Monday, May 2, 2016

Namna ya kubuni bustani nzuri ya maua


Bustani nzuri ni eneo la kuvutia nje ya jengo lolote. Bustanini kunaweza kuwa mahali pazuri kwa kufurahia mapumziko ya jioni wakati wa kiangazi. Hata hivyo kabla hujaanza kutumia muda wako na pesa kuanzisha bustani ni vyema kutafiti kwa umakini na kuweka mipango mahususi kama
ifuatavyo:

Angalia eneo unalotaka kuanzisha bustani husika. Tembea kulizunguka na kuona ni kwa namna gani unataka  bustani yako iwe. Zingatia sehemu ambazo unataka zibaki kama zilivyo. Hakikisha una pembe nne za dira ya bustani yako, yaani kaskazini, kusini, mashariki na magharibi.

Chora mchoro wa umbo la mahali unapotaka kubuni bustani. Mchoro huu utakusaidia kupata maono ya nini ungependa kiwe kwenye kila kisehemu. Mchoro uonyeshe vitu ambavo ni vya kudumu kwenye eneo hilo, kwa mfano mashimo ya maji taka na kuona ni jinsi gani unaweza kuyafanya yavutie ndani ya bustani. Inaweza kuwa ni pamoja na kuyazungushia maua, au kuyawekea vyungu vya maua, au kuyapaka rangi za kuvutia na kadhalika. Weka majina sehemu ambaypo ungependa iwe na mti/miti, maua na bila kusahau sehemu ya kuketi.

Ainisha maeneo magumu. Maeneo haya ni yale kama kwenye mwinuko, bonde, kichuguu au kona ambayo haijakaa sawa. Huna haja ya kuingia gharama ya kuyarekebisha badala yake kuwa mbunifu kwa kutengenezea bustani ya mawe, kitanda cha maua na kadhalika. Fanya utafiti kutoka  mitandao na vitabu mbalimbali vya busatani jinsi ya kufanyia kazi maneo ya namna hiyo.

Tembelea bustani mbalimbali kwenye eneo lako au kwa ndugu na marafiki, kwani kuona kitu ni chanzo kikubwa cha kuhamasika. Angalia jinsi bustani  zilivyobuniwa kwenye majengo ya biashara na ya serikali.

Ukishamaliza hayo yote sasa rudi kwenye eneo lako na anza kuorodhesha idadi ya maua na mimea ya maeneo uliyoainisha kwenye mchoro. Bustani kubwa inapendeza vitanda vya maua vikiwa vikubwa na ndogo vitanda vidogo.

Chagua maua yanayopenda jua kwa ajili ya sehemu za jua na ya kivulini kwa sehemu hizo. Tafiti kila ua na kuwa na hakika linakidhi vigezo na mahitaji ya bustani yako. Mfano ni huenda utamwagilia maji ya chumvi, hakikisha maua na mimea unayootesha itakubaliana na hali hiyo.
Maua na mimea mingi ya kutambaa inapendeza ikizunguka uzio au mti wa bustani. Vilevile tafuta maua itakayokubaliana na bustani ya mawe.

Sasa ni wakati wa kuotesha maua yako. Tumia kamba kwa maeneo ambayo kitanda cha maua kinatakiwa kiwe kimenyooka hasa kama kimezungukwa na maua ya boda. Mfano mzuri ni maua ya kuzunguka uzio. Otesha maua marefu nyuma na mafupi mbele. Ipe mimea na maua mapana eneo zaidi na pia changanya mimea ya rangi mbalimbali

Kumbuka kama udongo wa bustani ni mgumu sana au una asili ya mwamba unatakiwa kujaza udongo mwingine kabla ya kuotesha chochote na pia unaweza ukatakiwa kuweka mbolea kabla ya kuotesha.

Malaka hii imeandaliwa na Vivi ili kukuwezesha kupendezesha nyumba yako

No comments:

Post a Comment