Tuesday, April 12, 2016

Njia 7 za kuweka mpangilio kwenye makabati ya jikoni


Je unaishi kwa hofu ya kitu kukudondokea kichwani pale unapofungua makabati ya jikoni? Au labda unajikuta ukitoa karibia nusu ya vitu kabatini ili kupata kile kitu kimoja unachokihitaji? Kupata suluhisho la kadhia hii fuatana nami katika njia hizi 7 nilizokuandalia za kuweza kuweka mpangilio kwenye makabati ya jikoni kwako.

Ni vyema kwanza tufahamu kwamba ili kuweza kuweka mpangilio mahali unahitaji ongezeko la
eneo la kuhifadhia. Na ongezeko hili linaweza kuwepo popote pale unapoongeza vitu rahisi kabisa vya kuhifadhia. Kwa upande wa jikoni ni kwamba kwenye maduka ya vyombo kuna vitu vingi  vya kukuwezesha kuweka mpangilio kwenye makabati ya jikoni. Vitu hivyo ni  kama vile, raki, vikontena, vitenga na vikasha au wengine wanaita vikapu, vyote hivi vikiwa vimetengenezwa kwa maumbo madogo ya kuweza kufiti vizuti kwenye makabati ya jikoni. Endelea kusoma uone vile unavyohitaji.

1.      Vitenga na vikasha
Vitumie kuweka vikontena vidogodpogo ambavyo badala yake vinaweza kusababisha mrundikano kabatini. Vitu unavyoweza kuhifadhi kwenye vitenga na vikasha ni vikontena au chupa za viungo au  sabuni na dawa za kusafishia.

2.      Vyumba katika droo
Kimsingi chumba cha droo ni kikubwa kwa kuweka vijiko pekee kwa mfano. Badala ya kweka droo moja vijiko tu, na la pili uma tu na la tatu visu tu na kuendelea, kiukweli kwa kupangilia hivi ni matumizi mabaya ya nafasi katika droo zako. Pia kuchanganya visu, uma na vijiko kwenye chumba kimoja cha droo ni kukaribisha mrundikano na uwezekano wa kisu kumkata mtafutaji. Njia sahihi ni kuweka vyumba vidogo kwenye chumba kikubwa cha droo na ndipo unapoweza kupanga kila kifaa kwenye kichumba chake kidogo na hatimaye ukabakiwa na droo nyingine kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vingine kama vile vitaulo eproni, vitambaa vya meza na vinginevyo.

3.      Raki
Raki zinaweza kutumika kwa manufaa sana ndani ya makabati ya jikoni ambapo unaweza kuwa nazo za miundo mbalimbali kwa ajili ya kusimamisha vitu kama sahani, mifuniko ya sufuria, chupa za mvinyo, mbao za kukatia na hata chupa za viungo.

4.      Mbao za kutenganisha
Hizi ni mfano wa nyumba ya ghorofa. Unapopanga vitu kama vikombe na glasi kwenye kabati kuna eneo kubwa tu linabaki wazi juu ya vyombo hivyo humo humo ndani ya kabati. Cha kufanya ni kuweka bodi juu yake ambapo unaweza kupanga seti nyingine tena ya glasi au vikombe.

5.      Kubebanisha
Vyombo kama mabakuli, sufuria na vikaangio vilivyo kwenye muundo wa kufanana lakini ukubwa tofauti vinawezekana kubebanishwa ili kuweka mpangilio na kuhifadhi eneo. Na ili kuondoa mikwaruzano weka karatasi kati ya chombo kimoja na kingine.

6.      Jinsi vinavyotumika
Glasi, sahani za kulia na mabakuli ya kujaza vyakula vinaweza kupangwa kwa makundi kutokana na kazi ya kila moja. Kwa mfano glasi za kutumila kila siku zipange kwenye kundi moja na zile za wakati maalum kwenye kundi jingine. Pia unaweka kupanga kwa muundo wa glasi za juisi na maji pamoja, za mvinyo pamoja na za pombe nazo kundi lake. Vivyohivyo kwa hili kundi lingine la sahani na mabakuli.

7.      Jagi la vijiko na miiko
Weka vifaa vya kupondaponda na kukoroga chakula wakati wa kupika katika kundi moja. Unaweza unavisimamisha kwenye jagi ambalo pia linajulikana kama utensil jar na kuliweka karibia na pale unaposimama wakati wa kupika ili iwe rahisi kuchukua kutumia.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023 

No comments:

Post a Comment