Baada
ya miaka kadhaa ya kuishi kwenye nyumba hiyo hiyo, nyumba wengi wanatamani kubadilisha mionekano
ya nyumba zao hizo. Na mara nyingi wazo linalowajia ni marekebisho ya jengo na
kubadilisha fenicha. Hata hivyo hii inamaanisha gharama kubwa na kushirikisha
wataalam wa kutekeleza jambo hilo.
Lakini
je, kwanini mwenye nyumba asifikirie kufanya mabadiliko ya gharama nafuu kama
vile badala ya kununua fenicha mpya akafanya maboresho kidogo ya zilizopo na zikaleta
mvuto kabisa.
Makala
zangu nia yake ni kukupa mawazo lukuki ambayo unaweka kutumia kuboresha maisha
ya nyumbani kwako kwa gharama nafuu. Endapo mwenye nyumba utaamua kufanya
utafiti kidogo na kufuata ushauri unaweza kufanikisha kazi yako kirahisi na kwa
gharama nafuu sana. Kwani utakuwa umeshaelewa picha nzima ya unachotakiwa
kufanya na kwa wewe kushirikiana na watendaji wachache utafanikisha lengo lako.
Matumizi
tofauti ya rangi, karatasi za ukutani, vitambaa na malighafi nyingine
zilizotengenezea fenicha zako vinaweza kubadilisha kabisa muonekano na kukupa
wa kuvutia.
Zipo
rangi za kung’aa kama polishi na zipo zisizong’aa za mati unazoweza kutumia
kuboresha fenicha zako. Kwa mfano kupaka rangi upya kabati la luninga, miguu ya kiti au meza kunabadilisha kabisa
muonekano wake. Vile vile bila kusahau kubadilisha kitambaa kilichotengenezea
viti au sofa endapo kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Dondoo
nyingine ni kubadili vitu kidogodogo kama vile tai na fimbo za pazia. Ni ukweli
kuwa vitu vya nymbani vinabadilika kila baada ya kipindi kifupi. Huenda tai
zako za pazia za miaka mitano iliyopita ni tofauti kabisa na zilizopo kwenye
mitindo sasa. Cha muhimu ni kuangalia hivi vitu vidogo visivyo vya gharama
kubwa ambavyo ukivibadili vinapendezesha nyumba yako zaidi.
Eneo
lingine ni la kwenye mito ya makochi. Kuwa na foronya mbalimbali na badilisha
mara kwa mara. Vilevile kwa upande wa bakuli la taa, balbu siku zote ni
hiyohiyo kinachobadilika ni jumba lake. Endapo utabadili jumba la taa kama vile
taa ya jikoni au chumba cha chakula na kuweka ya kisasa zaidi bila shaka
utakuwa umeboresha muoneakno kwa gharama nafuu kabisa.
Tukienda
kwa upanda wan je ya nyumba huenda ukataka kuboresha kwa kupaka rangi upya na
pia kuongeza taa za ulinzi. Unapopaka rangi zingatia kuboresha zaidi yale
maeneo yaliyomeguka meguka. Kwa mfano nimeona watu wakitengenezea mikanda
kuzunguka madirisha ambapo mwanzoni haikuwepo. Matokeo ya hii mikanda ni kufanya
nyumba kuwa ya kisasa zaidi kwa nje na vilevile kuficha zile kona zilizokuwa
zimemeguka.
Kwa
upande wa bustani huenda mwanzoni miaka ya nyuma uliweka njia ambazo sasa
huzihitaji tena kwa maana ya kwamba hazitumiki. Ni wakati wa kuziondoa na
kufanya eneo lote liwe na ukoka. Pia kuna wakati vitofali vinakuwa vimemeguka
aidha kwa sababu ya maji ya chumvi au ni kwamba tu vimekaa muda mrefu. Kutokana
na hali yake unaweza kuvipaka rangi au laa kuviondoa na kuweka sakafu ya malighafi nyingine bora zaidi
iliyopo sokoni kwa kipindi hicho. Wakati huohuo usisahau kuboresha stendi
na vyungu vyako vya maua aidha kwa
kuvipaka rangi (kazi ambayo unaweza kufanya mwenyewe) au kuotesha maua mazuri
zaidi.
Hizi
ni dondoo za maeneo kadhaa unayoweza kuangalia ili kuboresha muonekano wa
nyumba yako uwe wa kisasa zaidi na mahali pazuri pa kuishi. Na kama wewe ni
mpenzi wa vitu vizuri hii inaweza kuwa ni tabia yako kila baada ya miaka
kadhaa.
Vivi
anakuwezesha kupendezesha nyumba yako kwa gharama nafuu kabisa, atakushauri na aidha utatekeleza wewe mwenyewe au atakuunganisha na watendaji wa maeneo hayo. Kwa maelezo zaidi simu 0755200023
No comments:
Post a Comment