Tuesday, June 18, 2013

My article for newspaper: Bustani usiku




Furahia bustani yako hata baada ya giza kuingia


Kwa wale wenye bustani zao binafsi, kutumia muda bustanini ni wasaa wanaoupenda sana. Eneo la nje la bustani ni moja ya vitu vichache vya thamani unavyopata katika ulimwengu huu ambapo unaweza kukaa, kustarehe, kufurahia na kushangaa uzuri wa mimea na hewa ya asili. Kuwa na mwanga wa kutosha bustanini nyakati za usiku mara nyingi inawaruhusu wenye bustani kurefusha muda wanaoweza kutumia kwenye eneo hili la nje ya nyumba zao.

Ili kuweza kuwa na mwanga kwenye bustani inabidi kuweka taa za bustanini mbali na zile za ulinzi. Taa hizi zinarahisisha maisha ya usiku ya kwenye bustani na zipo za aina mbalimbali kama vile za kuonyesha njia, zenye matawi zinazowekwa kwa ajili ya  kusisitiza eneo fulani la bustani, za chini ya maji kwa mfano kwenye bwawa au maanguko ya maji na zile zinazoweza kutundikwa kwenye miti.

Taa za bustanini zina malengo mawili: kuangaza na kupamba. Kama zilivyo nyanja nyingine za ubunifu wa bustani, malengo haya mawili yanaendana bega kwa bega ili kuleta muonekano wa bustani ya kuvutia. Ingawa mmoja anaweza kumulika bustani nzima kwa kuweka taa za mwanga mkali na kuondoa dalili yoyote ya giza, hii italeta muonekano usiovutia. Vilevile mwingine anaweza kuweka taa chache tu za kusaidia miguu kuona eneo la kukanyaga kwenye njia ya bustani. Hata hivyo hii itafanya eneo lingine lote la bustani kubaki karibia sawa na giza, kumzuia mtazamaji kufurahia uzuri wa bustani usiku.

Mpango wako wa kuweka mwanga kwenye bustani unatakiwa kuweza kuleta suluhisho kwa hali zote hizi mbili. Nia ya mwanga kwenye bustani ni rahisi. Chagua ni nini kwenye bustani yako ungependa kionekane zaidi kwa wageni wako, na ni shughuli gani unayotaka kuifanya kwenye bustani.

Je huwa unaburudisha kwenye bustani yako? Kama una varanda au fenicha kwenye bustani yako, fikiria mfumo wa mwanga kwenye bustani ambao utaruhusu wageni kufurahia bustani usiku nyakati za kiangazi. Kama wewe ni mmojawapo wa wanaopenda kualika wageni chakula cha usiku kwenye bustani yako hakikisha mfumo wa mwanga unawezesha mgeni kuona anachokula toka kwenye sahani yake. Kama una watoto wanaopenda kucheza kwenye bustani usiku hakikisha una taa moja au mbili za mwanga mkali ambazo unaweza kuwasha wakati wa michezo na kuzizima michezo ikiisha.

Kila mwenye bustani lazima ana walau ukanda mmoja au zaidi wa maua, au eneo mojawapo kama vile bwawa au hata mti ambao unaufurahia. Weka mfumo wa mwanga kwenye bustani ambao utawezesha wageni wako kuona vitu unavyopenda waone kwenye bustani yako usiku kama vile wangeweza kuviona machana. Kwa mfano taa zenye matawi zinafaa sana kumulika eneo fulani la bustani kulifanya lionekane zaidi kuliko maeneo mengine wakati wa usiku.

Taa za chini ya maji ni aina ya taa za bustani zinazowekwa maeneo ya kwenye bwawa, maanguko ya maji na maeneo mengine yanayofanana na hayo. Taa hizi huwa zinawekwa chini ya eneo la maji ili kusaidia kufanya eneo hilo lionekane zaidi nyakati za usiku. Na huwa taa hizi zipo hata za rangi kwa nia ni ile ile ya kuonekana zaidi na vile vile kuleta staili.

Taa za mwanga mkali za kwenye bustani pia zinaweza kutumika kama taa za ulinzi. Taa hizi zinaweza kuunganishwa na vihisi mwendo (motion sensor) ambapo ikiwa mvamizi atatokea anazama kwenye mwanga mkali hivyo kukwamisha mkakati wake wa kivamizi.
Kimsingi, mpango mzima wa mwanga kwenye bustani uwekwe kwa jinsi ambayo mgeni halazimiki kujua umbo la taa bali kuona mwanga tu. Cha muhimu ni aone vile vinavyomulikwa, vile unavyotaka aone kwenye bustani yako, pengine ni mti, njia, bwawa, maanguko ya maji na kadhalika. Kwa hivyo taa za bustani zilizowekwa kwenye urefu wa kutosha wa kile unachotaka kionekane zitasaidia kukionyesha kitu hicho tu huku kukiwa na kivuli maeneo ya jirani hivyo kuleta mvuto wa aina fulani ukilinganisha na kuona kitu kile kile wakati wa mchana.

Kwenye mfumo wako wa taa za kwenye bustani unaweza ukachanganya pia taa za rangi. Taa za rangi za kwenye bustani zinatumika zaidi kama mapambo ya msimu wa sikukuu. Hata hivyo  taa za rangi zilizowekwa kwenye mpangilio wenye ladha unaweza kuongeza uzuri wa muonekano mzima wa bustani. Aina fulani ya maua inaweza kubadilika kabisa kutokana na kumulikwa kwa taa za rangi wakati mengine yanaweza kufunikwa yasionekane. Na unaweza kuwa na balbu moja au mbili za rangi mkononi mahususi kwa kubadili na zilizopo kuendana na msimu.
Wakati wa kuchagua taa za bustani fikiria mimea na vitu vingine kwenye bustani yako vinavyoakisi mwanga kwa sana. Mimea na vitu visivyoakisi mwanga kwa sana vinahitaji mwanga mkubwa zaidi kuvifanya vionekane.

Hata kama mfumo wa mwanga wa kwenye bustani haukuhusishwa kwenye mpango wa awali wa bustani unaweza kuweka taa za jua na paneli za kuchaji wakati wa jua badala ya zile za kutumia umeme ambapo hizi za umeme zinahitaji kutandika nyaya tokea awali na kadhalika. Kwa hivyo taa hizi za kutumia mwanga wa jua zinakuwa bei nafuu kwa kuwa bustani yoyote inapokea mwanga wa jua bure.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

Wednesday, June 12, 2013

My article for newspaper: njia za kuhifadhi taulo




Unavyoweza kuhifadhi taulo zako za bafuni

Ni bafu chache zenye sehemu ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi taulo. Lakini usijali kwani hata kama bafu lako ni dogo namna gani njia mojawapo kati ya hizi itakufaa kutundika ama kuhifadhi taulo zako.

Kuweka fimbo za kutundika taulo kwenye ukuta wa bafu ama nyuma ya mlango (uwe wa mbao kwa uimara) ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi taulo zako. Fimbo za kutundikia taulo hazichukui nafasi kubwa na wala hazina marembo kwa hivyo ni suluhisho tosha kuhifadhi taulo zako kavu na hata zile zenye unyevu. Fimbo za taulo zinaruhusu taulo kukauka kwa usafi zikiwa zimetundikwa kwa kukunjwa nusu. Fimbo za bafuni za kuwekea taulo zinasaidia mambo makubwa mawili: kwanza, zinaweka taulo kavu na safi kwa jinsi ambayo ni rahisi kuchukua na kutumia; pili, zinatandazwa taulo zenye unyevu na kuzifanya kukauka rahisi, kwa hivyo kuzuia kuota kwa ukungu. Licha ya kufungwa bafuni fimbo za taulo zinaweza kufungwa pia jikoni kwa ajili ya kuwekea taulo za mkononi.

Muonekano wa fimbo za taulo ni kawaida sana. Ni fimbo iliyowekwa ukutani ama nyuma ya mlango kwa kutumia mashine ya kutobolea ukuta na taulo huwekwa hapo, hutolewa kutumika na hurudishwa tena hapo baada ya kutumika kwa ajili ya kukauka. Ni muhimu fimbo hizi ziwe zimeweka imara  kwa kuwa kama tujuavyo taulo zikiwa mbichi zinakuwa nzito na pia mara nyingine fimbo hizi hutumika na watoto (wakati mwingine ni kwa utundu wao wa kupenda kubembea kila waonapo panafaa) ama wazee kujishikilia wakiwa bafuni. Kwa hivyo siwezi kuacha kusisitiza kuwa fimbo za taulo ni lazima zifungwe kwenye ukuta wa tofali ama mlango wa mbao kwa ajili ya uimara.

Fimbo za kuwekea taulo zinapatikana kwenye maduka ya fenicha za nyumbani na zimetengenezwa kwa chuma. Saizi ambazo ziko kwa wingi ni inchi 18 kwa ajili ya taulo za mkononi na inchi 24 kwa ajili ya taulo za kuogea. Hakikisha umeshatathmini bafu lako na kuamua ni wapi pa kuchimbia fimbo ya taulo na uone pana nafasi ya kutosha urefu wa fimbo zilizopo sokoni.

Fimbo za taulo sizo tu zinazoweza kuhifadhi taulo kwa usafi na kuruhusu zile zenye unyevu kukauka. Kulabu (hook) za taulo, susu (rack) za kusimama wima, bangili na ngazi za taulo nazo ni njia nyingine za kuhifadhi taulo za bafuni. Bangili iliyotobolewa ukutani ambapo taulo kadhaa zinatundikwa ni maarufu sana siku hizi na kwenye maduka ya fenicha wanaziita bangili za taulo. Chuma kingine kinachoonekana kama ngazi ndogo ambacho hutumika kuwekea taulo nacho ni njia mojawapo ya kuhifadhi taulo za bafuni. Je una nafasi kwenye ukuta wa chumba chako cha kulala ambapo unaweza kuweka ngazi hii? Ni kiasi cha kuishikilia na braketi juu ili isianguke na unaweza kuhifadhi kwa kutandaza taulo zako za kuogea. Uzuri wa ngazi ya taulo ukilinganisha na fimbo ni kuwa wakati kwenye fimbo unaweza kuweka taulo zisizozidi 2 kwenye ngazi ya taulo unaweza kuweka hadi taulo 6.

Lakini kuna njia nyingine ambazo hazitakufanya uusumbue ukuta wako ambazo zinaonekana za kimapambo zaidi kwa mfano kuweka susu ya kusimama inayojitegemea kama ile ya kutundika makoti ofsini. Kama chumba chako cha kulala kina nafasi kidogo ya ziada basi simamaisha susu ya koti kwa ajili ya kutundikia taulo za bafuni. Susu inaweza kutundikwa taulo kadhaa kwa wakati mmoja. Fikiria kuiweka sehemu ambayo inaingiza hewa au vinginevyo uwe unazigeuza mara kadhaa kuwezesha kukauka. Kama susu hii inatundika taulo za wanafamilia tofauti basi wawe na taulo za rangi tofauti kwa kila mmoja. Hakuna anayependa kushirikiana taulo.

Badala ya ile susu ya kusimama kuna hii nyingine inayofanana na ya kuhifadhia chupa za mvinyo. Baadhi ya watu hawafikirii kutumia taulo za bafuni zaidi ya mara moja kabla hawajaziweka kwenye kapu la nguo chafu ili kufuliwa. Nenda kistaili zaidi kwa kuhifadhi taulo zako safi zilizobiringishwa vizuri kwenye susu ya taulo. Susu za taulo zina muonekano wa kuvutia kwa hivyo kwa upande mwingine ni kama pambo. Taulo safi zinabakia zimebiringishwa vizuri ndani ya susu hadi wakati wa kutumiwa, na hii inachukua nafasi kidogo kuliko ile susu ya kusimama. Kuhifadhi taulo kwa kutumia susu ya taulo inakubidi uwe ni mtu wa kutumia taulo mara moja tu na kulifua.

Kwa hivyo kama ulijisikia kwamba bafu lako ni dogo kiasi kwamba huna mahali pa kuhifadhi taulo zako hatimaye leo umefahamu njia kadhaa za kuweza kuhifadhi na kutunza taulo zako wakati huohuo ukiwa unazitumia. Wekeza katika njia mojawapo kati ya hizi ili kurahisisha maisha bafuni.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023