Thursday, July 4, 2013

My article for newspaper: Doormats



Uchaguzi na matumizi ya tandiko la mlangoni

Kwa nyumba nyingi wakati mgeni wako akifika mbele ya nyumba yako, kitu cha kwanza anachokutana nacho ni mlango uliofungwa na tandiko la mlangoni. Ingawa tandiko za mlangoni zina kazi ya kufutia miguu pia kuna njia mbalimbali ya kuzifanya ziwe ni kama mapambo ya kwenye nyumba.

Uchafu na unyevu  unaobebwa kwenye nyayo toka nje ya nyumba unaweza kuharibu sakafu na pia unachafua, na hii inamaanisha kutakuwa na hitaji la kufagia, kusafisha kwa mashine ya upepo au kudeki mara nyingi zaidi ya ambavyo ingekupasa.  Tandiko za mlangoni ambazo ni  jamvi kama ni nje ya nyumba ama kizulia kwa eneo la ndani ya nyumba; ingawaje watu wamekuwa wakizidharau ni njia yako ya mwanzo kabisa ya kuzuia uchafu, mchanga na udongo visiingie ndani. Tandiko hizi si za gharama kubwa na mara nyingine wala hazihitaji mvuto kwa hao wanaozitumia.

Weka tandiko za mlangoni kwenye sehemu zote za kuingilia na hasa zile zinazotumika zaidi. Kuendana na hali yako ya kuishi unaweza kuwa na milango ya pembeni na ya nyuma zaidi ya ule wa mbele. Hakikisha kuwa yote ina tandiko za mlangoni. Pia kwenye sehemu ambazo hazijamaliziwa kwa mfano kwenye banda la gari ambalo lina mlango mdogo wa kuingilia ndani hakikisha napo unaweka jamvi mlangoni.

Tandiko za kukanyagia kwenye milango ya nje yaani jamvi chagua ambazo zina matobomatobo au zenye nyuzi zilizo kama brashi. Jamvi zinaweza zisionekane kuwa na mvuto lakini ni madhubuti kwa kufutia viatu na zinadumu muda mrefu, zinafanya kazi nzuri sana kama tandiko za milango wa nje. Zitumie nyumbani kwa eneo lenye matope na kwenye banda la gari au kwa mlango wa nje wa pembeni na wa nyuma kama huzitaki kwenye mlango wa mbele.
Pia waweza kuweka kile chuma cha kutolea matope pale ambapo kuna (au unategemea) kuwe na matope mengi na watie watu moyo kukitumia pale wanapokuwa wamebeba tope kubwa kwenye viatu vyao.

Chagua tandiko hizi za mlangoni kwa kuzingatia zinawekwa ndani au ni nje. Tandiko za mlango za ndani zinaonekana zaidi kama vizulia na zinasaidia kufuta majasho ya miguu. Hakikisha mlango unaweza kufunguka vizuri kizulia kikiwepo.

Kwa hivyo tandiko za mlangoni zinaweza kukaa kwa ngazi tatu kutokana na mahitaji yake. Zile za nje kabisa zikiwa ni kama brashi zikifuatiwa na za mseto ambazo ni mchanganyiko wa kubrashi na kunyonya majasho na za mwisho zikiwa ni laini kama zulia ambapo zote hizi zinasaidia kudaka uchafu kwa ngazi zote ili kuondoa kabisa uwezekano wa uchafu wa nje kuingia ndani.

Kama jamvi zitakuwa maeneo ambayo zitaloa mvua chagua staili ambayo itakauka haraka. Chagua zulia za mlangoni za ndani ambazo hazitaharibu sakafu ya chini yake na ambazo zitaendana na mapambo ya ndani yaliyopo. Je kizulia husika ni kwa ajili ya mapambo tu? Chagua rangi ambazo hazitaonyesha uchafu kwa mfano nyeusi na damu ya mzee na pia rangi zisizochuja.

Safisha jamvi na vizulia vya mlangoni mara kwa mara. Inawezekana vikajaa uchafu kiasi kwamba havisafishi viatu tena bali ndio vinavyochafua. Kung’uta, safisha kwa mashine ya upepo au fagia takataka zilizo juu juu. Kama tandiko ni kavu hatua hii itasaidia kuondoka uchafu mwingi kabla ya kusafisha kwa kulowesha kwa kuzipiga maji yenye shinikizo.

Vua viatu vyako wakati unaingia ndani mwako, hasa kama umetokea sehemu yenye matope au udongo mwingi. Jenga njia ya kuingilia kwa sakafu ngumu ili kufanya mazingira masafi kabla hujaingia ndani.
Kwa kuwa tandiko za mlangoni zipo za aina nyingi kutokana na matumizi baadhi ya watu wanapata taabu wakati wa kuchagua tandiko sahihi kwa mahitaji na ladha yao. Kwa sababu hiyo basi jiulize maswali mawili pale unapohitaji kununua tandiko jipya la mlangoni, ambayo ni “ unaenda kulifanyia nini hilo tandiko na unaenda kuliweka wapi?” Majibu ya maswali haya mawili rahisi yatakuongoza wewe mnunuzi na muuzaji kupata tandiko litakalokufaa kuendana na hitaji lako.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment