Wednesday, December 19, 2012

My article for newspaper: Chumba cha kulia chakula wakati wa sikukuu


Wakati wa sikukuu ni wa kula na kunywa; weka chumba cha chakula tayari.

Chumba cha kulia chakula ni mahali ambapo familia hukutana na kula chakula huku wakishirikishana kila mmoja juu ya mwenendo wa siku yake ulivyokuwa. Sikukuu kadhaa zikiwa njiani zaja wengi wetu tunajua kuwa ni wakati wa kufurahi na jamaa zetu kwa kula na kunywa.

Kimsingi, wakati wa sikukuu unapaswa kuwa ni wa kusheherekea na kujumuika kwa wakati maalum na wapendwa wetu. Lakini kutokana na orodha ndefu ya mambo ya kufanya, zawadi za kununua, wageni wa kukarimiwa, mipango ya safari, wakati wa sikukuu kweli unaweza kuzalisha msongo wa mawazo. Kwa hiyo iwe unaalika familia kadhaa  pamoja au unapamba chumba chako cha kulia chakula kwa ajili ya watu wawili, makala hii itakupa dondoo chache za jinsi ya kufanya sikukuu yako iwe njema.

Kwanza panga mapema, usisubiri hadi dakika ya mwisho. Lakini ni nani asiyekaa hadi dakika ya mwisho na kuanza kuweka mipango siku hizi? Hata hivyo ni wazo zuri kuanza kuangalia kwenye stoo yako ni nini unacho na ni nini bado kinafanya kazi toka mwaka jana. Halafu tayarisha orodha ya nini unahitaji ili utakapoenda madukani kununua unajua moja kwa moja mahitaji yako.

Tafuta nafasi kwenye chumba chako cha kulia chakula kwa ajili ya mapambo. Kwa mfano ongeza ladha ya sikukuu kwa kufunga utepe wa rangi za sikukuu nyuma ya viti vya meza ya chakula. Usijaze mapambo ya sikukuu kwenye kila kitu kilicho chumba cha kulia chakula, na wala usitoe vifaa vyako vingine unavyotumia kila siku kwa ajili ya mapambo ya sikukuu. Ila badilisha muonekano wa kila siku kwenda kwenye wa kisikukuu sikukuu kwa mfano ondoa picha za kila siku na badala yake pamba kwa picha za msimu wa sikukuu. Kumbuka kutengeneza sehemu ya kati ya mapambo yako. Usisambaze mapambo kila eneo la chumba.

Sehemu ya kati ya mapambo ni ile inayoonekana zaidi kwa mfano kwenye chumba cha chakula sehemu hiyo itakuwa ni meza ya chakula. Meza ya chakula ndio fenicha kuu kwenye chumba cha kulia chakula. Inachukua nafasi kubwa zaidi na ndio inayotoa picha kamili ya muonekano wa chumba chote. Pamba meza hii wakati wa mlo wa sikukuu kwa vitu vya msingi kama kitambaa cha meza, napkini na bakuli la matunda.  Tupia kitambaa cha kupitia eneo la kati tu kisichofunika meza yote ili kuweza kuacha uzuri wa meza uonekane. Meza iliyopambwa vizuri ni msingi wa mlo wenye kumbukumbu.

Kosa moja kubwa ambalo watu wengi wanafanya ni kuremba mno pambo la kati la kwenye meza. Pambo hili kwa makosa linafanywa kuwa kubwa sana kiasi kuwa wageni wa upande mmoja wa meza hawaonani na wale wa upande wa pili hivyo linawagawa pande mbili na hivyo kupelekea kugawa mazungumzo ya wageni wako. Weka pambo la kati lililo dogo. Kitambaa cha meza kisaidie kuelekeza macho kwenye pambo la kati na sio kishindane na  pambo hilo kwa hivyo weka kitambaa kisicho na mbwembwe nyingi.  Angalia usipoteze nguvu nyingi kwenye kupamba na ukashindwa kufurahia sikukuu.

Meza za chakula kwa matumizi ya nyumbani ziko kwa ukubwa na maumbo tofauti tofauti kuendana na idadi ya watu kwa mfano zipo za watu wanne na hadi hata watu kumi na mbili. Meza hizi hasa zile za mbao ngumu zinauzwa gharama kubwa kwa hivyo kabla hujanya manunuzi hakikisha unanunua itakayokidhi mahitaji yako.
Kwa ujumla chumba cha kula chakula kilichokamilika kwa uchache kinatakiwa kiwe na fenicha ambazo ni meza, viti na kabati la pembeni. Kuendana na ukubwa wa chumba fenicha hizi zinaweza kuzidi lakini zisipungue. Kazi ya kabati la pembeni ni kuhifadhia vyombo vya ziada, vitambaa vya meza na pia juu yake panatumika kama sehemu ya kuwekea mabakuli ya vyakula na/au kuwekea  mapambo na mishumaa. Kioo cha ukutani juu ya kabati hili kitasaidia kuakisi mwanga na kuonyesha kama eneo ni kubwa kuliko kiukweli lilivyo.

Taa maalumu ya kuning’inia juu ya meza ya chakula ni lazima. Taa hii iwe na ukubwa sahihi kuendana na ukubwa wa chumba na pia muonekano wake uoane na mapambo mengine yaliyopo eneo hilo.

Wakati wengi wetu tukifikiria chumba cha kulia chakula tunafikiria meza, viti, kabati na taa kuna kitu ambacho kina umuhimu sawa na hivi nacho ni pazia. Zaidi ya fenicha zote ngumu zinazojaza chumba hiki ni muhimu kuwa na vitambaa ambavyo vinaleta hali ya ulaini. Kwa hiyo kama huna utamaduni wa kuweka pazia kwenye chumba chako cha kulia chakula, inalipa kuanza kufikiria kufanya hivyo.

Ni rahisi kuchoshwa na hekaheka na shamrashamra za sikukuu, lakini usisahau sehemu muhimu sana ya sikukuu ni kuona wapendwa wako, kuwa na wakati mzuri pamoja na kuhesabu baraka zenu !!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23

Friday, December 14, 2012

My article for newspaper: Maazimio ya mwaka mpya kwa makazi yako


Mazingira ya nyumbani kwako yasaidie kufanikisha maazimio yako ya mwaka mpya

Ni wakati mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu wanapenda kufanya mabadiliko kwenye maisha yao. Je umeshafikiria mabadiliko ya mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko haya yanajulikana na wengi zaidi kama maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo. Malengo yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano kuamua kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha zaidi mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya kuwa unaenda kufanya nini wakati ujao.

Mara nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha yanafanikiwa. Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani kwako kutosaidia kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama unataka kufanya mabadiliko ndani ya maisha yako bila kuhusisha mazingira yako kufanikiwa ni hatihati. Kwa maana ya kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka 2013 kwa ajili ya makazi yako na ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana kubadili chochote. Hata matangazo kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanaonyesha uhusiano kati ya maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea maambukizi hayo.

Kanuni ya malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka ujao uwe tofauti basi unatakiwa kuweka mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji? Kwenye mazingira ya nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au vimekaa mahali ambapo havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha kutimiza malengo yako hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo angalia kwa umakini kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya kutupa. Fanya hivyo kwa nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia kufanikisha malengo yako.

Pengine lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo kwa nia ya kupungua uzito. Je mara zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa nyuma ambapo unaingilia moja kwa moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona mwanzo kinagusa zaidi akili yako, kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na jokufu, chakula na kadhalika utapata hamu ya kula hapo hapo. Tumia mlango wa mbele ambapo utaona kitu tofauti mara uingiapo ndani - kitu ambacho hakitakufikirisha kula.

Mahusiano mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya nyumbani hasa katika swala la kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni mahali patakatifu kwa wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo lako mwakani ni kuwa na wageni wengi zaidi nyumbani? Hakikisha basi mlango wa mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya kuingilia. Taa zinazomulika njia ya kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi. Pitia mlango wa mbele kama mgeni mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwakani?

Kwa wale ambao azimio lao kuu la mwaka 2013 ni kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi kwa umakini, fikiria mpangilio wa fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa chumba husika. Angalia vitu ambavyo inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano sakafu ya sebule yako ni ya marumaru na unachoka kusugua na kudeki kila siku na unakiri kuwa ni ngumu kuifanya iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo utapitisha mashine ya kunyonya mchanga mara mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo basi mwaka ujao lenga kuosha chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha wanafamilia wengine pia wanafanya hivyo.

Huenda kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya kuweza kuwa na bustani za ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau ukifungua pazia la chumba cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja kwa mwezi.
Kweli, baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini kuna mabadiliko mengi sana ambayo hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na nguvu ( na pengine kautaalamu)  kwahiyo kwa 2013 kwa nini usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa ajili ya makazi yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya nyumba yako mara moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na isismamie). Shikrikisha na wanafamilia wengine pia.

Hii inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni mawazo binafsi kuwa azimia kila anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya wanawake vilivyo na visigino vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za marumaru na mbao na kuacha alama na vile vya wanaume baadhi vina soli zinazoacha rangi sakafuni na hivyo kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.

Mwaka ujao lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila mara kama vile unategemea mgeni wa heshima!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23

Wednesday, December 5, 2012

My article for newspaper: Fanana na mazingira yako



Fanana na mazingira ya nyumbani kwako
Kila mtu anachagua ni vipi anataka mazingira ya nyumbani kwake yawe. Ingawa tunaweza tusijali kuhusu uchaguzi huo lakini mazingira yetu ni dili kubwa kutuhusu. Una nafasi ya kutengeneza mazingira ambayo yatarahisisha maisha yako ama yatayafanya  yazidi kuwa magumu.

Kuna kanuni ya kwanza ya msingi kuwa katika kila kitu kilichopo kwenye eneo linalokuzunguka kina nguvu fulani iwe kitu hicho kina uhai ama hakina. Ni kama watu wa kale walivyoamini kuwa kila kitu kina uhai. Kanuni ya pili ni kuwa kila kitu kwenye mazingira yetu kinahusiana na kitu kingine. Inawezekana kwa mtizamo wa kiroho au wa kisayansi. Na kanuni ya tatu ni kuwa kila kitu kinabadilika kila wakati.

Sasa basi kama kila kitu kwenye mazingira yako kina uhai na kimeunganishwa na wewe basi mabadiliko yakitokea kwenye eneo lako nawe unaguswa. Mazingira yako yanakugusa nawe unayaakisi. Hii ni kama usemi kuwa kila kitu kwenye mazingira yako kinaongea na wewe. Je vitu vya mazingira yako vinasema yale ambayo unapenda kusikia, je vinakusaidia kupata kile unachotaka kupata katika maisha.

Fikiria jinsi unavyoingia nyumbani kwako na kukumbuka usemi kuwa unachokutana nacho mwanzo kinakugusa zaidi . Kama unaingilia varanda iliyojaa makorokoro kila mara unapoingia nyumbani kuna uwezekano mkubwa wa kuchoka hapo hapo nje hata kabla hujafika ndani. Vilevile kama unatembea kuelekea karibia na kizuizi unaanza kujifikiria kuwa inahitaji nguvu kupita pale. Pia kama unafungua mlango wa ofisi asubuhi na kukutana na meza iliyojaa nyaraka, unaweza kujisikia kama siku yako tayari imejaa na hakuna nafasi ya kuanza kitu kipya kwa siku hiyo.

Tembelea kila chumba nyumbani kwako. Je kuna kitu kinakuambia kuwa maisha ni mazuri na yamejaa fursa? Au una picha usiyoipenda, fenicha ambayo haijakaa sawa au rangi ya ukuta ambayo inakupa ukakasi kuitazama? Kila mara unapooana vitu kama hivi, unapotembelea chumba hiki unapata ujumbe hasi. Hata kama akili yako itazoea kuona hivyo lakini dhamira itakuwa inakereka.

Mkusanyiko wa picha unaweza kuwa chanjo cha ujumbe hasi. Hakikisha ni za kumbukumbu na hisia nzuri za watu hao kwako. Zinaweza kuwa ni picha nzuri sana kwa kuonekana kwa macho lakini kama mojawapo inakukumbusha tukio au wakati wa huzuni basi iondoe.  Weka zile zinazokufanya uwe na tabasamu. Watu mara nyingi wana picha kwenye kuta zao kwa sababu tu hawana kitu kingine cha kuweka hapo na sio kwamba ni kwa kuwa wanakipenda kilichopo. Sanaa ukutani inaweza kuwa nzuri sana ila kama ukiitazama haikubariki haina faida kwako. Badala yake inakupa ujumbe hasi na kukunyonya nguvu kila unapoiona. Ni vyema kuiondoa na kuacha nafasi kwa kitu ambacho kinakupa mtizamo chanya katika maisha.

Kuchukua hatua hii mbele zaidi, fikiria ni nini unakipenda kwenye maisha. Mfano mzuri ni mtu anayetaka kuwa na uhusiano. Mara nyingi picha atakazoweka nyumbani kwake na hasa chumba cha kulala ni za akiwa singo. Chumba hicho kitakuwa na taa moja tu ya kivuli na hata kimeza cha kando kimoja. Vyote hivi vinatoa ujumbe kuwa mhusika hana mtu. Badala ya vitu vilivyopo kwenye seti kwa mfano picha yenye watu wawili, na taa mbili za vivuli vinaleta alama za mahusiano.

Mazingira ya mahali unapoishi yanahusika katika kila eneo la maisha yako. Kama unahitaji akili tulivu hakikisha kuwa mazingira yako hayakupi kinyume na matakwa yako kwa kuwa na vitu ambavyo haviko mahali pake. Pia kama unataka kuwa mbunifu zaidi angalia kama je kuna nafasi zaidi ya kuweza kuwa hivyo? Kama unahitaji miundo mbinu safi je njia ya kuendea mlangoni kwako ni wazi, safi na inakaribisha?
Unavyotembea kwenye mazingira ya nyumbani kwako angalia kila kitu kwa jicho la ziada. Ondoa kila kitu ambacho huwezi ukasimama na kushuhudia kuwa unakipenda na ni kitu ungependa kuwa nacho. Unaweza usiwe na kiti kingine cha kuweka kwenye hiyo sehemu ulipotoa kile usichokipenda, lakini kama kinakuletea tukio la huzuni badi potelea mbali kitoe tu. Kinaziba kile unachokipenda na pia hicho usichokipenda kinakuletea hisia mbaya. Kwa kuamini utapata kingine unatengeneza uwezekano. Kuwa makini na hivyo vitu vinavyoongea na wewe furaha na kuvipa nafasi ya heshima nyumbani kwako.

Katika nyakati hizi za mihangaiko mingi, ni muhimu kuwa mazingira yako hayakuongezei vikwazo kwenye dunia yako. Hii inahusu hata taarifa za habari kwenye matukio ya mauaji, ajali na mengi ya kutisha. Fuatilia ni nini kiko kwenye vyumba vya watoto. Kama mazingira ya vyumba vyao yanaongea amani, watakua wakijifunza amani.
Kwa kuwa makini na kila kitu kwenye mazingira yako unatengeneza makazi ambayo yanafanana na wewe kwa kukupa ujumbe chanya na zenye kukutia nguvu. Kuwa kitu kimoja na makazi yako unakuwa na mtizamo chanya zaidi katika maisha. Mtazamo chaya unagusa kila kitu kwenye maisha yako. Yasikilize mazingira yako.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23

Friday, November 30, 2012

shape ya hizi nail polish mmmmhh!

kweli biashara yahitaji mbinu nyingi. najiuliza hizi nail polish zinahusiana vip na makalio..

Tuesday, November 27, 2012

My article for newspaper: Mlango wa mbele

Mlango wa mbele ni kivutio cha nyumba

Mlango wa mbele wa nyumba yako ni kielelezo chako. Mlango huu zaidi ya kuleta mvuto wa nyumba pia unakuhuisha mara uingiapo nyumbani.

Mlango wa mbele ni moja ya vitu vya mwanzo watu wanavyoona kuhusu nyumba. Rangi, staili na hali yake ni sehemu kubwa ya jinsi nyumba inavyoonekana kwa nje. Mlango huu una kazi ngumu ya kufanya nje kuwe nje na ndani kuwe ndani. Unapata adha ya unyevu, jua, upepo na hata vumbi na kama umetengenezwa kwa mbao kuna uwezekano wa kusinyaa na kuvimba kuendana na hali ya hewa ya majira ya mwaka. Hali hii inafanya mlango kuwa mgumu kufunguka nyakati nyingine au kupiga kelele. Njia nzuri ya kuzuia ni kuhakikisha mlango umepakwa dawa sahihi za kuzuia hali hii kabla ya kuujengea kwenye nyumba.

Mlango wa mbele wa nyumba unaweza kuwa wa mbao, chuma ama glasi. Vyovyote uwavyo uangalizi wa mara kwa mara unahitajika ili kuufanya uonekane maridadi kila wakati. Kama mlango unapigwa na jua la moja kwa moja hakikisha unaupaka  rangi au finishi inayonyonya miale ya jua ili kufanya rangi yake idumu muda mrefu.

Kaya nyingi zimefanya mlango wa mbele kuwa rasmi kwa maana ya kwamba unatumika zaidi na wageni. Kutokana na kuwa hautumiwi mara kwa mara ni muhimu kuhakikisha kuwa unafanya kazi jinsi inavyotakiwa. Swali ni kuwa ni kwanini watu wengi hawatumii mlango wa mbele mara kwa mara? Ni kama vile mlango huu umewekwa kwa ajili ya wengine na wanafamilia hawastahili kuutumia wao wenyewe ambapo wengine hao huja na kuutumia mara chache kwa mwaka. Wakati mwingine hata marafiki na majirani wakija nyumbani, wanatumia mlango wa nyuma au wa pembeni ila sio wa mbele. Matokeo yake mlango wa mbele unakaa tu bila kutumika.

Watu wengi wanaingia ndani mwao kwa kupitia mlango wa nyuma ambao labda umeunganika na varanda iliyojazwa vitu vingi ama hata pengine umeunganika na gereji. Ule usemi wa unachokiona mwanzo kinadumu zaidi ni muhimu sana hapa. Kama unaingia ndani ya nyumba kupitia mlango wa nyuma uliojaa makorokoro na vifaa vya miradi ambayo haijakamilika au hata vifaa vya bustani moja kwa moja utajisikia kuchoka hata kabla hujafika ndani. Nyumbani kwako panatakiwa kuwa himaya yako. Jipe raha kwa kupitia mlango wa mbele, hata kama inamaanisha kuegesha gari yako kwanza halafu unazunguka mbele. Utashangaa ni vip utakavyohuisha nafsi yako!

Mlango wa mbele unasema mengi kuhusu watu wanaoishi kwenye nyumba husika. Kuna watu eneo la ndani la mlango huu linatumika kama stoo. Mlango wa mbele uliozibwa kwa ndani ni alama kuwa wenye nyumba hawataki mtu apitie mlango huo.
Kwa kawaida kitu kinachokuvutia kinakuhamasisha na hivyo kukuongezea nguvu mwilini. Kama mlango wa mbele unakuhamasisha ina maana nguvu inazalishwa. Kama huo mlango huupitii hata mara moja kwa mwezi basi hamna nguvu.

Mazingira ya mlango wa mbele kwa nje ni muhimu sana. Je ni rahisi kuuona mlango uko wapi na kuna njia nyepesi ya kuufikia? Je maua na mimea ya eneo lile imepunguzwa kuufanya mlango uonekane? Jicho linavutwa kuutazama na ni nini hasa kinachokuvutia ukitazama maeneo ya nje ya mlango wa mbele wa nyumba yako? Mlango wako huo unavutia vile ambavyo unasema unapenda katika maisha? Njia ya kueleweka kupitia mlango wa mbele, rangi za kuvutia au mapambo, ni hatua za kwanza kukuwezesha kutumia mlango huo na hivyo kujiongezea nguvu ya kusonga mbele na maisha. Weka eneo la mlango safi na huru, kwa ndani pasiwe stoo na mwisho utumie mlango huu. Kama bado unashawishika kuwa ni usumbufu kutumia mlango wa mbele kwa kila siku basi amua kuutumia japo mara moja kwa wiki. Ukiwa unajua kuwa unajiongezea nguvu kwa kutumia mlango huo.

Kwavile  imeonekana kuwa kaya nyingi hazitumii mlango wa mbele kila siku, basi ni vyema kuhakikisha na kucheki mara kwa mara kuwa mlango unafanya kazi vyema na hata eneo lake ni safi kwa ajili ya ukaribisho rasmi wa wageni. Usianze kuondoa buibui, vumbi na mavi ya mijusi kwenye mlango wako huo mbele ya mgeni wakati wa kumfungulia. Fanya hatua ya mwanzo ya mgeni anayekutembelea kuwa ya kumbukumbu. Pia hakikisha kuwa kile kizulia cha mlangoni ni kisafi.

Macho yanafurahia kuona vitu vizuri, mlango wako wa mbele ni moja ya pambo la kwanza kabisa wageni wanaloona wanapofika nyumbani. Mlango wako uvutie na uoane na mapambo yako mengine ya nje ya nyumba. Mlango huu pia unakulinda unapokuwa ndani, kwa hiyo unatakiwa kuwa imara.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023