Monday, March 28, 2016

Mambo ya kuzingatia unaponunua shuka


Shuka zinachukua nafasi kubwa ya kuwa kivutio cha kitanda. Unapoamua kuzinunua kuna mambo kadhaa ya kuzingatia. Mara nyingi wanunuzi wanaangalia rangi, michoro, ukubwa na bei. Hata hivyo vitu hivi  pekee havitoshi kuthibitisha ubora wa shuka hizo unazotaka kununua.

Kuchagua kitambaa cha shuka chenye ubora wa hali ya juu ndio jambo muhimu zaidi. Kwa kuzingatia hili zifuatazo ni
dondoo kadhaa za kukuwezesha kununua shuka bora mahali popote.

Kitambaa
Katika masoko ya kisasa, iwe ni mitandaoni au madukani unaweza kukutana na aina mbalimbali za shuka kwa makundi tofauti ya malighafi zilizohusika kuzitengeneze. Malighafi zilizozoeleka ziadi kwa ajili ya kutengeneza shuka ni pamba, hariri na polista. Mguso na uzuri wa shuka unatofautiana kutokana na malighafi iliyotengenezea kitambaa cha shuka husika. Na hapa ndipo unakuta mazungumzo kati ya muuzaji na mnunuzi kuwa na maswali kama “je, shuka za pamba au za kuteleza?”. Kimsingi shuka zilizotengenezwa kwa pamba asilimia mia kwa mia zinapendwa kuliko shuka nyingine zote. Kwa hivyo hata bei ya shuka za namna hii ni kubwa.

Usukaji
Katika usukaji wa shuka tunamaanisha ule unene na uzito wa kitambaa cha shuka. Na ndio maana unakuta mnunuzi anataka kujua kama ni shuka nzito au nyepesi. Uimara na ulaini wa shuka unatokana na aina ya usukaji wake kwamba ni nyuzi kiasi gani zimetumika kwenye kila inchi ya mraba. Endapo shuka unazotaka kununua zimefungashwa katika vigezo vinavyokubalika iwe ni kitaifa na kimataifa, lazima utakuta kwenye karatasi yake ya maelezo kuna jambo hili la kiasi cha nyuzi ambapo linaandikwa ni thread count. Hesabu ya nyuzi inapokuwa kubwa ndivyo na ubora wa shuka unavyozidi. Kwa kawaida kiasi hiki cha nyuzi kinaanzia 200 hadi 1,000.

Muundo
Kuna miundo miwili mikuu ya shuka. Nayo ni shuka flati na shuka za kufitisha. Shuka flati hazina mpira uliyoizunguka zimekaa tu flati kama kanga wakati zile za kufitisha zina mipira kuzunguka shuka nzima au kwenye maeneo ya kona tu. Shuka za kufitisha zinatandikwa kuendana na ukubwa wa godoro na hizi ndio hasa za kulalia. Zinarahisisha utandikaji kwani huna haja ya kuchomekea kila wakati unapotaka kutandika kitanda maana tayari mipira yake imeshajibana kwenye godoro. Unachofanya ni kunyoosha kidogo tu mikunjo michache juu ya godoro tofauti na ambavyo ingekuwa kwa shuka za flati ambazo zinachomoka na kukimbia godoro.

Mtindo
Unaponunua shuka hakikisha mtindo wake ni kati ya mambo unayozingatia. Mtindo ni pamoja na ile michoro, mguso na rangi ya shuka. Mara unaporidhika na uimara na ulaini wa kitambaa cha shuka, ndipo unapoweza kuchagua mtindo ambao utaoana na mapambo yako mengine kwenye chumba cha kulala.

Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment