pamba au faiba za kujazia mito zinazouzwa madukani.
Baada ya hapo funga mto huo na uvalishe foronya ya nje na ndipo unakuwa na
kusheni jipya ambalo halijasinyaa. Sababu ya kutengenezea foronya la kitambaa
kinene ni kuepuka mabondemabonde kwenye kusheni lako.
Badilisha vitu vinavyozizunguka
Japo njia hii si ya kugusa sofa moja
kwa moja, ila kuna wakati unaweza kufufua sofa kabisa kwa njia tu ya kuboresha
vitu vinavyolizunguka.. Jaribu kutundika picha mpya au hata kubandika karatasi
za ukutani yani wallpaper nyuma ya ukuta ilipo sofa. Zikiwa zimezungukwa na
vitu tofauti na vizuri, sofa zako zinaweza kuvutia pia!
Simu 0755 200023
No comments:
Post a Comment