Thursday, April 24, 2014

my article for newspaper: garden entrance


Jinsi ya kutengeneza na umuhimu wa eneo la kuingia kwenye bustani
Eneo la kuingia kwenye bustani ya maua ni kiungo muhimu cha bustani ya nyumba yako. Ni eneo sahihi la wewe mwenye bustani kuonyesha ladha na ubunifu wako binafsi.
Muonekano wa kuvutia wa eneo hili sio tu unaboresha muonekano wa bustani bali pia ni ishara kwa wageni wako kuwa wameshafika bustanini.  Eneo hili ni kama linasema“hapa ndio mahali panapoanzia bustani yangu ya nyumbani,” anasema mbunifu wa bustani Bi Tatu Mbegu.
Kuna staili nyingi tofauti za eneo la kuingia kwenye bustani au sehemu nyingine ya nje ya nyumba. Katika makala hii mbunifu Tatu Mbegu anakushauri aina hizi mbalimbali na ndipo utakapoweza kuamua ni ipi itafaa kwenye bustani yako.

Sehemu ya kuingia kwenye bustani inaweza kuwa eneo rahisi tu kwa mfano mawe mawili yaliyowekwa mkabala katika eneo hilo, vyungu vya maua, kiingilio kama fremu ya mlango kwa mfano wa vibao vya kupishana au hata chuma, milingoti miwili iliyozungushiwa mimea mitambaazi na hata geti la chuma na kadhalika na kadhalika. Uwezekano ni mwingi na upeo ni mwisho wa ubunifu wako. Vizuri, kitu muhimu cha kufahamu ni kuwa ni eneo la mwanzo linaloonekana kabla ya kuingia kwenye bustani, anasema Tatu. Eneo hili linatoa tamko la papo kwa papo la utambulisho wa mwenye bustani na linaleta mguso wa eneo lingine lote la bustani lililobakia.

Mbao na chuma zinaweza kuchanganywa kwa uzuri na kufanya eneo la kuingia. Vifaa vya ujenzi navyo vinafanya wigo mpana wa kuchagua mtindo wa muonekano wa eneo hilo. Kama unadhani mbao zinaonekana kuoza sana ndani ya muda mfupi basi tumia chuma peke yake.
Pamoja na hayo ni muhimu kufahamu kuwa sio kila eneo la kuingia kwenye bustani liko mbele ya nyumba. Wengine hupendela kugawa bustani kwenye vyumba na hivyo kuwa na maeneo tofauti ya kuingia katika kila chumba.

Kuzungushia hiyo fremu ya eneo la kuingia kwa mimea na maua inaonyesha ubunifu zaidi. Mgeni anayepita chini ya kivuli anafunikwa na kijani na hivyo kujisikia burudani kwa hewa safi.
Hii yote inatokana na ladha ya mwenye nyumba, muonekano na bajeti. Eneo la kuvutia la kuingia kwenye bustani ni utambulisho wako kwa mapambo yako ya nyumbani.

Sasa unaanzaje kupata mawazo ya jinsi ya kutengeneza eneo la kuingia? Bi Tatu anajibu swali hili kwa kusema kuwa anza kubuni kwa kuangalia kwanza bustani yako kwa ujumla. Ni wapi ungependa kuweka eneo la kuingilia? Wakati mwingine uamuzi unatokana na eneo lililozoeleka kupitwa hapo kabla, na pia ni jinsi gani ungependa wageni waifikie nyumba yako? Je unapenda kubuni njia ya moja kwa moja kutoka kwenye bustani kuingia kwenye nyumba ama kuwe na kona ya kuingia kwenye bustani kwanza kabla ya kufikia mlango wa mbele wa nyumba?
Halafu jifanye kama wewe ni mgeni kwenye makazi yako mwenyewe. Jiulize kama ungefika mahali hapo kwa mara ya kwanza ni wapi ungepitia kufika bustanini. Sasa weka baadhi ya maelezo haya kwenye mawazo yako ya kuamua ni wapi utengeneze sehemu ya kuingia kwenye bustani yako.
Hakikisha kuwa utatumia njia yako ya kuingilia kwenye bustani. Hii ina maana kuwa kama utaitengeneza mahali ambapo huvutiwi kupitia basi ni dhahiri kuwa utaitumia kwa mara chache sana au hata inawezekana hutaitumia kabisa. Kwa hiyo kabla hujatengeneza njia hakikisha kuwa utaitumia.

Muonekano wa eneo la kuingilia uwe ni muendelezo wa mapambo mengine ya nyumba yako. Kama nafasi inaruhusu tengeneza eneo la kutosha kwa ajili ya kupitia watu kadhaa. Eneo la kuingilia la upana mdogo zaidi ni mita moja na nusu kwa bustani ya wastani hadi mita mbili na nusu kwa bustani kubwa, anasema Bi Tatu.

Mwisho fikiria bajeti; haihitaji hela nyingi kutengeneza eneo la kuingia kwenye bustani. Kama mbunifu alivyosema kuwa hata vyungu viwili vilivyooteshwa maua vikawekwa mkabala vinaweza kufanya eneo la kuingia kwenye bustani, au hata boda za maua zilizozunguka bustani zinaweza kuachwa nafasi ya eneo la kuingilia na ikawa ndio hicho tu unachohitaji. Ni rahisi tu kama hivyo wala haihitaji mambo makubwa.
Wawezeshe wageni wako kupunguza mwendo wanapofikia bustani yako kwa kuweka njia ya kuingilia, watafurahia kwa undani maua mazuri na mimea laini ya bustani yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Wednesday, April 23, 2014

my everyday life....hapa na pale baada ya weekend ndefu..

marafiki zangu waukweli wamerudi shule


kuelekea kwenye mishe..mambo mazuri yanakuja..
kwa nini unachukua pima joto yangu..

Tuesday, April 22, 2014

block pavers na mvua ni kama zimepigwa deki!

makoko yote yameng'olewa na mvua...ni zaidi ya kupiga mashine ya pressure
p
vitofali viking'aa na miguu inang'aa

Thursday, April 17, 2014

makala ya kabati la sebuleni ilibamba zaidi...

hakika wasomaji wengi wanavutiwa na makala ya kabati la sebuleni.
makala hii imekuwa ikipotelea na kurudi kila mara kwa ajili ya wasomaji wapya kuivuta tena na kuisoma na hata wengine wanadhani kuwa nauza haya makabati.
ukitaka kabati la staili yoyote ni kiasi cha kuteta na fundi anayejua kazi yake, kumnunulia vifaa na anakutengenezea kwa ladha yako mwaya..

Tuesday, April 15, 2014

my article for newspaper: umuhimu wa dressing table nyumbani

Kumpenda mwingine, ni muhimu kujipenda mwenyewe kwanza. Mtu anatakiwa kujithamini utu wake mwenyewe na kujifurahia alivyo. Kila mmoja anajiona mzuri mbele ya kifaa kinachoitwa kioo, ambacho kinatuonyesha sura zetu zilivyo. Wengi wanapenda kutumia muda mwingi ndani ya sehemu ya nyumba palipo na kioo kwa maana ya kuwa sehemu ya kuvalia yenye kioo. Hapo mahali ni kwenye dressing table! Meza ya kuvalia kwa lugha nyingine dressing table ikiwa imeambatanishwa na droo, kioo na kiti ni fenicha muhimu mno ndani ya nyumba ya kuishi.
Kuna aina kadha wa kadha za fenicha ambazo ni kama zimepuuzwa katika baadhi ya nyumba. Meza ya kuvalia ni le aina ya fenicha ambayo ni muhimu sana kuwa katika kila nyumba ambapo sio tu kwamba inaongeza uzuri na rehema ndani ya nyumba bali pia inaonyesha ushirikiano mkubwa  katika matumizi yake.
Vioo vilivyoko kwenye meza ya kuvalia vinasaidia mno kwa kuwezesha wewe mwanamke mzuri na mwanaume bomba kujiandaa vyema wakati wa kuvaa na hivyo kutoka nyumbani ukiwa unajiamini. Kiti kidogo ama kistuli cha meza ya kuvalia kinakusaidia kukaa na kujiandaa kwa kuvaa, kutupia na kuweka vipodozi vyako bila wasiwasi huku ukijitazama kwenye vioo. Hasa wanawake huwa tunachukua muda wa kujiandaa na kupaka vipodozi, kiti kinahtajika sana wakati huo. Pia fahamu kuwa hiki kiti au kistuli cha meza ya kuvalia huwa ni kidogo kwa hivyo hakisababishi mrundikano kwenye chumba chako.
Droo za meza ya kuvalia hutumika kuhifadhi vitu mbalimbali hivyo kuwa rahisi kupata kile unachohitaji mara moja.
Kwa kawaida huwa meza ya kuvalia ina droo 3 hadi 4 ambazo hutumika kuhifadhia vitu kadhaa. Meza hii inaakisi utambulisho wa mtu anayeitumia. Kwa mfano, bachela atajaza meza yake kwa kila aina ya deodoranti, pafyumu, nguo za ndani, mikanda na wakati mwingine hata mipira ya kiume miwili au mitatu! Mwanamke naye anaweza kuhifadhi vitu kama vile nguo (kwenye droo zake), kuhifadhi vipodozi na manukato, kuhifadhi vitupio kama bangili, shanga, mikufu na hereni. Meza hii pia huwa hutumika kuhifadhi vitu vya faragha kama nguo za ndani kwa vile mara nyingi huwa inawekwa chumba cha kulala.

Meza za kuvalia zinapataikaan za aina na mitindo mbalimbali. Zipo za mbao, chuma na hata plastiki ngumu na kadhalika. Unaweza kununua yeyote ambayo inafaa kwa nyumba yako na inaendana vyema na mapambo yako mengine ya ndani. Gharama pia zitatofautiana kuendana na kifaa kilichotumika kutengenezea meza na pia aina ya kioo, anasema seremala Musa Hussein. Meza nyingine huwa zina vioo viwili ambapo unaweza kujiona nyuma na mbele.
Unaweza kununua meza iliyotengenezwa tayari au unaweza kupeleka oda yako kwa fundi akakutengenezea. Kama fundi atafanya kazi nzuri meza ya kuvalia ya kubuni mwenyewe inaweza kukupa burudiko la kudumu. Kufahamu mitindo iliyopo tembelea mitandao na soma majarida mbalimbali yanayohusu mapambo ya nyumbani. Wakati wa kuoda au kununua ni vyema kuzingatia sehemu au chumba utakachoweka seti yako hiyo. Kila mmoja ana ladha yake binafsi linapokuja swala la kununua fenicha za nyumbani, ila ni vyema kupokea ushauri wa wanafamilia wengine ama hata wabunifu wa ndani kabla ya kuamua kununua aina fulani ya meza ya kuvalia.
Kwa kawaida meza hii inakaa chumba cha kulala ingawa baadhi ya wabunifu wa fenicha wanashauri iwekwe bafuni kama una eneo kubwa, na hata zipo meza za kisasa zaidi zilizounganishiwa umeme kwa ajili ya kutumia vikaushia vywele na visafisha uso vya mvuke.
Meza ya kuvalia ilivumbuliwa kukusaidia kujiandaa ukiwa huru na amani tele kwenye chumba chako mwenyewe cha kulala. Unaweza kujiremba na kujipendezesha kwa raha zako kwenye meza hii.

Unaweza sasa ukatafakari ni kwa jinsi gani unaweza kuwa mbunifu kwa kutumia dressing table na droo zake maridadi bila kusahau kioo na kiti chake cha staili. Ni fenicha muhimu mno kuwa nayo. Pia usisahau kuwa meza ya kuvalia ni kituo cha vitu vyako vingi ambavyo vingeweza kuwa vimewekwa maeneo mengine chumbani na kuleta muonekano wa mrundikano. Chumba cha kulala kinasemekana hakijakamilika bila kuwa na eneo hili la kuvalia kwenye ukuta wake mmojawapo.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Friday, April 11, 2014

friday finest

mvua za hapa na pale leo zimefanya hali ya hewa iwe ya kiubaridi ila madimbwi sasa...kukaa ndani kunalipa ukiwa umejivalia soksi na kujikunyata kiaina...weekend njema wapendwa..


Tuesday, April 8, 2014

my article for newspaper: chumba cha binti - tumboni hadi 18


Karibu msomaji kwenye makala ya leo ambayo nitaongelea jinsi ya kupamba chumba cha kulala cha binti yako miezi michache kabla hajazaliwa hadi akiwa na umri wa miaka 18.  Fuatana nami kwenye makala hii.
Sasa basi ni miezi michache imebaki kabla binti yako hajazaliwa. Kutokana na teknolojia kuwa juu mama mjamzito amepewa uwezo wa kujua jinsia ya mtoto wake aliye tumboni kama atapenda kufanya hivyo. Endapo basi wazazi watakuwa wanatarajia kuna binti yao anakuja duniani basi moja kwa moja wanaanza kufikiria kitanda cha mtoto na nguo na mapambo ya rangi za pinki, njano na kijani ambazo zitatawala chumba cha kijacho. Wakati ukiwa kwenye maandalizi hayo ni vyema ukaandaa kwa kufikiria miaka mitano hadi kumi mbeleni.

Kutokana na ukali wa maisha jaribu kuweka vitu ambavyo ni vya kudumu kwa kukumbuka kuwa kila kitu unachoweka kwenye chumba hiki ni chake na atakitumia kwa miaka 18 inayofuata  na hata kama ni mabadiliko yawe madogo yasiyo na gharama kubwa. Sasa utaniuliza je, kitanda cha mtoto kitatumika kwa miaka 18?  Endelea kujisomea ili upate jibu la hili swali. Rangi za pinki, njano na kijani nazo pia ni sawa kwa chumba cha mtoto wako wa kike mchanga lakini jaribu kutumia rangi ambazo zinakaa kati. Kwa mfano ukitumia pinki iliyokolea na njano ya mwanga wa jua kama rangi za ukuta wa chumba cha binti yako vitadumu hata atakapokuwa mkubwa na ataipenda pinki hii kuliko ile nyepesi ya kitoto!

Kununua fenicha ambazo zina matumizi zaidi ya moja na ambazo zinaweza kukaa kwenye chumba hicho kwa muda mrefu inaweza kuwa changamoto kuliko swala la rangi. Unahitaji kutembelea maduka mbalimbali ya fenicha na pia karakana za waseremala. Wote tunajua kile kitanda cha kichanga binti yako hawezi kukitumia kwa miaka 18 ijayo. Ni sawa kuwa na kitanda cha mtoto kwa ajili kina vizuizi pembeni ili asianguke. Ila ili kuweza kuwa na matumizi ya kitanda hiki kwa umri wote wa utoto wa binti yako tafuta kitanda cha bebi ambacho kinaweza kugeuzwa na kuwa cha binti hapo baadaye. Kuna baadhi ya maduka ya fenicha ambayo unaweza kupata kitanda kama hiki. Vinginevyo unaweza kwenda kwenye karakana za waseremala na kuagiza utengenezewe kitanda cha kikubwa ila kiwekwe vizuizi ambavyo vitafanya kazi kama ile ya kitanda cha bebi.
Hapo baadae kadri binti yako anavyokua unapamba chumba chake upya ambapo utaondoa vizuizi na kitabakia kuwa kitanda cha binti na sio bebi tena. Mzazi siku hizi usitafute kitanda cha bebi kinachosimama peke yake. 

Tafuta ambacho bebi yako pia atakitumia akiwa binti, kwa njia hii utakuwa umetumia pesa yako kwa busara. Usitumie hela nyingi na uchumi huu kununua vitu ambavyo utaviondoa tena miaka michache itakayokuja. Kama unataka kuongeza kitu kwenye chumba cha mtoto wako ambacho anafurahia sasa lakini sio hapo baadaye hakikisha sio cha gharama kubwa na ni rahisi kukiondoa.

Chumba cha kulala cha binti yako ni sehemu ambayo atatumia muda mwingi zaidi wakati akiwa msichana mdogo, atakuwa analala hapo pia wakati mwingine atacheza na madoli yake hapo. Kuwa mbunifu kwenye kupamba chumba hiki na utumie gharama za kawaida. Weka zulia la rangi moja ambalo utaweza kutupia kizulia kingine kidogo cha rangirangi juu yake pale pembeni ya kitanda. Kizulia hili kidogo rangi kuu ziwe zinaendana na rangi nyingine za hapo chumbani hata kama ni pazia ama shuka ama ukuta. Zulia litasaidia kuweka miguu ya bintiyo kwenye joto na hata akiwa amekaa chini na pia linaongeza uzuri wa muonekano wa chumba. Mwekee shuka, mito na pazia zinazooana na rangi ya mandhari uliyochagua. Chagua pazia na shuka za kike na pia zenye rangirangi kama maua au nyota au hata rangi za upinde wa mvua.

Hatimaye binti yako mdogo anaanza chekechea; muda unakimbia. Weka mpangilio wa chumba kivingine ili kutengeneza nafasi kubwa ya kucheza na matoi na kusuka madoli yake. Kadri binti anavyokua, ladha yake inabadilika kwa kasi siku hadi siku achilia mbali mwaka hadi mwaka. Unaweza ukatetea kutumia hela kwa umakini kwa ajili ya chumba chake kwa kujua ni nini cha kununua na jinsi ya kukitumia.

Unapamba chumba chake tena kwa awamu nyingine ya kikubwa. Chagua mandhari itakayotokana na vitu na rangi anazopendelea binti yako kabla ya kumshtukiza na kuanza kupanga na kuweka vitu upya chumbani kwake. Pia unaweza kupamba nae pamoja. Anza kwa kupaka tena rangi na baada ya hapo ongeza fenicha ambazo bintiyo atahitaji ambazo ni kimeza na kiti chake , meza ya kuvalia, kisofa kidogo na kishelfu cha vitabu. 

Rangi ya vitu hivi iendane na mandhari uliyochagua. Kwa mfano kama mandhari ni rangi ya pinki, usiweke sofa ambalo halioani na pinki. Pia sasa ni wakati wa kuondoa zile mbao za kuzuia asianguke na kitanda kubakia cha binti mdogo sio kile cha kichanga tena.

Kwenye droo za hiyo meza ya kuvalia hifadhi vitu vyake vya michezo na vitu vidogovidogo viwekwe humo visitupwetupwe. Kwenye droo hizo weka kwa mpangilio ili asipate shida kuona vitu. Kama kutakuwa na nafasi ya ziada pia weka kiti cha kubembea. Mabinti wanaokua wanakipenda kukalia wakati wa kusoma kitabu cha hadithi, gazeti au jarida. Kwa ajili miaka imeenda kile kizulia cha rangirangi ulichotupia juu ya lile zulia la rangi moja unaweza ukakibadilisha kwa  kumnunulia kingine. Maadam sasa ni mkubwa ataweza kuchagua rangi anazopenda ambazo zitaoana na zingine hapo chumbani.

Baada ya hapo unaweza ukaenda na bintiyo kweye maduka ya mapambo ya ndani akachagua vitu vidogodogo vya kuongezea kama taa za vivuli fremu za picha, kifungashio cha kalamu na penseli kwenye deski lake, mishumaa na kibox cha kuweka hereni na mikufu na vitu vyake vingine vya urembo. Na pia kama atapenda waweza mwekea vioo vya ukutani. Sasa kitu pekee anachohitaji kwenye lile deski ni kompyuta. Mzazi usione bintiyo anataka kutumia kompyuta yako ukamfukuza. Ni muda wake nae kuwa na yake kwake.

Kwa majumuisho, pamba kwa jinsi ambayo chumba kinakuwa na mwanga wa kutosha na sehemu kubwa ya kuhifadhi vitu ili asitupetupe vitu chini kwa madai ya kuwa hakuna nafasi ya kuweka. Mwanga wa kutosha na deski ni kwa ajili ya kujifanyia kazi zake za shuleni. Na kama unapenda binti yako ajenge tabia ya kujisomea basi usidharau umuhimu wa kumwekea shelfu la vitabu kwenye chumba chake kuweka vitabu vyake vya zamani na vipya mahali pamoja.

Hongera! Umefanikiwa kupamba chumba cha binti yako toka akiwa bebi hadi miaka 18 bila usumbufu mkubwa, muda au pesa nyingi!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk