Wednesday, June 12, 2013

My article for newspaper: njia za kuhifadhi taulo




Unavyoweza kuhifadhi taulo zako za bafuni

Ni bafu chache zenye sehemu ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi taulo. Lakini usijali kwani hata kama bafu lako ni dogo namna gani njia mojawapo kati ya hizi itakufaa kutundika ama kuhifadhi taulo zako.

Kuweka fimbo za kutundika taulo kwenye ukuta wa bafu ama nyuma ya mlango (uwe wa mbao kwa uimara) ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi taulo zako. Fimbo za kutundikia taulo hazichukui nafasi kubwa na wala hazina marembo kwa hivyo ni suluhisho tosha kuhifadhi taulo zako kavu na hata zile zenye unyevu. Fimbo za taulo zinaruhusu taulo kukauka kwa usafi zikiwa zimetundikwa kwa kukunjwa nusu. Fimbo za bafuni za kuwekea taulo zinasaidia mambo makubwa mawili: kwanza, zinaweka taulo kavu na safi kwa jinsi ambayo ni rahisi kuchukua na kutumia; pili, zinatandazwa taulo zenye unyevu na kuzifanya kukauka rahisi, kwa hivyo kuzuia kuota kwa ukungu. Licha ya kufungwa bafuni fimbo za taulo zinaweza kufungwa pia jikoni kwa ajili ya kuwekea taulo za mkononi.

Muonekano wa fimbo za taulo ni kawaida sana. Ni fimbo iliyowekwa ukutani ama nyuma ya mlango kwa kutumia mashine ya kutobolea ukuta na taulo huwekwa hapo, hutolewa kutumika na hurudishwa tena hapo baada ya kutumika kwa ajili ya kukauka. Ni muhimu fimbo hizi ziwe zimeweka imara  kwa kuwa kama tujuavyo taulo zikiwa mbichi zinakuwa nzito na pia mara nyingine fimbo hizi hutumika na watoto (wakati mwingine ni kwa utundu wao wa kupenda kubembea kila waonapo panafaa) ama wazee kujishikilia wakiwa bafuni. Kwa hivyo siwezi kuacha kusisitiza kuwa fimbo za taulo ni lazima zifungwe kwenye ukuta wa tofali ama mlango wa mbao kwa ajili ya uimara.

Fimbo za kuwekea taulo zinapatikana kwenye maduka ya fenicha za nyumbani na zimetengenezwa kwa chuma. Saizi ambazo ziko kwa wingi ni inchi 18 kwa ajili ya taulo za mkononi na inchi 24 kwa ajili ya taulo za kuogea. Hakikisha umeshatathmini bafu lako na kuamua ni wapi pa kuchimbia fimbo ya taulo na uone pana nafasi ya kutosha urefu wa fimbo zilizopo sokoni.

Fimbo za taulo sizo tu zinazoweza kuhifadhi taulo kwa usafi na kuruhusu zile zenye unyevu kukauka. Kulabu (hook) za taulo, susu (rack) za kusimama wima, bangili na ngazi za taulo nazo ni njia nyingine za kuhifadhi taulo za bafuni. Bangili iliyotobolewa ukutani ambapo taulo kadhaa zinatundikwa ni maarufu sana siku hizi na kwenye maduka ya fenicha wanaziita bangili za taulo. Chuma kingine kinachoonekana kama ngazi ndogo ambacho hutumika kuwekea taulo nacho ni njia mojawapo ya kuhifadhi taulo za bafuni. Je una nafasi kwenye ukuta wa chumba chako cha kulala ambapo unaweza kuweka ngazi hii? Ni kiasi cha kuishikilia na braketi juu ili isianguke na unaweza kuhifadhi kwa kutandaza taulo zako za kuogea. Uzuri wa ngazi ya taulo ukilinganisha na fimbo ni kuwa wakati kwenye fimbo unaweza kuweka taulo zisizozidi 2 kwenye ngazi ya taulo unaweza kuweka hadi taulo 6.

Lakini kuna njia nyingine ambazo hazitakufanya uusumbue ukuta wako ambazo zinaonekana za kimapambo zaidi kwa mfano kuweka susu ya kusimama inayojitegemea kama ile ya kutundika makoti ofsini. Kama chumba chako cha kulala kina nafasi kidogo ya ziada basi simamaisha susu ya koti kwa ajili ya kutundikia taulo za bafuni. Susu inaweza kutundikwa taulo kadhaa kwa wakati mmoja. Fikiria kuiweka sehemu ambayo inaingiza hewa au vinginevyo uwe unazigeuza mara kadhaa kuwezesha kukauka. Kama susu hii inatundika taulo za wanafamilia tofauti basi wawe na taulo za rangi tofauti kwa kila mmoja. Hakuna anayependa kushirikiana taulo.

Badala ya ile susu ya kusimama kuna hii nyingine inayofanana na ya kuhifadhia chupa za mvinyo. Baadhi ya watu hawafikirii kutumia taulo za bafuni zaidi ya mara moja kabla hawajaziweka kwenye kapu la nguo chafu ili kufuliwa. Nenda kistaili zaidi kwa kuhifadhi taulo zako safi zilizobiringishwa vizuri kwenye susu ya taulo. Susu za taulo zina muonekano wa kuvutia kwa hivyo kwa upande mwingine ni kama pambo. Taulo safi zinabakia zimebiringishwa vizuri ndani ya susu hadi wakati wa kutumiwa, na hii inachukua nafasi kidogo kuliko ile susu ya kusimama. Kuhifadhi taulo kwa kutumia susu ya taulo inakubidi uwe ni mtu wa kutumia taulo mara moja tu na kulifua.

Kwa hivyo kama ulijisikia kwamba bafu lako ni dogo kiasi kwamba huna mahali pa kuhifadhi taulo zako hatimaye leo umefahamu njia kadhaa za kuweza kuhifadhi na kutunza taulo zako wakati huohuo ukiwa unazitumia. Wekeza katika njia mojawapo kati ya hizi ili kurahisisha maisha bafuni.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment