Njia
chapchap za kupamba ndani na nje ya nyumba yako msimu huu wa sikukuu
Chochea furaha na msisimko wa kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kupamba ndani na nje ya nyumba yako. Vitu rahisi hata kama ni vijipambo vya meza tu huleta tofauti kubwa ya muonekano wa mazingira ya nyumbani.
Baadhi ya njia tofauti unazoweza
kuhuisha muonekano wa kizamani wa nyumba yako ni kama ifuatavyo:
Ongeza picha: Kuongeza picha nyumbani kwako
kunaongeza muonekano mpya mara moja kutoka ule wa zamani. Ni njia rahisi kabisa
kuhuisha sebule yako. Au unaweza kuongeza picha za familia yako ama nunua picha
za fremu kuleta muonekano wa kipekee.
Mimea na maua: Pamba mazingira ya ndani na nje ya nyumba kwa maua na mimea. Vesi
ya maua au mmea uliooteshwa kwenye chungu kwenye kona ya mahali ndani mwako vinaleta
mvuto.
Badili pazia: Hizo pazia za kila siku zinafanya
nyumba isionekane tofauti au na mvuto kwa ajili ndio hizo hizo kila siku.
Hakuna kitu kinacholeta tofauti kubwa kwenye muonekano wa nyumba kama pazia.
Weka mapazia ya aina, mitindo na vitambaa na mishono mbalimbali.
Rangi: Kupaka rangi ni njia iliyozoeleka zaidi wakati
wa kusheherekea. Zimua kuta za mazingira ya nyumbani kwako japo kwa kuongeza
koti moja tu ya rangi. Kama labda kupaka rangi chumba kizima ni gharama na kazi
kubwa basi paka hata mlango tu.
Weka mito mipya: Badilisha mito ya sebuleni kwako
na uweke ya rangi mbalimbali. Mito yenye rangi kali zilizokolea kwenye sofa
zako au hata ile mikubwa ya kukalia sakafuni inabadilisha muonekano wa ndani ya
nyumba bila ya kutumia gharama au kazi kubwa.
Panga vitu upya: Sio cha zaidi bali tu ni kuhamisha
tuseme fenicha moja toka eneo moja hadi lingine. Kufanya hivyo utashangaa jinsi
itakavyohuisha muonekano wa mahali.
Pamba eneo la lango kuu: Kinachoonekana kwanza kinamkaa mtu
moyoni daima kwa hiyo unaweza ukahuisha muonekano wa kuingialia nyumbani kwa
kupamba eneo la kuingilia. Kwa mfano vyungu vya maua vya chini au vya kuning’inia
lango kuu vitaleta mvuto wa kipekee.
Boresha fenicha: Paka rangi fenicha ya zamani au
hata ibadili kuongeza matumizi yake. Hii haitaleta tu muonekano mpya bali pia
itaongeza thamani na matumizi ya fenicha hiyo.
Weka virembo vidogodogo: Katika nyumba nyingi utakuta kuna
sehemu ambazo unaweza kuweka virembo vidogodogo kama vile juu ya kabati au
shelfu na kadhalika. Kutumia nafasi hizi kuweka marembo kutaleta mvuto ndani ya
nyumba na kuongeza uzuri wa kutazama na kushangaa.
Mapambo ya msimu: Vitu vya wakati husika vyenye mvuto vinaweza kuwekwa kama mapambo
nyumbani bila hata kutoa jasho. Kwa mfano unaweza weka matunda au maua ya msimu
kwenye bakuli la kuvutia, au vesi na kuweka mezani na ikavutia sana.
Pia unaweza kuzungushia taa
zisizo na gharama za msimu wa sikukuu kwenye miti ya bustanini au eneo la lango
kuu au hata eneo la ngazi wakati wa sikukuu na kuleta muonekano wa maajabu.
Kama tujuavyo sikukuu za mwisho wa mwaka zinazokuja ni krismasi na
mwaka mpya hivyo usisahau kupamba kwa mti wa krismasi! Mti huu umekuwa ni pambo
la kipekee kwenye nyumba nyingi duniani na hata maeneo ya jumuiya na ofisi nyingi
kila mwaka kwenye sikukuu ya krismasi.
Kama
unataka kuongeza viungo vya mapambo kwenye nyumba yako yenye muonekano wa siku zote
wala huhitaji kutumia gharama kubwa. Mabadiliko kidogo lakini yeye mashiko yatafanya
nyumba yako kuonekana upya. Kutembea kwenye nyumba inayoonekana tofauti wakati
wa sikukuu kiukweli kutahuisha na kuongeza msisimko wa sikukuu. Hutakiwi kuwa
mtaalamu wa mapambo ya nyumbani ili kuleta mabadiliko haya. Kinachotakiwa tu ni
kuwa mbunifu wa kufikiri. Jinsi ya kushehereke sikukuu ni kupamba nje na ndani
ya nyumba kwa vitupio murua. Kutegemeana na ladha yako unaweza kupamba kwa
rangi zilizozoeleka kwa sikukuu za mwisho wa mwaka ambazo ni nyekundu, nyeupe na kijani.
Mawazo ya upambaji ni lukuki, kutegemea na bajeti, ladha binafsi na mazingira
ya makazi yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni tuwasiliane viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.
No comments:
Post a Comment