Chini
ya mwezi mmoja ujao tutakuwa na sikukuu ya Krismasi na baadhi ya sehemu hasa
kwenye maduka makubwa tayari wameshaweka mapambo ya krismasi ambayo ni pamoja
na mti, taa za kumeremeta na kadi.
Lakini
je, ni wakati gani unaweka mapambo yako ya Krismasi nyumbani? Na pia je, ni
wakati gani unayaondoa? Je, unayaweka wiki kadhaa kabla au unasubiri siku
chache tu kabla ya sikukuu? Au labda
hupambi kabisa, huenda yanawaletea watoto
ugomvi na wanakimbilia kuyanyofoanyofoa!
Nimefanya
mahojiano na baadhi ya wakazi wa jiji la Dar kuhusu swala hili la ni muda gani
muafaka wa kuweka na kutoa mapambo ya krismasi na hapa ni majibu niliyopata.
Yasome uyatathmini wewe maono yako je yanaendana na baadhi ya hawa?
“
Mti wangu wa krismasi na mapambo yake nauweka kuanzia tarehe 1 Desemba kila mwaka.
Watu hawatakiwi kuamini eti mambo ya bahati mbaya kwamba unaweza kufa kabla ya kuiona
sikukuu, ni upuuzi”, anasema Sara kutoka Bonyokwa.
“
Nadhani mapambo ya krismasi yanatakiwa kuanza Desemba 1, yaanze na sherehe za
msimu wa sikukuu, na yaondolewe Januari 3 baada ya kuuona mwaka mpya”, anasema
Monica wa Gongo la Mboto.
“
Yanatakiwa yawekwe siku 12 kabla Yesu hajazaliwa. Hata hivyo ndio sababu ya
mapambo haya”, anasema Robert wa Kinyelezi.
“Nadhani
mapambo ya Krismasi yanatakiwa yawekwe toka Novemba, ambapo ni vizuri kwani
yananyanyua mioyo ya watu ndipo wanaanza kujitayarisha!”, anasema Shana wa Mbuyuni.
“Nyumbani
kwangu, huwa tuna kawaida ya kuweka mapambo ya Krismasi toka mwezi wa tisa
lakini pia ni wazo zuri kuyaweka kuanzia
Desemba 1 kwasababu ndio mwanzo wa sikukuu ya Krismasi”, anasema mama mchungaji
Anna wa Mzambarauni.
“Mimi
ni Muislam kwahivyo sisheherekei Krismasi. Lakini bado nawapa watu kadi na
zawadi kwasababu ni msimu wa sikukuu” , anasema Asia wa Kitunda.
“Nadhani
mapambo yenu ya Krismasi myaweke Desemba, lakini baadhi ya watu na maduka
wanaweka toka Novemba. Inasikitishaje? Anasema Dominic wa Vingunguti.
“Nadhani
mapambo ya Krismasi yaanze kuwekwa Desemba 1 na yaondolewe mara baada ya mwaka
mpya, anasema Elli wa Tabata.
“Nadhani
kuanza kuweka mapambo ya Krismasi Novemba ni mapema sana. Ya kwangu nayaweka Desemba
1, lakini baadhi ya marafiki zangu wanasubiri hadi siku ya mkesha wa Krismasi
ndio wanaweka. Mimi siwezi kusubiri hivyo! Sijui ninachopendelea zaidi kwenye
mapambo haya ila kikubwa ni furaha tu kuwa sikukuu iko njiani”, anasema Lizi wa
Karakata.
“Yanatakiwa
yawekwe tarehe 1 Desemba ili yaanze na kipindi cha majilio”, anasema Anna wa
Banana.
“Familia
yetu inajali sana kipindi cha Krismasi. Tumeshaweka mapambo yetu yote tayari,
na kipindi hiki baba amenunua taa nyingi za vimulimuli kwa ajili ya kuzungushia
nje. Nyumba yetu inaenda kupendeza sana!”, anasema Stela wa Segerea.
“Krismasi
sio kuhusu mapambo wala santa klausi, ni kuhusu Kristo. Sisi hatujali kuweka
miti wala mapambo”, anasema Tom wa Mbuyuni.
“
Sisi hatuweki mapambo yetu hadi baada ya
siku ya kuzaliwa ya babu ambayo ni Desemba 15. Wote wanakuja na tunasheherekea
pamoja Krismasi”, anasema Jesca wa Kitunda.
“Nadhani
watu wanatakiwa kuwa na mapambo yanayohusu utamaduni wao kwasababu Krismasi ni
kuhusu kuzaliwa mkombozi na sio Santa. Watu wanayapaisha mapambo na kufikiria
tu zawadi na sherehe; inatakiwa kusherekea kuzaliwa Kristo. Kwahivyo weka mti
wiki moja kabla ya Krismasi”, anasema Bella wa Bonyokwa.
“
Sisi tumeweka yetu leo! Najua ni mapema kidogo lakini kwa maduka yaliyoko
kwenye jengo hili sisi ndio wa mwisho! Wenzetu wote wameshaweka” , anasema
Bertha wa Segerea
“Mimi
sisheherekei Krismasi, lakini nadhani hao wanaosheherekea inawapasa kujiandaa
mapema iwezekanavyo ili kuwa na muda na nguvu za kutosha” anasem Ndita wa
Makoka.
“Huwa
tunaweka mapambo yetu kwenye tarehe 12 Desemba. Sioni ni kwanini maduka mengi
makubwa yanaaza kuweka toka Oktoba hadi mapema Novemba”, anasema Margareti wa
Mbuyuni.
“Mti
wetu wa mwaka jana ndio tumeutoa stoo jana tumeanza kuunganisha na tutaupamba
leo!”, anasema Lucy wa Kipawa.
Msomaji
wangu umeona mawazo mbalimbali kuhusu wakati muafaka wa kuweka na kuondoa
mapambo ya Krismasi. Tukutane hapahapa wiki ijayo.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi.
Je, unauza
bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue?
Nijulishe simu/whatsapp 0755200023
www.vivimachange.blogspot.com
Mi hata sijui nashangaa nikirudi nyumbani kuna mapambo, baada ya krismas hivyo hivyo nashangaa hakuna mapambo.
ReplyDeleteSafi sana Matola, yaonekana una ubavu mzuri anayetunza nyumba vyema
Delete