Muonekano wa bustani ya mawe pamoja na utengenezaji wake
Ni wachache wanaoweza kukataa mvuto ambao bustani za mawe unazo. Kama hujawahi kuona mojawapo, bustani ya mawe kwa lugha rahisi ni kijisehemu kwenye bustani kuu chenye mchanganyiko wa mawe na mimea kadhaa mifupi iliyooteshwa humo katikati ya mawe. Bustani ya mawe inaweza kuwa ni ya mandhari fulani na pale kwenye kilele wengine hupendelea kuweka pambo, kisanamu, maporomoko ya maji ama chungu cha maua. Kwa bahati nzuri, kuwa na bustani ndogo ya mawe ndani ya bustani yako kubwa ni rahisi ajabu na kunabududisha mno.
Bustani za mawe ni suluhisho kwenye ile sehemu kwenye bustani ambayo huielewi elewi. Sehemu mbaya au ngumu kupitisha mashine ya kukata majani kutokana na labda mteremko au kuwa na asili ya mawe mawe inaweza kurahisishwa utunzaji wake kwa kuifanya iwe eneo la bustani ya mawe. Ukisha kuwa tayari umejifunza mbinu chache za biashara hii, unaweza kutengeneza bustani ya mawe ambayo itaoana na mandhari ya bustani yako kubwa. Kwa maneno mengine baada ya kumaliza kuweka mandhari yako unaweza kurudi na kufurahia bustani. Hutakuwa na kazi ngumu mbele yako zaidi ya kumwagilia mara chache au labda kuondoa gugu moja au mawili.
Fikiria ni kwa namna gani aina nyingine za bustani ziwe ni za mbogamboga, zinavyoweza kuonekana vizuri ndivyo vivyo bustani ya mawe yapaswa kuwa. Kwa maana nyingine bustani ya mawe iliyobuniwa vizuri kwa kuotesha vimimea vidogo na vya kipekee ambavyo vingeweza kusongwa na kumezwa kwenye bustani nyingine visionekane vinavyoweza kustawi kwenye bustani yako ya mawe na kuleta wivu hata kwa wageni wako.
Kama umebahatika kuwa na sehemu yenye kimlima kwenye bustani yako kubwa ambapo panapata jua la moja kwa moja, hapa ndio mahali sahihi pa kujenga bustani ya mawe iliyojaa muonekano wa asili. Kama hujawa na eneo lenye kimuinuko bado pia una chaguzi nyingi; ni kiasi cha kuchimba na kuweka msingi kwenye eneo ambalo litakuwa ni bustani yako ya mawe. Wengine huwa wanatengeneza bustani za mawe ili kutumia lile eneo lenye kimuinuko ndani ya bustani zao, wapo wengine wanaoingiza mawe ndani ya bustani zao ambazo ziko flati na hazina mawe, ni kazi kubwa lakini inalipa.
Kwenye kuchagua mawe ya kuweka kwenye bustani ya mawe wenye nyumba wana chaguzi mbali mbali. Wengine wanaangalia rangi ya mawe ambayo itahusisha pia mimea wanayochagua kuotesha humo, na wengine wanalenga mawe ya mndhari fulani. Kwa mfano mtu anaweza kuchagua bustani ya mawe mekundu na akafikiria kuweka maua na mimea yenye wekundu kiasi. Kwa bustani ya mawe kinachojalisha ni muonekano na sio ubora.
Kuna bustani za mawe ambazo zimenyanyuka sana kulinganisha na usawa wa eneo lingine la bustani, na zipo ambazo zimenyanyuka kidogo na kwa mfano kama zikiwa ndani ya maua mengine yaliyooteshwa kwenye udongo wa usawa wa ardhi basi bustani hizo za mawe zinaweza kulingana urefu na mimea hiyo.
Bustani za mawe kwa kanuni huwa zinakuwa na udongo kidogo (pale unapootesha maua na mimea mingine) ambao unapitisha maji vizuri kwa hivyo unatakiwa kuotesha mimea ambayo itakubaliana na udongo huu. Na pia kumbuka kuchanganya udongo na mbolea. Tumia mawe makubwa kwa kuanzia chini kwenye ardhi. Mawe haya ya kuanzia yanaweza yasihitaji kuwa na mvuto. Kwa mzunguko unaofuta mawe yanatakiwa kuvutia kwani ndipo jicho linaanza kuona na unatakiwa kuacha nafasi nafasi za kuotesha maua. Kadri unavyootesha, ongeza mawe. Kumbuka hii ni bustani ya mawe, muonekano unaotakiwa ni lundo la mawe na mimea inayochomoza kwenye kreki zake.
Kama tulivyokubaliana uzuri wa bustani ya mawe ni pale inapojengwa mahali penye jua la moja kwa moja kwa hivyo wakati wa kuchagua mimea kumbuka kuchagua ile inayostahimili jua kali na zingatia urefu wa mimea pia. Isijekuwa mirefu ya kufunika mawe yako. Kwenye makala zijazo nitazungumzia mimea inayofaa kuotesha kwenye bustani ya mawe.
Kama una bustani ya mawe labda ungependa kunishirikisha mawazo machache kuhusu ni kwa vipi uliijenga. Kwa mfano:
- Ni mawe ya aina gani ulitumia na je ulichagua mandhari fulani kwa mfano mawe na mimea ya ufukweni labda, n.k?
- Je mawe hayo yalikuwa tayari kwenye eneo husika au uliyaleta hapo?
- Ni mimea gani uliyotumia na kwa nini?
- Je kuna kitu cha ziada kwenye bustani yako ya mawe zaidi ya mawe na mimea/maua (kwa mfano maanguko ya maji ama kisanamu au pambo lingine lolote?)
No comments:
Post a Comment