Jinsi ya
kusafisha vifaa vya kufanyia usafi
Hatusafishi
vifaa vyetu vya kusafishia sio? Hata ukikataa, kubali tuu kuwa wengi
hawasafishi. Wengi tunajua umuhimu wa kusafisha na kutunza vitu….ila vifaa
vyetu vya kusafishia mara nyingi vinasahaulika. Haijalishi wewe ni msafi kiasi
gani, haiwezekani kuweka nyumba safi kama vifaa vyako vya kusafishia
havisafishwi! Makazi ya vijidudu vingi ni kwenye maeneo machafu. Angamiza
vijidudu kwa kusafisha sponji na vifaa vyako vingine vya kusafishia!
Kwa
sababu tu kinatumika kusafishia sio kuwa kinajisafisha chenyewe. Kiukweli vifaa
vya kusafishia vinaweza kuwa makao ya uchafu, vijidudu, tope na harufu kama
havitunzwi vizuri. Jinsi vifaa vinavyotunzwa ndivyo hela yako ya kununua vipya
itakavyobaki mfukoni. Ufagio mchafu unachafua zaidi sakafu na pia uchafu huo
unaweza kukwaruza sakafu yako. Mashine ya kusafishia kwa upepo ambayo haijasafishwa
haifanyi kazi yake vizuri. Weka vifaa vyako katika hali ya usafi ili kuwa na
matokeo mazuri.
Kuna ule usafi wa kawaida wa kusafisha vifaa vya kusafishia japo kwa sabuni
na maji na kuviacha vikiwa safi tayari kwa kuanza usafi mwingine. Brashi za
kusafishia bafuni zishafishwe kwa dawa za kuua vijidudu japo mara moja kwa
mwezi. Brashi za kusugulia zaweza kusafishwa kwa maji na sabuni ya kawaida. Brashi
zenye taka zilizojishikilia waweza kuchukua kijiti na kuondoa taratibu taka
zote ziwe ni tope au nyuzi nyuzi.
Ndoo
zako za kupigia deki usiziache zikiwa na uchafu wa aina yoyote hata kama ni
maji yaliyotumika tayari. Ziache zikiwa kavu aidha kwa kuzigeuza juu chini.
Sponji
la kuoshea vyombo uwe unaliosha kwa maji ya moto walau kila juma. Ikiwezekana
hata kulichemsha jikoni itakubwa bora zaidi, wengine wanaenda hatua ya mbali
zaidi ya kuliweka kwenye kipasha vyakula (microwave).
Ila kama utafanya hivi hakikisha sponji
limeloa chepechepe kabla ya kuliweka kwenye microwave.
“Asimilia 70 ya bacteria huishi kwenye sponji chafu”, anasema dokta Mbuya.
Tokea
ukiwa mdogo, kulikuwa na kitambaa cha kufutia vumbi nyumbani. Ukichukua kitabu
chenye vumbi unachukua kitambaa unakifuta. Vitambaa hivi vya kufutia vyumbi
ambavyo wengi wetu wanaviita dasta
vinapaswa kufuliwa kiumakini kama tunavyofungua nguo nyingine. Tofautisha kati
ya vile vyenye uchafu mkubwa wa kudiriki kutengeneza utando na vile vyenye
uchafu mwepesi.
Vichwa
vya mop na madekio mengine vinapaswa
kusuuzwa baada ya kufanyika usafi na kuachwa vikauke. Kabla ya kusuuza
hakikisha kuwa unaondoa udongo wote, mchanga na hata majani yanayoweza kuwa
yamejishikilia ndani. Sio sawa baadhi walivyozoea kuacha dekio linakanyagiwa
mlangoni. Pale ni sehemu ya kuweka tandiko la mlangoni na sio dekio. Sabuni ya
kawaida ya kufulia inatosha, huhitaji kuweka dawa za kusafishia kwenye vifaa
hivi. Ila ni muhimu vikuke kwani vinaweza kutoa harufu ya uvundo.
Kusafisha
mifagio..mmh ni wachache wanaofikiria kufanya hivyo! Unaweza kufungua ile
sehemu ya brashi ukaitenganisha na fimbo na ukaiweka kwenye ndoo ukasafisha na
brashi zako nyingine za kusafishia. Jambo la kuzingatia ni kuondoa matope
kwanza kwa kuwa sehemu ya ufagio ya brashi ni maarufu kwa tope na uchafu
uliojizunguishia kwenye vibrashi vyake.
Mashine
za kusafishia kwa upepo zinatofautiana kiumuundo ila kuna dondoo kadhaa za
kukuwezesha kuisafisha. Tafuta kama una kitabu ulichonunulia kitakuongoza jinsi
ya kuisafisha. Hakikisha unamwaga mfuko wa kukusanya vumbi mara kwa mara. Kutegemea
na jinsi unavyotumia mashine yako fua mfuko wa vumbi kila baada ya miezi
mitatu. Uanike ili ukauke kabisa kwani ukiiurudisha ukiwa na unyevu
utasababisha vumbi kufanya tope na hivyo kuiharibu mota kwa kuilazimisha ifanye
kazi kubwa ya kusukuma kushindana na ukuta wa tope. Kama unasikia harufu ya
vumbi inatoka ndani ya mashine yako ni kwa kuwa mfuko wa vumbi umejaa.
Ingawa hutumii mashine yako ya kufulia kwa kitu kingine zaidi ya nguo bado kuna wakati inakubidi ufungulie maji kuisafisha yenyewe bila kuweka nguo ndani.
Tumejuzana
namna ya kusafisha vifaa vya usafi ambavyo tunatumia mara kwa mara nyumbani.
Inaweza kuwa shughuli sahihi ya kufanya kwa muda wowote wa ziada ulio nao weekend hii!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment