Friday, August 31, 2012

I love the work that I do

Strapless dress


top



Wiki hii nimekaa na wateja wangu kadhaa na tukajadiliana juu ya nguo walizotaka kushona. Kwenye kazi ya kubuni na kumshonea mteja nguo inahitaji uvumilivu na mawasiano muda wote. Ninachofanya ni kufanya kazi na mhusika bega kwa bega. Sifanyi uamuzi wowote bila kumhusisha. Je unahitaji kushona nguo yoyote? Njoo tufanye kazi hiyo pamoja..

Thursday, August 30, 2012

My Article for Newspaper: Viatu vinaweza kukutoa au kukuangusha!


Viatu vinaweza kukutoa au kukuangusha!

Kwa kawaida binadamu anapenda anachovaa miguuni hivyo kujua kanuni za jinsi ya kuvaa michuchumio, buti, flat na mkuki moyoni itakusaidia kununua kwa busara na kuvaa aina mbalimbali za viatu kuendana na mwili wako.
Viatu ni kiambatanisho cha mitindo kipendwacho sana na vinaweza kutoa ushuhuda kuhusu mvaaji awe ni mtu maarufu au sio. Viatu vinavyoonekana vizuri sana kwenye shelfu la duka la muuzaji vinaweza visikufae kutokana na mwili wako, baada ya kuviweka miguuni ndio unapoweza kufanya uamuzi.  Kutochagua sahihi wakati kuna viatu kibao itakua mbaya sana. Ni vizuri kujiangalia muonekano mzima toka utosini hadi kidole cha mguu kwenye kioo kirefu na kuona ni nini wataalamu wanasema juu ya viatu vitakavyokufaa.

Viatu vya wanaume vimegawanyika katika makundi mawili. Buti za ngozi na viatu kwa ajili ya kuvaa kila siku. Hii ndio mitindo ya viatu vya wanaume.

Haipingiki kuwa viatu ni mojawapo ya kitu kinachomgusa mtazamaji kwenye muonekano wa mvaaji. Haijalishi kuwa mguso ni hasi au chanya ila viatu ni kivutio cha mitindo kwa vizazi vyote. Baadhi tunaamini kuwa viatu  ndio vinaleta muonekano mzima wa utofauti  kwa waigizaji, wanasiasa, wanahabari na watu wote wanaoonekana mara kwa mara katika macho ya jamii. Ni ukweli kuwa viatu fulani fulani vinatoa tamko mvaaji ni mtu gani hasa kama mbunifu wa viatu husika atakuwa anajulikana pia. Tumeona na kusikia jinsi viatu vya mbunifu Christian Louboutin maarufu kama CL au Loubs vinavyowatamanisha watu wengi maarufu duniani kote. Viatu hivi vina soli ya rangi nyekundu ambayo kwa furaha ya kuvipata mvaaji akiweza kuvinunua anapiga picha akiwa kanyanyua mguu kuonyesha soli. 

Ndio, viatu vinaweza kufanya mavazi yakawa rasmi au sio rasmi. Kama una kifundo cha mguu chembamba una bahati kwani kwenye ulimwengu wa viatu utavipata vya kila aina na kila uzuri. Kila kitu kuanzia sketi fupi na mchuchumio hadi sketi ndefu na sandali vitakutoa bomba.
Viatu virefu vinene, maarufu kama magogo kwa miguu membamba vinaweza kuonekana kama vinamzidi mvaaji nguvu, jicheki uridhike kabla hujaamua kuvaa staili hii.

Kama miguu yako ni mifupi na myembamba kitu muhimu sana cha kukumbuka ni urefu. Hii ina maana kuwa unahitaji viatu virefu bila kambakamba. Nimesema bila kambakamba ili kusiwe na kitu chochote cha kugawanya mguu wako, isipokua tuu vile viatu maarufu kama sandali za  gladiator ambazo zinawapendeza wenye vifundo vidogo vya miguu. Kama unataka kujisikia huru unaweza kuvaa viatu flat ila na gauni lenye urefu wa kuvuka magoti. Vinginevyo miguu yako itaonekana mifupi zaidi. Viatu vilivyo wazi nyuma na vile virefu vilivyo slimu vitasaidia kufanya miguu  mizuri mifupi minene kuonekana mirefu.

Wanawake wenye vifundo vya miguu vinene wafikirie mara mbili kabla ya kuamua kuvaa viatu vilivyochonga vidoleni. Viatu vya duara mbele vitawapendeza zaidi. Pia viatu vyenye rangi iliyokolea na kisigino cha wastani vitapeleka macho ya mtazamaji kwenye viatu zaidi na kuyaondoa  kwenye kifundo hivyo kuleta uwiano kwenye muonekano mzima wa mguu wa mvaaji. Kwa wenye miguu yenye vifundo vinene viatu vya kamba kamba za kuzungushia mguu mzima viepukwe. Viatu vya kisigino cha wastani na vilivyo wazi vidoleni vitafaa zaidi kuliko vile vya flat na kuzibwa kotekote.

Kama una umbile refu na kifundo chako cha mguu ni chembamba basi umebahatika! Kila aina ya kiatu kutoka flat za kuziba kotekote hadi michuchumio ni kwa ajili yako. Angalia usisitize viatu vya kuchongoka vidoleni na hata buti za kisigino kirefu ambazo pia ni nzuri kwa wanawake wafupi.

Kwenye tukio maalumu kila mhudhuriaji anapenda kuonekana na viatu vya kisasa kwa hiyo vaa viatu sahihi kwa mwili wako. Neno moja: Haijalishi una mwili gani miguu ya aina gani, michuchumio mara zote itakufanya uonekane mrefu na mwembamba – unahitaji nini tena cha zaidi!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

Wednesday, August 22, 2012

My Article for Newspaper: Suti Sahihi ya Mwanaume



Suti sahihi ya mwanaume

Suti inahuisha muonekano wa mwanaume yeyote.  Kwa ujumla watu wanamchukulia kivingine mwanaume aliyevaa suti sahihi. Bahati nzuri ni kuwa kuna ushahidi wa kisayansi ya kuwa jinsi unavyovaa inaleta hisia tofauti tofauti kwenye dunia inayokuzunguka.
Maarufu sana kati ya suti za kiume ni suti ya taksedo, ni suti ambayo pia inajulikana kuwa rasmi zaidi.

Suti za kiume zipo za makoti yenye vifungo vilivyojipanga mstari mmoja  na za makoti yenye vifungo vilivyojipanga mistari miwili. Hizi za vifungo vilivyojipanga mstari mmoja ni za kisasa zaidi na hazipitwi na wakati. Suti zenye mistari miwili ya vifungo zinawafaa wanaume warefu na wembamba  kwa kuwa hii mistari miwili ya vifungo inaleta muonekano wa upana kuliko zile za mstari mmoja. Kama mazingira ya kazi yako yanakuhitaji kuvaa suti kila siku suti za mistari miwili ya vifungo hazikufai.
Zaidi pia suti za kiume zinakuja kwa staili mbalimbali – kifungo kimoja, viwili na vitatu. 

Kuna kanuni za wewe mwanaume kufuata kabla hujaamua kununua suti yako mpya.

Kwanza, kitambaa na rangi vinachukua sehemu kubwa kwenye uchaguzi wa suti yako. Vitambaa vya pamba, linen na polista ni vizuri kwa suti. Kwa kuendana na wakati chagua suti ya rangi nyingine badala tu ya nyeusi iliyozoeleka.

ukijaribu suruali ya suti unayotaka kununua na ukiweza kuchomeka kiunoni vidole viwili bila kubana inakuhakikishia kuwa suruali hiyo ni sahihi kwako. Hii ni suruali utakayoweza kuvaa kama ukiongezeka uzito kidogo na pia ukiwa umeshiba. Kama una nyama za ziada tumboni suruali yenye vipindo kiunoni itakuwa nzuri zaidi kwako kuficha nyama ila kama ni mwembamba usivae yenye vipindo kwani itakufanya uwe mwembamba zaidi. Suruali iwe na urefu sahihi ukiwa umeivaa ifunike soksi. Ile mikunjo ya chini kabisa ya suruali ni mizuri kwa kusaidia kuleta uwiano wa uzito kufanya suruali itulie mwilini. Suruali isiyokuwa na mikunjo chini inamfanya mvaaji aonekane mrefu. Hata hivyo vijana wa kisasa wawe wafupi ama warefu wameonekana kupendelea zaidi suruali zisizokuwa na mikunjo ya chini. Mikunjo ya chini ya suruali ninayozungumzia hapa ni ile ya kukunjiwa kwa nje.

Chagua koti lenye mikono ya urefu sahihi kwako. Mikono mirefu sana au mifupi sana inafanya watu wafikirie hiyo suti labda umeazima. Mikono mirefu sana ya koti la suti ni ile iliyofunika kabisa shati; kwa maana hiyo hii haitakiwi. Mikono ya koti la suti yenye urefu sahihi ni ile ambayo shati uliloovaa ndani limetokeza nje kati ya nusu hadi inchi moja. Kwa maana hiyo mikono ya shati itokeze kidogo nje ya mikono ya koti la suti. 
Jisikilizie kama uko huru kutembea ukirusha mikono ukiwa umevaa suti yako. Isiwe taabu kunyoosha au kukunja mikono, kuhakikisha hili nyoosha mikono yako kwenda mbele. Urefu wa koti la suti uwe sahihi, ukiwa umesimama na kunyoosha mikono koti lifikie walau kati ya kiganja na kwenye ncha ya kidole chako cha kati.

Kwa swala zima la muonekano  wa suti sahihi ya mwanaume soksi zioane na suruali, mkanda uoane na viatu kwa rangi na tai iwe na urefu wa kugusa bakoli ya mkanda. Viatu au buti za kuvaa na suti ziwe nyembamba mbele na visiwe na kisigino kirefu. Kuvaa suti na viatu vya aina hii inaleta muonekano mzuri zaidi kuliko viatu vya duara mbele na visigino virefu. Kalamu zisiwekwe kwenye mfuko wa shati, ziwekwe kweye mfuko wa ndani wa koti la suti. Vilevile simu zinazovaliwa kwenye mkanda nazo si sahihi, pengine fikiria kubeba briefcase!

Zingatia kanuni kuu ya msingi ya vifungo vya koti la suti kuwa kwa koti la staili ya vifungo vilivyojipanga mstari mmoja unaweza ukawa umefunga vifungo vyote lakini kamwe usifunge kifungo cha chini. Kifungo cha chini cha koti la suti iwe ni staili ya vifungo viwili, vitatu ama vinne (kwa suti chache) kamwe hakikuwekwa ili kifungwe. Mara zote vifungo vyote vya staili ya koti la suti la vifungo vya mistari miwili vifungwe.

Suti ni vazi linaloonyesha mamlaka na utanashati kwa hiyo walau kila mwanaume anatakiwa kuwa na suti moja “inayomtoa” kwenye kabati lake la nguo hata kama havai suti mara kwa mara.  

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

Sunday, August 19, 2012

Mvua imefanya mambo..

Ian CAR WASH imependeza mapemaaa. Nimekumbuka wimbo mvua na jua kipi bora..
Wa kufanya waxing nao wapo. Zaidi ya kung'arisha gari wax pia inasaidia kulinda mafuta yaliyoko kwenye rangi za gari yako hivyo kufanya rangi idumu. Wax gari yako mara kwa mara.. na karibu Ian CAR WASH..0755 200023

Thursday, August 16, 2012

My Article for Newspaper: Mkanda unavyomtoa mwanamke bomba


Mwanamke anavyovutia akivaa mkanda kuendana na umbile lake
 
Mikanda sio rafiki wa kila mtu. Mkanda unaweza kuwa kitupio cha mitindo chenye changamoto kuvaa hasa kama huna umbile kama la wanamitindo. Kiukweli mkanda unaweza kuwa kinyume chako kwa kuonyesha yale maeneo ya mwili ambayo ungependa kuficha kama utachagua saizi, aina au kuvaa mahali pasipo sahihi.

Mikanda ya wanawake ipo iliyotengenezwa kwa ngozi, vitambaa, vito na kadhalika. Ipo ya rangi moja au yenye malighafi nyingine kama nyuzi, vito, mawe, bakoli na nyingine nyingi. Mikanda iliyozoeleka sana ni ya ngozi na vitambaa, chagua mkanda ambao sio tu unaendana na vazi lako, bali pia unaonyesha vyema umbo lako la kike. Kwa mfano mkanda mpana unapendeza kwa mwanamke mwenye umbo namba nane  kwa kutenganisha vyema kiuno hivyo kuleta mvuto kiunoni. Mkanda huo ukivaliwa sehemu nyembamba kuliko yote ya kiwiliwili – sehemu ya asili ya kiuno ambapo ni pale penye kitovu unasisitiza umbo halisi la kike na pia unamfanya mvaaji kuonekana slimu.

Kiasili mikanda ya wanawake ilivaliwa kwenye nyonga tuu ila karne hii inavaliwa popote kwenye kiwiliwili chake. Ipo inayovaliwa chini tu ya matiti, ipo inayovaliwa sehemu ya asili ya kiuno na ipo inayovaliwa chini ya kiuno karibia kabisa na makalio.

Inalipa kujaribu mikanda mbalimabali sehemu mbalimbali za kiwiliwili kuona matokeo tofauti tofauti. Pia zingatia aina na ukubwa wa bakoli kwa kuwa zinaweza kukuonyesha kiwiliwili kipana au chembamba. Usijali, kwa majaribio kadhaa utapata picha ya mkanda wa kukutoa bomba.

Kama baada ya kujifungua umebaki na tumbo kubwa wala usione aibu kuvaa mkanda. Mkanda uliovaliwa vyema kiunoni utanyonga tumbo na kukupa umbo namba nane. Mkanda mpana  wenye rangi zilizokolea unaovaliwa kwenye eneo asili la kiuno ( yaani pale kwenye kitovu) unakufanya uonekane tumbo slimu.  Usinyonge sana ili nyama zisigawanyike labda tu kama umevaa blauzi pana ambayo haitaonyesha mikunjo ya nyama.

Ukiwa umefungwa vyema mkanda wa kuzunguka nyonga ndio njia iliyozoeleka zaidi ya kuvaa mkanda na ambayo haipitwi na wakati. Vaa mkanda mwembamba au mpana nyongani na suruali au sketi ya mtindo wa katibu muhtasi au gauni la shifti au juu ya blauzi yenye vifungo. Ukivaa mkanda wa kwenye nyonga jitahidi kupunguza vitupio vingine na pia usivae na hereni au bangili za plastiki kwa ajili unawezekana kuonekana kama wa mwaka 47..

Jitahidi kuoanisha rangi kwa mfano, kama unavaa suruali pensi nyeupe na shati jeusi unaweza ukafikiria mkanda mweupe vile vile.

Kama mkanda utavaliwa karibia na makalio badala ya kwenye nyonga itasaidia kuondoa macho ya mtazamaji kwenye tumbo na kuelekezea kwenye mkanda. Pia kama una tumbo kubwa njia nyingine ni kuvaa mkanda chini tu ya matiti kuliko kiunoni kabisa. Mikanda inayovaliwa eneo hili la kiwiliwili inatakiwa kuwa myembamba na bila madoido. Vaa mkanda chini ya matiti pale tu nguo yako ikiwa ina vile vishikizo vya mkanda kwa ajili kama tujuavyo bila hivi vishikizo mkanda utang’ang’ania kushuka chini. Ila jua kuwa uvaaji huu wa mkanda utakufanya uonekane na kifua kikubwa.

Kama  una kiwiliwili kifupi unatakiwa kuvaa mkanda kwa jinsi ambayo kitaonekana ni kirefu. Chagua mkanda wa rangi ya jamii moja na nguo uliyovaa kwa ajili mkanda ukiwa na rangi tofauti kabisa na vazi utaleta mgawanyiko hivyo kufanya kiwiliwili kizidi kuonekana kifupi kwa kuonekana kimekatika nusu mbili. Kuvaa mkanda wa jamii moja na vazi ni njia pia ya kuonekana slimu hasa maeneo ya tumboni.
Kama una bahati ya kuwa na kiwiliwili cha umbo namba nane au umbo la tofali mkanda mpana ukivaliwa nyongani utakutoa bomba. Mkanda wa kiunoni utakufaa zaidi wewe mwenye umbile hili kulikoni ule wa chini ya matiti au wa kwenye makalio.

Miili midogo inapendeza na mikanda myembamba wakati wale wenye miili kikubwa wang’ang’anie mikanda mipana. Mikanda myembamba sana kwa miili mikubwa inaweza kuongeza ukubwa wa mwili wa mvaaji kimuonekano wakati ile minene na mipana kiasi italeta uwiano wa muonekano.

Uwe uwavyo mkanda kwa mwanamke ni sawa na polishi kwenye mbao huongeza mvuto kwa kila vazi. Kila leo mikanda inavaliwa kiubunifu zaidi kiasi kwamba unaweza kuazima mmojawapo hata kwenye kabati la nguo la patna wako.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

Monday, August 13, 2012

Asubuhi hii nimeanza na DFP

Karibu Ian Car Wash Survey tukuoshee gari yako..Tuna mashine ya kunyonya mchanga yenye hadhi ya viwandani, ukiosha mara 9 ya 10 ni bure na tunagarantii kukukabidhi gari safi iwezekanavyo.


Thursday, August 9, 2012

My Article for Newspaper: Kabati la sebuleni


Boresha sebule yako kwa kuweka kabati
Kabati la sebuleni mara nyingi ni ndefu linaloanzia sakafuni; ni mara chache kuona limening’inia ukutani isipokuwa kama ni vishelfu vidogo vya kusimamishia mapambo na maua. Kabati la sebuleni linaweza kutumika kuwekea luninga au mapambo pamoja na picha za familia.
Kabla hujaamua kuweka kabati sebuleni kwako kwanza tafakari matumizi yake na ukubwa wa sebule. Kwa mfano kama kabati ni la kuwekea luninga hakikisha kabla ya kuwa luninga husika itatosha. Pia amua kama unataka kabati mbili ndogo za kufanana au moja kubwa. Tafakari aina ya mbao ungependa kabati lako litengenezewe; mninga na mkongo kwa mfano ni mbao imara na zinazopendwa zaidi na zina urembo wa asili kwa ajili ya fenicha za sebuleni. Makabati ya sebuleni ya viwango ni ya mbao ngumu na ni ya gharama lakini utakapoamua kubadilisha kwa kuliuza gharama yake huwa haishulki sana na ni kitu cha kudumu miaka nenda rudi.

Unapoweka kabati acha nafasi ya kutosha watu kupishana sebuleni, kutoka nje, kwenda chumba kingine ama kwenda kwenye ujia.
Hakikisha kabati lako limemaliziwa vyema pande zote hasa nyuma ili usiliweke ligusane na ukuta. Kwa ajili nyuma kutakuwa kumetengenezwa vizuri kama pande zingine huna haja ya kuficha upande wa nyuma na ukuta kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakifanya ambapo ni makosa ya upangaji wa fenicha sebuleni kugusisha fenicha na ukuta.

Makabati ya sebuleni yanakuja kwa aina na maumbo mbalimbali ambapo inaweza kumfanya mtumiaji achaganyikiwe matumizi. Makala hii itakujuza aina ya makabati unayoweza kuweka chumba hiki ambacho kinatembelewa zaidi nyumbani kwako.

Uwe na sebule ndogo ama kubwa kuna aina mbalimbali za mkabati haya ambayo utapata ya kukidhi hitaji lako:

Makabati ya kuweka mapambo
Makabati haya ni kwa ajili ya kuweka mapambo unayopendelea yawe sebuleni kwako.  Makabati ya kuweka mapambo yanakuwa wazi mbele au yanakuwa yamewekwa kioo kwa hivyo vilivyomo ndani vinaonekana. Huwa ni madogo na yanasimama yenyewe toka chini au madogo sana kama vishelfu vilivyotengenezewa ukutani au kuninginia toka juu na ukawa umeweka mapambo yako ndani. Kwa kawaida huwa yametengenezewa taa kwa ndani ambayo huwashwa ili kuonyesha uzuri wa mapambo yaliyomo kabatini.

Makabati ya kuhifadhia
Kama una upungufu wa sehemu kwa ajili ya kuwa na sebule ndogo, tumia makabati ya kuhifadhia kama suluhisho. Mengi ya makabati ya kisasa ya sebuleni ya aina hii yana sehemu mbili yaani ya kuweka mapambo na madroo ya kuhifadhia. Unaweza kuonyesha mapambo yako na wakati huohuo ukahifadhi vitu kama majarida, CD za muziki na vitu vingine vidogodogo.

Makabati ya kuweka luninga
Hii ni fenicha ambayo kwenye sebule nyingi haiepukiki, asante kwa umaarufu wa luninga kama chombo muhimu zaidi cha burudani na habari! Pia yapo makabati ya kuweka luninga yanayotumika kuwekea mapambo na pia kwa kuhifadhia.  Weka ambalo litakidhi mahitaji yako.

Makabati ya Vitabu
Haya yanasaidia sana kuwekea vitabu, majarida na hata magazeti. Mapambo kama fremu za picha na vesi za maua juu ya makabati haya yanaongeza uzuri wa sebule. Makabati ya vitabu yamegawanywa kwa mashelfu madogo kwa ajili ya kuhifadhia vitabu vidogo na mashelfu makubwa kwa ajili ya vitabu vikubwa. Katikati ya mgawanyo huu kuna nafasi ambayo unaweza kuweka mapambo yako madogomadogo vilevile.

Makabati ya kituo cha burudani
Makabati haya uzuri wake ni kuwa yametengenezwa kwa jinsi ambayo kuna sehemu za kupitishia waya  na miungo ya vifaa vyako vya burudani vya elektroniki na kuficha nyaya hizi kwa ndani ili kufanya kituo kionekne nadhifu. Mara nyingi makabati haya yanakuja kama vipande vipande na mtumiaji anaunganisha mwenyewe hadi kabati zima linatokea.  Baadhi yake yamegawanywa viboksi vya saizi ya kuweka DVD na michezo ya elektroniki, eneo la luninga, spika za miziki na eneo la ziada kuhifadhia vifaa vingine.

Sebule zinatumika tofauti kwa kila familia. Kwenye nyumba nyingine sebule inatumika kama eneo maalum la familia nzima kukutana, wakati kwa wengine sebule imekaa zaidi kama chumba cha maonyesho, kinachotumika tuu pale mgeni anapotembelea nyumbani. Kwa matumizi yoyote yale, nyumba zenye sebule zenye kabati ni nadhifu zaidi.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

Saturday, August 4, 2012

Kazi yangu leo: Elastic Waist Top

shingoni
tumboni/kiunoni


Pamoja na ku vacuum magari kadhaa leo, nimeweza kubuni hii top. Blouse kama hii yenye lastic kiunoni ni bomba kwa yeyote awe na tumbo ama laa. Waweza kuulamba casual na suruali ya jeans au hata formal na sketi.

Friday, August 3, 2012

Rubbing Compound sasa ipo Ian CAR WASH

Rubbing compound kwa ajili ya kuondoa mikwaruzo kwenye gari yako sasa inapatikana Ian CAR WASH. Karibu ufanye mambo..0755 2000 23

Thursday, August 2, 2012

My Article for Newspaper: Mitindo; Wanawake Dhidi ya Wanaume


Mitindo; wanawake dhidi ya wanaume


Mara nyingi wanawake wanakuwa macho na mitindo zaidi ya wanaume – wakitafuta mitindo iliyopo na ambayo itawapendeza. Mwanamke atanunua majarida ya mitindo, kwenda kwenye mitandao kuangalia mitindo ya nyakati na ni nini wanamitindo wanaonyesha kwenye maonyesho mbalimbali ya mavazi. Hata hivyo, wanaume wengi hawako hivyo, wao wanavaa kile tu wanachojisikia watakuwa huru. Kwa nini kuna tofauti ya mtizamo wa mitindo kati ya wanawake na wanaume; na je jinsia ya kiume kweli inajali kama mwanamke anavaa kuendana na wakati ama laa?

Msisitizo wa uzuri wa mwanamke unaongezeka kila kukicha. Jinsia ya kike inaonekana kupendelea na kuthamini zaidi kuvaa kuendana na mtindo uliopo. Katika ulimwengu wa mablog na mitandao mingine ya kijamii wanawake wamekuwa wakiweka picha zenye kuonyesha mitindo yao wakiwa wametoklezea bomba (na wanaume nao wanaelekea hukohuko). Kutokana na kuwa macho juu na mitindo wanawake mara nyingi kuwa na hela na muda wa kufanya manunuzi ya haraka na mwishomwisho kwa ajili ya viwalo vya mtoko wa jioni na shoga zake sio kitu cha kushangaza. Wanaume kwa upande mwingine wamekuwa wakionekna kama hawana ubunifu sana wa kujua wanavaa nini. Hata hivyo hisia hizi zinaonekana kuyeyuka kadri siku zinavyosoga kwani wengi wameonekna wakiwa madukani wakicheki ni raba gani zitakazoendana na kaptula zao za jinzi.

Kupata toleo jipya la gauni linaloshika kiuno ni njia ya urembo kwa wanawake karne hii. Tasnia ya mitindo nayo imejikita zaidi kwa wanawake – majarida mengi yanatoa dondoo na miongozo ya mitindo ya kike, kwa mfano ni wapi pa kununua magauni ya maksi wakati huo huo majarida haya hayatoi mwongozo huu kwa wanaume.

Pamoja na kuwa muonekano wa mwanamke umekuwa sehemu kubwa ya mitindo ya kike historia inaonyesha kuwa tangu kale mwanamke kuvaa kuendana na wakati kumemfanya ajisikie yuko juu na wa kisasa zaidi. Kupitia mitindo mwanamke anaongeza kujiamini kwake wakati kwa wanaume ni tofauti. Wanaume wao wanaongeza kujiamini kwao kwa njia nyingine ambazo sio mitindo ambazo zinaweza zikaeleza kwa nini wanaume wanavutiwa sana na mazoezi ya kuongeza misuli na ukakamavu kinyume na kuwa macho juu kujua ni mitindo gani ya nguo za usiku za kiangazi imeingia kwenye maonyesho na madukani.

Burudani kwa sehemu kubwa imechangia wanawake kuvutiwa na mitindo.  Bila kuwa na mvuto kwenye sanaa ya mitindo tasnia hii isingekuwepo. Kwa wengine ni njia ya maisha, kazi zinapatikana kutokana na mitindo. Wakati kufuatilia mitindo ni kwa wanawake ni kama labda mpira wa miguu wa wanaume – kitu wanachopendela na ni burudani kwao.

Wakati kuna wanaume pia wanaopenda kufuatilia mambo ya mitindo, wanawake wanajijali zaidi muonekano wao na ni nini wanavaa. Hata hivyo ulimwegu unabadilika kila siku na karne zijazo huenda wanaume wakawapiku wanawake kwenye kufuatilia mambo ya mitindo.

Mwanamke anapenda upekee na staili za kivyakevyake zaidi ya mwanaume alivyo. Hebu fikiria kisa hiki: Mwanamke anaingia kwenye mkusanyiko na kukuta wanawake wengine wawili wamevaa gauni kama lake. Kwa mwanamke yeyote yule atashangaa hee imekuwaje! Na kama mwanamke huyo ni mtu maarufu kama walio na wasaidizi binafsi wa kuwapangia nguo za kuvaa basi hata huyo msaidizi huenda akafukuzwa kazi kuwa alimchaguliaje gauni kama sare ya shule. Sasa tuangalie kisa hikihiki kwa upande wa wanaume.  Mwanaume ameingia kwenye sherehe na kukuta wanaume wengine wawili au watatu wamevaa suti kama yake.  Wanaume wengi watachukulia hii kama chanya. Fikra kama: “inaonekana kama nimevaa sahihi kwa ajili ya tukio hili” au “ niko mahali sahihi” mawazo haya yatakuja akilini mwa wanaume walio wengi.  

Kwa kuwa wanawake wengi wanapenda staili za peke yao zaidi ya wanaume walivyo wabunifu wengi wa mavazi wameweka nguvu zaidi kwenye mavazi ya kike. Pia ukisoma historia za wabunifu wengi maarufu walianza kubuni mavazi ya wanawake kabla ya kubuni ya wanaume.

Mwanamke usimkasirikie patna wako kuwa haulambi, wanaume wanapenda kuvaa wajisikie huru na kwao haijalishi sana kama ni mtindo uliopo ama laa.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 200023