Thursday, July 25, 2013

My article for newspaper: Tablecloth



Vitu vya kuzingatia wakati wa kununua kitambaa cha meza
Kutandika kitambaa mezani kunatengeneza mandhari tulivu na kunaivalisha meza wakati wa chakula au tukio maalum. Kitambaa cha meza chaweza kuwa ni kwa ajili ya mapambo au kuilinda meza isidondokewe vyakula wakati wa kula. Kitambaa cha meza chaweza kuwa ni kwa matumizi ya meza ya ndani au nje. Sio gharama kubwa kununua au kushonesha kitambaa cha meza na huwa vitambaa hivi vinapatikana kwa rangi na michoro mingi.

Kitambaa cha meza chaweza kuwa cha nguo au jamii ya mpira.  Kwa kawaida vitambaa vya meza vya nguo ni rasmi kuliko vile vya mipira. Vitambaa vingi vya meza vya nguo vimetengenezwa kusafishika kirahisi, isipokuwa lesi, ambayo huenda ikahitajika kulowekwa na kufuliwa kwa mikono kwa uratatibu. Wakati wa kuchagua kitambaa cha meza cha nguo, chagua kile ambacho kinaendana na staili ya chumba chako cha chakula. Meza rasmi ya chakula inahitaji kitambaa rasmi cha meza.
Kwa umaridadi zaidi unaweza kutandika kitambaa cha lesi juu ya kitambaa cha meza cha nguo. Na pia unaweza kununua vitambaa vya meza viwili vya staili tofauti sahihi kwa muonekano rasmi au wa kawaida wakati wa kujumuika mezani kwa chakula.

Kama unachagua kitambaa cha meza kwa ajili ya meza ya nje, fikiria kununua cha mpira kwa ajili kitambaa cha nguo kinapauka kirahisi na jua na pia ni ngumu kukisafisha. Kitambaa cha meza cha mpira kinaweza kufutwa tu na kikatumika bila ya kukitoa mezani na kukifua. Vitambaa vya meza vya mipira huwa ni vya bei nafuu zaidi ila havidumu sana lakini vinastahimili zaidi mazingira ya nje.

Wakati wa kuchagua kitambaa cha meza inakupasa kutizama vitu kama rangi, ukubwa wa kitambaa, michoro na vifaa vilivyotengenezea kitambaa. Oanisha kitambaa unachotaka kununua na vitupio vingine hapo mezani kama vile mati, utambaa na napkini.

Matumizi ya kitambaa cha meza kwenye meza ya chumba cha chakula yanakuongezea nafasi ya ubunifu katika mapambo ya ndani mwako, hasa kama unataka kubadili muonekano lakini huna bajeti kubwa ya kupamba upya. Vitambaa vya meza vinakuja kwa kila rangi, na ni mahususi  kwa msimu wa sikukuu au mapangilio wa meza kwa mandhari fulani. Kuwa mbunifu kwa kuweka vyakula na mapambo yako ya meza kirahisi ili yasichoshe walaji walioko mezani.

Chagua kitambaa cha meza kilichotengenezwa kwa nyuzi za asili kwa kuwa huwa vitambaa vya aina hiyo vinakuwa laini na burudani zaidi kimuonekano. Kwa mfano vitambaa vilivyotengenezwa kwa pamba vinadumu kwa miaka mingi. Vitambaa vya meza vilivyotngenezwa kwa pamba na linen vimeonekana ni sahihi kwa matumizi ya mezani na vinadumu kwa muda mrefu.

Ukubwa wa kitambaa unahusu hasa pale unapotaka ni kwa kiasi gani kitambaa kining’inie kwa maana ya baada ya kitambaa kujaa mezani kile kinachodondokea chini kuelekea sakafuni. Kwa mpangilia wa kawaida wa meza kitambaa kinachoking’inia chaweza kuwa kifupi, kutegemea na maamuzi yako. Kama unapenda kuchagua mpangilio maridadi, kitambaa cha meza kinatakiwa kikaribie kabisa kugusa sakafu, na hii pia huleta muonekano rasmi zaidi. Kujua urefu wa kitambaa cha meza unahitajika kupima meza. Kwa meza zilizozoeleka za pembe nne, pima urefu wa meza ongezea na urefu wa mguu wa meza mara mbili ( Kumbuka kitambaa kinaanguka sawa panda zote za meza). Kama una meza ya yai ama duara, ni rahisi, nunua kitambaa cha yai ama duara na kumbuka kutumia mbinu ile ile ya kipimo ili kujua ukubwa wa kitambaa utakaoning’inia. Na pia kumbuka kuwa kuna vitambaa vingine ambavyo vimefungwa kwenye pakiti ambapo nje ya pakiti kuna vipimo vimeandikwa.

Kama una muonekano fulani kichwani na hujapata kitambaa sahihi, fikiria kushonesha kwa fundi. Vitambaa vya meza za pembe nne ni rahizi sana kushonesha na mara nyingi ndio meza ngumu kuweza kupata kitambaa cha ukubwa sahihi kilichotengenezwa tayari tayari. Kama utaamua kushonesha kitambaa kwa fundi hakikisha unakuwa na uhakika wa mambo kama kuchujiana rangi na pia kuna vitambaa vingine vinasinyaa na kupungua ukubwa vikifuliwa.

Kama wewe ni mtu unapenda sana mapambo fikiria pia marinda ya kona. Kitambaa cha meza kikifanya marinda maeneo ya kona kinaongeza umaridadi kwenye muonekano wa mapambo yako ya ndani.
Kwa kuwekeza kidogo, unaweza kununua au kushonesha vitambaa vya meza kwa ajili ya matukio yote na kuleta muonekano wa ukaribisho kwa meza iliyovalishwa maridadi. Unaweza kujikuta unafurahia muonekano huo na hivyo kufurahia msosi wako.

Usidanganyike kuwa kwa kusema tu ni meza ya yai ya watu 6 basi utapata kitambaa sahihi. Inaudhi umenunua kitambaa chako cha meza na mara unapokifikisha nyumbani hakitoshi mezani. Hakikisha unakuwa na vipimo sahihi vya meza yako kwa ajili ya kitambaa unachohitaji.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment