Wednesday, November 14, 2012

My article for newspaper: Mapambo ya msimu wa sikukuu




Njia chapchap za kupamba ndani na nje ya nyumba yako msimu huu wa sikukuu

Chochea furaha na msisimko wa kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kupamba ndani na nje ya nyumba yako. Vitu rahisi hata  kama ni vijipambo vya meza tu huleta tofauti kubwa ya muonekano wa mazingira ya nyumbani.

Baadhi ya njia tofauti unazoweza kuhuisha muonekano wa kizamani wa nyumba yako ni kama ifuatavyo:
Ongeza picha: Kuongeza picha nyumbani kwako kunaongeza muonekano mpya mara moja kutoka ule wa zamani. Ni njia rahisi kabisa kuhuisha sebule yako. Au unaweza kuongeza picha za familia yako ama nunua picha za fremu kuleta muonekano wa kipekee.
Mimea na maua: Pamba mazingira ya ndani na nje ya nyumba kwa maua na mimea. Vesi ya maua au mmea uliooteshwa kwenye chungu kwenye kona ya mahali ndani mwako vinaleta mvuto.
Badili pazia: Hizo pazia za kila siku zinafanya nyumba isionekane tofauti au na mvuto kwa ajili ndio hizo hizo kila siku. Hakuna kitu kinacholeta tofauti kubwa kwenye muonekano wa nyumba kama pazia. Weka mapazia ya aina, mitindo na vitambaa na mishono mbalimbali.
Rangi:  Kupaka rangi ni njia iliyozoeleka zaidi wakati wa kusheherekea. Zimua kuta za mazingira ya nyumbani kwako japo kwa kuongeza koti moja tu ya rangi. Kama labda kupaka rangi chumba kizima ni gharama na kazi kubwa basi paka hata mlango tu.
Weka mito mipya: Badilisha mito ya sebuleni kwako na uweke ya rangi mbalimbali. Mito yenye rangi kali zilizokolea kwenye sofa zako au hata ile mikubwa ya kukalia sakafuni inabadilisha muonekano wa ndani ya nyumba bila ya kutumia gharama au kazi kubwa.
Panga vitu upya: Sio cha zaidi bali tu ni kuhamisha tuseme fenicha moja toka eneo moja hadi lingine. Kufanya hivyo utashangaa jinsi itakavyohuisha muonekano wa mahali.
Pamba eneo la lango kuu:  Kinachoonekana kwanza kinamkaa mtu moyoni daima kwa hiyo unaweza ukahuisha muonekano wa kuingialia nyumbani kwa kupamba eneo la kuingilia. Kwa mfano vyungu vya maua vya chini au vya kuning’inia lango kuu vitaleta mvuto wa kipekee.
Boresha fenicha: Paka rangi fenicha ya zamani au hata ibadili kuongeza matumizi yake. Hii haitaleta tu muonekano mpya bali pia itaongeza thamani na matumizi ya fenicha hiyo.
Weka virembo vidogodogo:  Katika nyumba nyingi utakuta kuna sehemu ambazo unaweza kuweka virembo vidogodogo kama vile juu ya kabati au shelfu na kadhalika. Kutumia nafasi hizi kuweka marembo kutaleta mvuto ndani ya nyumba na kuongeza uzuri wa kutazama na kushangaa.
Mapambo ya msimu:  Vitu vya wakati husika vyenye mvuto vinaweza kuwekwa kama mapambo nyumbani bila hata kutoa jasho. Kwa mfano unaweza weka matunda au maua ya msimu kwenye bakuli la kuvutia, au vesi na kuweka mezani na ikavutia sana.                                                                                      
Pia unaweza kuzungushia taa zisizo na gharama za msimu wa sikukuu kwenye miti ya bustanini au eneo la lango kuu au hata eneo la ngazi wakati wa sikukuu na kuleta muonekano wa maajabu.
Kama tujuavyo sikukuu za mwisho wa mwaka zinazokuja ni krismasi na mwaka mpya hivyo usisahau kupamba kwa mti wa krismasi! Mti huu umekuwa ni pambo la kipekee kwenye nyumba nyingi duniani na hata maeneo ya jumuiya na ofisi nyingi kila mwaka kwenye sikukuu ya krismasi.

Kama unataka kuongeza viungo vya mapambo kwenye nyumba yako yenye muonekano wa siku zote wala huhitaji kutumia gharama kubwa. Mabadiliko kidogo lakini yeye mashiko yatafanya nyumba yako kuonekana upya. Kutembea kwenye nyumba inayoonekana tofauti wakati wa sikukuu kiukweli kutahuisha na kuongeza msisimko wa sikukuu. Hutakiwi kuwa mtaalamu wa mapambo ya nyumbani ili kuleta mabadiliko haya. Kinachotakiwa tu ni kuwa mbunifu wa kufikiri. Jinsi ya kushehereke sikukuu ni kupamba nje na ndani ya nyumba kwa vitupio murua. Kutegemeana na ladha yako unaweza kupamba kwa rangi zilizozoeleka kwa sikukuu za mwisho wa mwaka ambazo ni Top of ForBnyekundu, nyeupe na kijani. Mawazo ya upambaji ni lukuki, kutegemea na bajeti, ladha binafsi na mazingira ya makazi yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni tuwasiliane viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.

Tuesday, November 13, 2012

Fashion designing is my passion!

Top
  
Gauni nililombunia mteja wangu Monica. Nashona nguo kwa kuwa ni kitu nakipenda na nachukua muda mwingi kuhakikisha nguo inatoka bomba.

Thursday, November 8, 2012

Obama Ladies' Style Evolution

2008 Vs 2012..are you inspired?

Tuesday, November 6, 2012

My article for newspaper: Mapambo ya bafuni



Mapambo ya Bafuni
Ongeza mvuto bafuni kwako kwa gharama kidogo tu. Kuanza kujenda bafu tokea mwanzo ni gharama ila kuongeza mvuto kwenye lililoko tayari sio kazi kubwa. Kwa baadhi ya watu bafuni ni sehemu ambayo inaachwa kando (au ya mwisho kabisa kufikiriwa)kwenye maswala haya ya mapambo ya ndani. Fahamu kuwa bafuni panaweza kubeba ujumbe mzito hasa kwa wageni wanaokutembelea nyumbani.

Unapopanga kupamba bafu lako (au chumba kingine chochote) pa kuanzia ni kwenye ukuta. Ukuta unachukua sehemu kubwa ya chumba kwa hivyo fikiria ungetaka ukuta wa bafu lako uweje. Je unapenda kuweka taili ukuta wote hadi juu au nusu tu halafu umalizie na rangi. Taili hadi juu ni gharama ila inasaidia kunyonya mvuke hasa kama bafu linatumika na maji yote ya moto na baridi. Pia kama huwezi kuweka taili kuta zote unaweza kuweka hadi juu kwenye kuta za eneo la kuogea na kuta zingine ukaweka nusu ili kujipambia kwa kupiga rangi mbalimbali kwenye kuta zilizobaki bila taili. Taili za kufika hadi mwisho wa ukuta zimeonekana kuleta muonekano wa usafi zaidi na hata kama kuna mapambo au vitundikio vingine unapenda kuweka ukutani basi kuna mashine za kutoboa ukuta wenye taili na hivyo kuweza kutundika mapambo yako kirahisi.

Eneo la kuogea
Taulo na vizulia vidogo vyenye plastiki kwa chini za kuzuia maji ni vitupio muhimu bafuni; utakapoweka vya rangi mbalimbali na kuvibadili mara kwa mara basi vitabadili muonekano wa bafu zima. Weka pazia la eneo la kuogea lenye mvuto linalooana na rangi za taili.
                                                                                                                                                    Eneo Eneo la sinki
Kwa kuboresha muonekano wa eneo hili njia kuu ni kubadili staili ya bomba la sinki. Mabomba ya sinki yanakuja na mitindo mipya kila leo kwa hivyo kwa kuweka bomba jipya itabadili muonekano mzima wa eneo hili. Kama kioo juu ya sinki ni kidogo badili uweke kikubwa ambacho pia kitasaidia kuongeza mwanga bafuni. Badilisha taa ya juu ya kioo iendane na rangi nyingine za hapo bafuni kama vile rangi za mataulo au hata za pazia la eneo la kuogea.

Labda hili ni bafu lako la kuanza maisha baada ya kuachana na wazazi iwe ni kwa kuanza maisha ya ndoa au maisha ya peke yako ya kujitegemea basi kuna vitu kadhaa ambavyo ni muhimu kuwa navyo bafuni. Nimeorodhesha vitu ambavyo nadhani ni muhimu kuwapo bafuni kwako nyumbani, na kwa kweli nimechagua vile ambavyo vinavutia! Unaweza kuishi bila baadhi ya hivi vitu lakini kwa nini ufanye hivyo?
Kumbuka unastahili sehemu nzuri ya kujiandaa kabla ya kwenda kuchakarika siku nzima. Kwa nini usiwe na kila unachohitaji mahali hapo?

Bafuni pawe na mwanga wa kutosha. Linapokuja swala la taa za ndani, bafuni mara nyingi hapapewi kipaumbele na ni pa mwisho kufikiriwa kati ya vyumba vingine vyote. Wenye nyumba wengi wanaweka zaidi hela yao kwenye taa za sebuleni na jikoni. Bafuni kunahitajika taa hasa eneo la kioo, wengi wanaweka ile taa moja tu ya juu ya kichwa. Bafuni ni sehemu ya kuhuisha mwili kwa kuumwagia maji na ni sehemu ya kuanzia na kumalizia siku yako hivyo tusipasahau wakati wa kuamua swala la mwanga wa nyumba.
Bafuni kuwe na vioo vya kukidhi hitaji lako. Weka kioo popote bafuni unapodhani ya kuwa unahitaji kuweka kioo. Usinganganie tu utamaduni wa kioo cha bafuni kinakuwa juu ya sinki. Pia kuwe na seti ya mataulo yale hasaa ya kukausha maji na sio hayo ya barabarani yenye nailoni yasiyokausha vizuri.                                                                                                      
 

Vizulia, pazia la eneo la kuogea na kindoo cha uchafu maalum kwa mazingira ya bafuni ni muhimu viwepo bafuni.                                        
Bafuni kuwe na vifaa sahihi vya usafi na eneo la kuhifadhia . Pia mlango na kioo cha dirisha viwe vimetengenezwa kwa jinsi ya kuwepo faragha.

Kiwekeo cha miswaki ni kitu kidogo na  hutakiona cha maana kuwepo bafuni hadi pale mswaki wako utakapoanguka chini au chooni. Usisahau kuweka sabuni na taulo la mikono kwa ajili ya wageni.
 
Je kuna chochote hapa ambacho kimesahaulika kuwepo bafuni? Kuna katika orodha hii ambacho unadhani hukihitaji bafuni kwako? Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.k au simu namba 0755 200023

Thursday, November 1, 2012

My article for newspaper: Muonekano wa jiko



Muonekano wa Jiko

Jikoni huenda ni mahali ambapo panadharaulika sana kwenye nyumba za watu wengi; wanafikiria jiko kama ni mahali au chumba cha kupikia chakula tu kwa hiyo mapambo mahali hapo hayahusu. Hawawezi wakawa wanakosea zaidi ya kufikiria hivi; jiko linaweza kuwa mahali pazuri kuliko pote katika nyumba unayoishi kama una staili na unajua jinsi ya kupamba.

Jikoni ni moja ya sehemu muhimu sana kwenye nyumba yako. Ni sehemu ambayo pia inatembelewa mara nyingi zaidi kwa siku kuliko sehemu nyingine yoyote hapo nyumbani. Unatakikana kwenda jikoni mara kadhaa kwa siku, kuandaa chakula au hata kuchukua glasi ya maji baridi. Hutataka kuona jiko lako likiwa limejaa uchafu mavumbi na mafuta. Zaidi ya yote jiko linatakiwa kupambwa na kuonekana maridhawa na linalohuisha nafsi.

Chumba cha jiko la kawaida la kisasa kinakuwa na vitu kama jiko, sinki la maji moto na baridi, jokufu, makabati, kipasha chakula na vifaa vingine vya umeme. Yapo majiko makubwa kwa wenzetu wa magharibi ambapo kwao zaidi ya chumba cha jiko kuwa ni mahali pa kuandaa chakula pia ni mahali pa kufulia, kulia chakula na stoo ya kuhifadhia vyakula. Kubuni jiko la kukidhi mahitaji yako iwe ni kwa nyumba mpya au kubadilisha muonekano wa jiko la zamani inabidi kutembea na kutafiti kwa kuangalia aina mbalimbali za majiko ambayo tayari walau yanakidhi mahitaji ya jiko la kawaida ndipo nawe ukaweza kujiamulia la kwako. Kuna wataalamu ambao wanaweza kubadili jiko lako na kuwa la kisasa kuendana na mahitaji yako.

Chumba cha jiko kinahitaji vyombo ambavyo ni vya kawaida kwa walau kila mtu au familia. Sasa unamsaidiaje mtu ambaye anaanza maisha na anahitaji jiko. Lengo la makala hii ni kuongelea muonekano wa jiko la kisasa la kawaida kabisa sio hayo yenye sehemu ya kulia hapo hapo na sehemu ya kufulia.
Ingawa kuna aina mbalimbali za majiko kwa kila kaya, bado unaweza kujaribu kitu kipya na cha kisasa kwa ajili ya sehemu hiyo ambayo inatembelewa kuliko zote katika nyumba yako. Jiko lako ni mahali panapotakiwa kuwa na mvuto na pia kufanyia kazi kwa uhuru kwa kuwa na vifaa vinavyohitajika.
Vyombo kama sahani, vijiko, glasi na vikombe vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi hivyo sitaviongelea hapa. Vitu vifuatavyo vitafanya jiko lako liwe nadhifu:
  • Makabati
Aina ya makabati utakayochagua na mpangilio wake unatoa picha kubwa ya jiko kwani makabati yanachukua nafasi kubwa zaidi katika chumba cha jiko. Unaweza kuchagua makabati ya mbao hadi ya chuma ila ya mbao yanapendeza na yanadumu kuliko yote. Ya chuma yamekaa kiviwandani zaidi sio kwa ajili ya nyumba za kuishi. Kama una vyombo ambavyo ungependa vionekane basi weka makabati ya mbao ila yenye milango weka vioo. Vitasa na  mikono ya makabati na madroo na hata bomba la sinki visiwe vya urembo mwingi ila tu hakikisha ni imara na vina usalama kwa mfano visiwe na ncha za kumkwaruza mtumiaji. Vitu vyenye urembo mwingi vinaharibu muonekano wa jiko.

  • Sakafu
Jikoni kunatumika na kila mwanafamilia hivyo inatakiwa kuwa na sakafu ambayo ni imara na isiyoharibika kirahisi. Kama una watoto wadogo basi ni vyema kuwa na sakafu isiyoteleza, ambayo pia ni rahisi kusafisha kwa ajili watoto wana tabia ya kuokota vitu chini na kuweka mdomoni. Haishauriwi kuweka zulia jikoni kwa kuwa kuna mafuta na majimaji yanawagika chini wakati wa kupika na kusafisha vyombo na jiko lenyewe.
  • Hifadhi
Kama unahitaji sehemu ya ziada ya kuhifadhia zaidi ya makabati basi unaweza kuweka vitundikio vya masufuria au viraki kwenye kona ambayo unaweza kuweka vitu vidogovidogo.
  • Mwanga
Jiko linahitajika mwanga mwingi kwa kuwa shughuli nyingi na vifaa vingi vinatumika hapo kwa ajili ya kuandaa vyakula. Pia dirisha la kupitishia mwanga na hewa liwe kubwa kwa kuwa joto jingi linazalishwa jikoni na kwa mfano hapa kwetu watu hawana mazoea pia ni wachache sana waa uwezo kifedha wa kuweka kiyoyozi jikoni. Feni ya jiko kwa ajili ya kunyonya mvuke ikiwepo itakua vyema.
Mapambo ya jikoni sio kama ya chumba kingine kwa mfano chumba cha kulala au sebule, jiko linaweza kupambwa kipekee bila kuhusisha muonekano wa vyumba vingine. Nyumba yako bado itakuwa inavutia hata kama jiko limepambwa tofauti kabisa na vyumba vyote. Yote kwa yote, muonekano wa jiko lako unaweza ukavutia zaidi ya unavyofikiri kama una ladha ya staili na mitindo  basi unaweza kufanya jiko lako likawa ni sehemu kila mwanafamila anapenda kutembelea na pia kurahisisha kazi ya mpishi. Muhimu zaidi ya yote jikoni napo papambwe kama ilivyo vyumba vingine ndani ya nyumba yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23

Wednesday, October 24, 2012

My article for newspaper: Unatokea ofsini kwenda kimnuso



Jinsi ya kuvaa ukiwa unatokea ofsini kwenda kwenye kimnuso

Ni saa kumi na moja jioni lakini sio muda wa kwenda nyumbani. Badala yake, kuna kimnuso na wanawake wengi walivyo ni tukio ambalo linaweza kukuacha ukihangaika juu ya nini huku duniani cha kuvaa kazini siku hiyo ili uunganishe na mtoko wako huo wa usiku.

Mbaya zaidi ni kuwa huna muda wa kwenda nyumbani kubadili ni lazima utokee kazini ulikokuwa umekaa mbele ya komptyuta moja kwa moja kwenye usiku wa tafrija na shampeni. Lakini kabla hujaumia kichwa zaidi, vitupio vinaweza kubadili kabisa muonekano wa vazi fulani kutoka muonekano wa kiofisi kwenda kwenye usiku wa sherehe.

Sasa ni wapi pa kuanzia? Anza siku yako kwa kuvaa sketi  fupi ya rangi yoyote na koti la rangi isiyofanana na sketi na kiblauzi ndani mwake. Usisahau mchuchumio wako kuonyesha umbile na urembo wako. Baada ya saa za kazi wakati wa kuelekea kwenye tafrija kama hutaweza kwenda nyumbani kubadili nguo unaweza kubaki na kiblauzi cha ndani ya koti na kuacha koti lako kwenye gari na beba pochi na sio ule mkoba mkubwa wa kazini.

Siri ya kuvaa nguo zile zile ila mionekano tofauti kutoka mchana kuingia usiku ni mpangilio wa  nguo na vitupio vyako. Changanya mavazi yako na vitupio kuendana na shughuli ya wakati husika ili mavazi yale yale yawe na mionekano tofauti. Jenga taswira mbalimbali kwa mfano kiatu hichi hicho ila na pochi tofauti tofauti inaonekanaje. Taswira ni msingi wa mafanikio yako.

Hereni zina nguvu kubwa ya kubadili muonekano wa mavazi ya kiofisi kwenda kwenye mg’ao wa muonekano wa usiku. Kama huwa huvai hereni kazini au unavaa vile vidogo sana basi usiku ni wakati wa kuvaa hereni kubwa zinazong’aa ambazo huwa zinabadilisha hata mavazi rahisi kabisa. Jaza shingo yako na mkufu au hata mtandio wenye rangi za kuwaka utabadili muonekano wa ofsini kuwa wa sherehe. Hii itasaidia kuleta mwanga na rangi usoni mwako na hivyo kubadili muonekano wako mzima. Kuendana na mtindo uliopo kuna wakati vidani, mikufu au shanga zinavaliwa zaidi ya mmoja na unaweza basi ukaongeza na bangili.

Pete kubwa yenye jiwe kubwa kati  iliyovaliwa kwenye kidole chochote inabadilisha muonekano wa kiofisi kuwa wa kisherehe zaidi. Pete hii moja tu inatosha usivae zaidi. Hakuna kitu kinachoonyesha unaelekea kazini kama mkoba wako. Mkoba unaweza kuharibu kabisa muonekano wako wa vazi la sherehe. Kwanye sherehe beba pochi (ile ndogo ambayo mara nyingi si ya kutundika) na weka vile vitu muhimu sana ambavyo ni lazma unavihitaji popote uwapo kama vile leseni ya udreva, pesa taslimu kidogo, kadi ya ATM, simu na funguo. Wakati wa kutoka kuelekea kwenye mnuso unaweza kufungia mkoba wako kwenye droo la ofsini na kuuchukua kesho yake. Kumbuka mkoba usiache kwenye gari kwani ni kishawishi kwa wezi wa kwenye magari.

Linapokuja swala la vipodozi, ukiwa unatokea ofsini kwenda moja kwa moja kwenye sherehe usijaribu kujipaka tena uso mzima. Badala yate tumia vichache tu kama lipstiki, ongezea mascara kidogo na kimguso cha poda kuondoa mngao kwemye uso wako na ongeza vipodozi kwenye mashavu.  Weka shedo za macho zenye rangi za silva na dhahabu. Vipodozi vya kwenye mashavu vizidi kidogo usiku kulinganisha na wakati wa kuwa ofsini.
Kwa nywele za chap chap chana ulizonazo kama ni fupi ama funga kifagio kama ni ndefu na kuongezea kibanio. Hizo hereni zako kubwa tayari zitakuwa zinashirikiana na nywele kuleta mvuto.

Mtandio ama skafu inasaidia sana kubadili muonekano wa mavazi toka siku ya kazi kwenda usiku wa kimnuso. Kwa ofsini funga kitambaa chako hicho shingoni wakati usiku  unaweza kufunga mtandio au skafu yako kiunoni kama mkanda.
Rangi zinaweza kuvalika kutokana na uamuzi wako ila nyeusi na nyeupe bado ni maarufu kwa wanawake. Vaa rangi kazini lakini zigeuze kuonyesha urembo wako nyakati za usiku.

Harufu yako ni muhimu kukamilisha muonekano wako mzima; inakupa utambulisho, wakati wa mchana tumia pafyum zenye ladha za maua ila usiku tumia pafyum yenye harufu kali zaidi kusisitiza utu wako.
Kama una mtoko utakaokugharimu kutokea ofisini moja kwa moja fuata dondoo hizi na zitakuongoza kupata muonekano wako wa kazini na usiku siku hiyo.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au  simu 0755 2000 23.





Sunday, October 21, 2012

ni kama jana tu

ukiona kitu kizuri cha kumfaa mwanao hata kama ni hapo miaka 10 ijayo usiache kumnunulia kwa ajili siku hazigandi. utashangaa mara anakitumia. nakumbuka baba mwenye nyumba alikutana na buti nzuri za mvulana kama wa miaka 12 akamchukulia mwanae wa miaka 2 watu wakamcheka na kumshangaa sana. lakini soon huyo kijana atazitinga..