Tuesday, May 10, 2016

Haya ni maswali 10 (na majibu yake) ninayoulizwa mara kwa mara kuhusu wallpaper

 
Kuna mwamko mkubwa wa mapambo ya nyumbani kwasababu  wenye nyumba wengi wa kileo wanataka nyumba zao zivutie. Sio ndani tu bali hata nje. Kwa sababu hii ushauri na mazungumzo kuhusu mapambo ya nyumbani ndio yameshamiri kwa wengi wanaojenga nyumba zao kwa sasa.
Na
ndio maana mapambo mapya yanaibuka kila siku, wallpaper kwa mfano, sio ngeni duniani lakini kwa karibia muongo mmoja uliopita limekuwa pambo linaloonekana kushika kasi kwenye nyumba nyingi za kisasa hapa nchini.

Ni kweli kuwa kupaka rangi kwenye kuta za nyumba zetu kunapendezesha lakini watu wanataka kuongezea na vitu tofauti.  Kutokana na hilo basi kuna maswali ambayo yamekuwa yakijirudiarudia kwa kuulizwa na wengi kati ya wanaotamani kupamba nyumba zao kwa wallpaper. Ingawaje baadhi ya maswali yanaweza kuonekana kama yanamlenga zaidi fundi mbandikaji lakini ni vyema pia wewe mwenye nyumba ufahamu zoezi zima ili usibabaishwe wakati wa mchakato huo. Baadhi ya maswali hayo na majibu yake ni kama ifuatavyo:

1.      Ninahitaji wallpaper kiasi gani kubandika kwenye chumba?
Ili kupata jibu la swali hili unatakiwa kuwa na futi kamba ili upime ukubwa wa ukuta unaotaka kubandika wallpaper.  Ukishafahamu ukubwa wake unachotakiwa kujua ni kwamba wallpaper zinakuja kwa roli za upana wa nusu mita na urefu wa mita kumi. Kwa namna hiyo ndipo utaweza kufahamu unahitaji roli ngapi kutokana na ukubwa wa eneo unalotaka kubandika

2.      Ni kuta gani nibandike wallpaper?
Kuta zote za chumba zinafaa kubandika wallpaper. Ila kwa matumizi mazuri ya rasilimali fedha wengi wanapendelea kubandika kwenye ule ukuta unaotazamwa zaidi. Kwa mfano kama ni sebuleni bandika kwenye ukuta wa luninga na kama ni kwenye chumba cha kulala bandika kwenye ukuta wa kichwani.

3.      Je sehemu za maungio naunganisha kwa kubebanisha?
Hapana.  Kwenye kubandika wallpaper huwa maeneo ya maungio karatasi hizo zinakutanishwa moja kwa moja na sio kubebanishwa. Mbandikaji anatakiwa kufanya kwa usahihi na umakini kabisa kiasi kwamba  sehemu za maungio hazigunduliki. Na pia ni vyema kuangalia maua na michoro ya karatasi zako kama inahitaji muendelezo, yaani inalenga umbo fulani na ndipo kwenye kuunganisha unahakikisha unaendeleza muonekano huo.

4.      Je nahitaji gundi ya ziada kupaka ukutani?
Jibu la swali hili ni hapana. Wallpaper zinakuja na gundi zake maalum ambazo ndizo unapaswa kutumia. Huhitaji kuongezea gundi nyingine yoyote. Usidanganyike na habari za kuambiwa ongezea gundi ya viatu na kadhalika.

5.      Naweza kubandika wallpaper mpya juu ya ya zamani?
Haishauriwi kabisa kubandika wallpaper mpya juu ya ya zamani kwa sababu inaweza kufanya msuguano kati ya hizi tabaka mbili na kusababisha ya juu kuumuka na kubanduka au kutengeneza nafasi za hewa ndani na kutuna.

6.      Naweza kufanyia marekebisho sehemu ndogo iliyoharibika?
Kama ikifanyika kwa usahihi inawezekana na kama utabahatika kupata wallpaper mpya inayofanana na hiyo unayotaka kurekebisha.

7.      Je inawezekana kupaka wallpaper rangi?
Ndio, japo si zote ila zipo wallpaper ambazo unaweza kupaka rangi.

8.      Je wallpaper inashika kwenye gypsum?
Ndio, wallpaper inafaa kubandikwa kwenye gypsum ndio maana kuna dari za gypsum na zimepambwa kwa wallpaper.

9.      Ukishabandika wallpaper inachukua muda gani kukauka?
Wallpaper chumba chenye hewa ya kutosha na kisicho na fukuto inakauka baada ya saa moja. Kwa maeneo mengine kama bafuni hasa bafu linalotumia maji ya moto inaweza kuchukua hadi siku tatu.

10.  Nawezaje kubandua wallpaper?
Kwa habati mbaya sio kazi rahisi sana kubandua wallpaper. Gundi inayobandikia imetengezwa kujiachia ikipata maji. Unapotaka kubandua wallpaper unachotakiwa kufanya ni kukwaruza kwanza kisehemu kutafuta chanzo cha kukutana na gundi halafu baada ya hapo unaanza kulowesha maji kwenye hicho chanzo. Maji yakiwa ya moto inasaidia kuahisisha zoezi.


Simu 0755200023

No comments:

Post a Comment