Thursday, April 24, 2014

my article for newspaper: garden entrance


Jinsi ya kutengeneza na umuhimu wa eneo la kuingia kwenye bustani
Eneo la kuingia kwenye bustani ya maua ni kiungo muhimu cha bustani ya nyumba yako. Ni eneo sahihi la wewe mwenye bustani kuonyesha ladha na ubunifu wako binafsi.
Muonekano wa kuvutia wa eneo hili sio tu unaboresha muonekano wa bustani bali pia ni ishara kwa wageni wako kuwa wameshafika bustanini.  Eneo hili ni kama linasema“hapa ndio mahali panapoanzia bustani yangu ya nyumbani,” anasema mbunifu wa bustani Bi Tatu Mbegu.
Kuna staili nyingi tofauti za eneo la kuingia kwenye bustani au sehemu nyingine ya nje ya nyumba. Katika makala hii mbunifu Tatu Mbegu anakushauri aina hizi mbalimbali na ndipo utakapoweza kuamua ni ipi itafaa kwenye bustani yako.

Sehemu ya kuingia kwenye bustani inaweza kuwa eneo rahisi tu kwa mfano mawe mawili yaliyowekwa mkabala katika eneo hilo, vyungu vya maua, kiingilio kama fremu ya mlango kwa mfano wa vibao vya kupishana au hata chuma, milingoti miwili iliyozungushiwa mimea mitambaazi na hata geti la chuma na kadhalika na kadhalika. Uwezekano ni mwingi na upeo ni mwisho wa ubunifu wako. Vizuri, kitu muhimu cha kufahamu ni kuwa ni eneo la mwanzo linaloonekana kabla ya kuingia kwenye bustani, anasema Tatu. Eneo hili linatoa tamko la papo kwa papo la utambulisho wa mwenye bustani na linaleta mguso wa eneo lingine lote la bustani lililobakia.

Mbao na chuma zinaweza kuchanganywa kwa uzuri na kufanya eneo la kuingia. Vifaa vya ujenzi navyo vinafanya wigo mpana wa kuchagua mtindo wa muonekano wa eneo hilo. Kama unadhani mbao zinaonekana kuoza sana ndani ya muda mfupi basi tumia chuma peke yake.
Pamoja na hayo ni muhimu kufahamu kuwa sio kila eneo la kuingia kwenye bustani liko mbele ya nyumba. Wengine hupendela kugawa bustani kwenye vyumba na hivyo kuwa na maeneo tofauti ya kuingia katika kila chumba.

Kuzungushia hiyo fremu ya eneo la kuingia kwa mimea na maua inaonyesha ubunifu zaidi. Mgeni anayepita chini ya kivuli anafunikwa na kijani na hivyo kujisikia burudani kwa hewa safi.
Hii yote inatokana na ladha ya mwenye nyumba, muonekano na bajeti. Eneo la kuvutia la kuingia kwenye bustani ni utambulisho wako kwa mapambo yako ya nyumbani.

Sasa unaanzaje kupata mawazo ya jinsi ya kutengeneza eneo la kuingia? Bi Tatu anajibu swali hili kwa kusema kuwa anza kubuni kwa kuangalia kwanza bustani yako kwa ujumla. Ni wapi ungependa kuweka eneo la kuingilia? Wakati mwingine uamuzi unatokana na eneo lililozoeleka kupitwa hapo kabla, na pia ni jinsi gani ungependa wageni waifikie nyumba yako? Je unapenda kubuni njia ya moja kwa moja kutoka kwenye bustani kuingia kwenye nyumba ama kuwe na kona ya kuingia kwenye bustani kwanza kabla ya kufikia mlango wa mbele wa nyumba?
Halafu jifanye kama wewe ni mgeni kwenye makazi yako mwenyewe. Jiulize kama ungefika mahali hapo kwa mara ya kwanza ni wapi ungepitia kufika bustanini. Sasa weka baadhi ya maelezo haya kwenye mawazo yako ya kuamua ni wapi utengeneze sehemu ya kuingia kwenye bustani yako.
Hakikisha kuwa utatumia njia yako ya kuingilia kwenye bustani. Hii ina maana kuwa kama utaitengeneza mahali ambapo huvutiwi kupitia basi ni dhahiri kuwa utaitumia kwa mara chache sana au hata inawezekana hutaitumia kabisa. Kwa hiyo kabla hujatengeneza njia hakikisha kuwa utaitumia.

Muonekano wa eneo la kuingilia uwe ni muendelezo wa mapambo mengine ya nyumba yako. Kama nafasi inaruhusu tengeneza eneo la kutosha kwa ajili ya kupitia watu kadhaa. Eneo la kuingilia la upana mdogo zaidi ni mita moja na nusu kwa bustani ya wastani hadi mita mbili na nusu kwa bustani kubwa, anasema Bi Tatu.

Mwisho fikiria bajeti; haihitaji hela nyingi kutengeneza eneo la kuingia kwenye bustani. Kama mbunifu alivyosema kuwa hata vyungu viwili vilivyooteshwa maua vikawekwa mkabala vinaweza kufanya eneo la kuingia kwenye bustani, au hata boda za maua zilizozunguka bustani zinaweza kuachwa nafasi ya eneo la kuingilia na ikawa ndio hicho tu unachohitaji. Ni rahisi tu kama hivyo wala haihitaji mambo makubwa.
Wawezeshe wageni wako kupunguza mwendo wanapofikia bustani yako kwa kuweka njia ya kuingilia, watafurahia kwa undani maua mazuri na mimea laini ya bustani yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment