Tuesday, April 5, 2016

Mazingira ya makazi yako ni utambulisho wako


Kila mtu anachagua ni vipi anataka mazingira ya nyumbani kwake yawe. Ingawa tunaweza tusijali kuhusu uchaguzi huo lakini mazingira yetu ni picha kubwa kutuhusu. Una nafasi ya kutengeneza mazingira ambayo yatarahisisha maisha yako ama yatayafanya  yazidi kuwa magumu.

Kuna kanuni ya kwanza ya msingi kuwa katika kila kitu kilichopo kwenye eneo linalokuzunguka kina nguvu fulani iwe kitu hicho kina uhai ama hakina. Ni kama watu wa kale walivyoamini kuwa kila kitu kina uhai. Kanuni ya pili ni kuwa kila kitu kwenye mazingira yetu kinahusiana na kitu kingine. 

Inawezekana kwa mtizamo wa kiroho au wa kisayansi. Na kanuni ya tatu ni kuwa kila kitu kinabadilika kila wakati.
Sasa basi kama kila kitu kwenye mazingira yako kina uhai na kimeunganishwa na wewe basi mabadiliko yakitokea kwenye eneo lako nawe unaguswa. Hii ni kama usemi kuwa kila kitu kwenye mazingira yako kinaongea na wewe. Je vitu vya mazingira yako vinasema yale ambayo unapenda kusikia, je vinakusaidia kupata kile unachotaka kupata katika maisha.

Fikiria jinsi unavyoingia nyumbani na ukumbuke usemi kuwa unachokutana nacho mwanzo kinakugusa zaidi. Kama unaingilia varanda iliyojaa mithili ya stoo, kuna uwezekano wa kuchoka ukiwa nje hata kabla hujaingia ndani. 

Vilevile kama unatembea kuelekea karibia na kizuizi unaanza kujifikiria kuwa inahitaji nguvu kupita pale au labda unafungua mlango wa ofisi asubuhi na kukutana na meza iliyojaa nyaraka, unaweza kujisikia kama siku yako tayari imejaa na hakuna nafasi ya kuanza kitu kipya kwa siku hiyo.

Angalia makazi yako, je kuna kitu kinakuambia kuwa maisha ni mazuri na yamejaa fursa? Sanaa ukutani inaweza kuwa nzuri sana ila kama ukiitazama haikubariki haina faida kwako. Badala yake inakupa ujumbe hasi na kukunyonya nguvu kila unapoiona. Ni vyema kuiondoa na kuacha nafasi kwa kitu ambacho kinakupa mtizamo chanya katika maisha.

Mazingira ya mahali unapoishi yanahusika katika kila eneo la maisha yako. Kama unahitaji akili tulivu hakikisha kuwa mazingira yako hayakupi kinyume na matakwa yako kwa kuwa na vitu ambavyo haviko mahali pake. Pia kama unataka kuwa mbunifu zaidi angalia kama je kuna nafasi zaidi ya kuweza kuwa hivyo?

Unavyotembea kwenye mazingira ya makazi yako angalia kila kitu kwa jicho la ziada. Ondoa kila kitu ambacho huwezi ukasimama na kushuhudia kuwa unakipenda na ni kitu ungependa kuwa nacho. Unaweza usiwe na kiti kingine cha kuweka kwenye hiyo sehemu ulipotoa kile usichokipenda, lakini kama kinakuletea tukio la huzuni basi potelea mbali kitoe tu. Kinaziba kile unachokipenda na pia hicho usichokipenda kinakuletea hisia mbaya. 

Kwa kuamini utapata kingine unatengeneza uwezekano. Kuwa makini na hivyo vitu vinavyoongea na wewe furaha na kuvipa nafasi ya heshima nyumbani kwako.

Katika nyakati hizi za mihangaiko mingi, ni muhimu kuwa mazingira yako hayakuongezei vikwazo kwenye dunia yako.

Kwa kuwa makini na kila kitu kwenye mazingira yako unatengeneza makazi ambayo yanafanana na wewe kwa kukupa ujumbe chanya zenye kukutia nguvu. Kuwa kitu kimoja na makazi yako unakuwa na mtizamo chanya zaidi katika maisha.


Endapo unahitaji ushauri wowote wa kuhusu mapambo na mpangilio nyumbani usisite kuwasiliana na mimi. Elimu haina mwisho...simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment