Thursday, March 17, 2016

Hatua sahihi za kusafisha meza ya kioo

Meza ya kioo inaweza kutumika kwenye nyumba yako katika vyumba ambavyo ni pamoja na sebuleni, chumba cha chakula na hata chumba cha kulala. Wapo wanaozitumia kwenye varanda na bustanini pia.  Bila kujali ni wapi ilipo meza yako ya kioo, ni wajibu wako kuhakikisha kuwa ipo katika hali nzuri kwa kuisafisha kwa kina kila inapochafuka.

Meza safi ya kioo ni pale inapokuwa na kioo kinachong’aa bila uchafu wowote. Vifaa unavyohitaji kusafishia ni dawa ya kusafishia vioo au maji mepesi kwa maana ya yasiyo na chumvi kwani huwa chumvichumvi zinaacha alama kwenye kioo, kitambaa kikavu na gazeti.

Fuata hatua hizi za jinsi ya kusafisha meza ya kioo ili ionekane kama mpya kila wakati.

1.     Hatua ya kwanza katika kusafisha meza ya kioo ni kuondoa kila kitu juu ya meza. Viweke pembeni na ukishamakiza kusafisha utavirejesha.


2.     Tumia kitamba kikavu kufuta uchafu usiong’ang’ania kama vile chumvi na vumbi juu ya meza wakati ule mwingine ukisubiri hatua inayofuata.

3.     Loanisha kitambaa chako kwa maji ya uvuguvugu na uanze kufuta meza. Maji ya uvuguvugu ni mazuri kwa kuwa yanaondoa uchafu wote kirahisi bila kuacha alama. Epuka kutumia sabuni kwani inaacha ukunguambao unasumbua kuuondoa kwa haraka. Kama kuna ulazima kabisa wa kutumia sabuni basi hakikisha unatumia kidogo sana.

Huenda ikahitajika rudia hatua hii ya tatu mara mbili au tatu kadri ya uhitaji huku ukihakikisha unaondoa madoa yanayong’ang’ania. Kama kuna alama imeshindikana kabisa kusafishika kwa mfano kuna gundi ilimwagikia kwa bahati mbaya, tumia kiwembe chenye makali ili kuondoa doa hilo.

4.     Kausha meza kwa kitambaa.

5.     Hatua ya mwisho, ni ya kung’arisha meza yako safi kwa kutumia gazeti. Unapotumia gazeti hakikisha meza ni kavu. Gazeti linaondoa ukungu wowote na kufanya kioo kimeremete.

Ni vyema kusafisha meza yako ya kioo kwa kina angalau mara moja kwa juma kwa kufuata hatua hizo chache na rahisi. Kwenye siku nyingine za juma safisha kawaida kwa kuondoa vimiminika au vyakula vilivyomwagikia kwa kitambaa na maji.
Pia inashauriwa endapo meza ni kioo kitupu na sio zile za mbao lakini zimewekewa kioo juu, basi safisha kwa juu na kwa chini.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment