Tuesday, April 8, 2014

my article for newspaper: chumba cha binti - tumboni hadi 18


Karibu msomaji kwenye makala ya leo ambayo nitaongelea jinsi ya kupamba chumba cha kulala cha binti yako miezi michache kabla hajazaliwa hadi akiwa na umri wa miaka 18.  Fuatana nami kwenye makala hii.
Sasa basi ni miezi michache imebaki kabla binti yako hajazaliwa. Kutokana na teknolojia kuwa juu mama mjamzito amepewa uwezo wa kujua jinsia ya mtoto wake aliye tumboni kama atapenda kufanya hivyo. Endapo basi wazazi watakuwa wanatarajia kuna binti yao anakuja duniani basi moja kwa moja wanaanza kufikiria kitanda cha mtoto na nguo na mapambo ya rangi za pinki, njano na kijani ambazo zitatawala chumba cha kijacho. Wakati ukiwa kwenye maandalizi hayo ni vyema ukaandaa kwa kufikiria miaka mitano hadi kumi mbeleni.

Kutokana na ukali wa maisha jaribu kuweka vitu ambavyo ni vya kudumu kwa kukumbuka kuwa kila kitu unachoweka kwenye chumba hiki ni chake na atakitumia kwa miaka 18 inayofuata  na hata kama ni mabadiliko yawe madogo yasiyo na gharama kubwa. Sasa utaniuliza je, kitanda cha mtoto kitatumika kwa miaka 18?  Endelea kujisomea ili upate jibu la hili swali. Rangi za pinki, njano na kijani nazo pia ni sawa kwa chumba cha mtoto wako wa kike mchanga lakini jaribu kutumia rangi ambazo zinakaa kati. Kwa mfano ukitumia pinki iliyokolea na njano ya mwanga wa jua kama rangi za ukuta wa chumba cha binti yako vitadumu hata atakapokuwa mkubwa na ataipenda pinki hii kuliko ile nyepesi ya kitoto!

Kununua fenicha ambazo zina matumizi zaidi ya moja na ambazo zinaweza kukaa kwenye chumba hicho kwa muda mrefu inaweza kuwa changamoto kuliko swala la rangi. Unahitaji kutembelea maduka mbalimbali ya fenicha na pia karakana za waseremala. Wote tunajua kile kitanda cha kichanga binti yako hawezi kukitumia kwa miaka 18 ijayo. Ni sawa kuwa na kitanda cha mtoto kwa ajili kina vizuizi pembeni ili asianguke. Ila ili kuweza kuwa na matumizi ya kitanda hiki kwa umri wote wa utoto wa binti yako tafuta kitanda cha bebi ambacho kinaweza kugeuzwa na kuwa cha binti hapo baadaye. Kuna baadhi ya maduka ya fenicha ambayo unaweza kupata kitanda kama hiki. Vinginevyo unaweza kwenda kwenye karakana za waseremala na kuagiza utengenezewe kitanda cha kikubwa ila kiwekwe vizuizi ambavyo vitafanya kazi kama ile ya kitanda cha bebi.
Hapo baadae kadri binti yako anavyokua unapamba chumba chake upya ambapo utaondoa vizuizi na kitabakia kuwa kitanda cha binti na sio bebi tena. Mzazi siku hizi usitafute kitanda cha bebi kinachosimama peke yake. 

Tafuta ambacho bebi yako pia atakitumia akiwa binti, kwa njia hii utakuwa umetumia pesa yako kwa busara. Usitumie hela nyingi na uchumi huu kununua vitu ambavyo utaviondoa tena miaka michache itakayokuja. Kama unataka kuongeza kitu kwenye chumba cha mtoto wako ambacho anafurahia sasa lakini sio hapo baadaye hakikisha sio cha gharama kubwa na ni rahisi kukiondoa.

Chumba cha kulala cha binti yako ni sehemu ambayo atatumia muda mwingi zaidi wakati akiwa msichana mdogo, atakuwa analala hapo pia wakati mwingine atacheza na madoli yake hapo. Kuwa mbunifu kwenye kupamba chumba hiki na utumie gharama za kawaida. Weka zulia la rangi moja ambalo utaweza kutupia kizulia kingine kidogo cha rangirangi juu yake pale pembeni ya kitanda. Kizulia hili kidogo rangi kuu ziwe zinaendana na rangi nyingine za hapo chumbani hata kama ni pazia ama shuka ama ukuta. Zulia litasaidia kuweka miguu ya bintiyo kwenye joto na hata akiwa amekaa chini na pia linaongeza uzuri wa muonekano wa chumba. Mwekee shuka, mito na pazia zinazooana na rangi ya mandhari uliyochagua. Chagua pazia na shuka za kike na pia zenye rangirangi kama maua au nyota au hata rangi za upinde wa mvua.

Hatimaye binti yako mdogo anaanza chekechea; muda unakimbia. Weka mpangilio wa chumba kivingine ili kutengeneza nafasi kubwa ya kucheza na matoi na kusuka madoli yake. Kadri binti anavyokua, ladha yake inabadilika kwa kasi siku hadi siku achilia mbali mwaka hadi mwaka. Unaweza ukatetea kutumia hela kwa umakini kwa ajili ya chumba chake kwa kujua ni nini cha kununua na jinsi ya kukitumia.

Unapamba chumba chake tena kwa awamu nyingine ya kikubwa. Chagua mandhari itakayotokana na vitu na rangi anazopendelea binti yako kabla ya kumshtukiza na kuanza kupanga na kuweka vitu upya chumbani kwake. Pia unaweza kupamba nae pamoja. Anza kwa kupaka tena rangi na baada ya hapo ongeza fenicha ambazo bintiyo atahitaji ambazo ni kimeza na kiti chake , meza ya kuvalia, kisofa kidogo na kishelfu cha vitabu. 

Rangi ya vitu hivi iendane na mandhari uliyochagua. Kwa mfano kama mandhari ni rangi ya pinki, usiweke sofa ambalo halioani na pinki. Pia sasa ni wakati wa kuondoa zile mbao za kuzuia asianguke na kitanda kubakia cha binti mdogo sio kile cha kichanga tena.

Kwenye droo za hiyo meza ya kuvalia hifadhi vitu vyake vya michezo na vitu vidogovidogo viwekwe humo visitupwetupwe. Kwenye droo hizo weka kwa mpangilio ili asipate shida kuona vitu. Kama kutakuwa na nafasi ya ziada pia weka kiti cha kubembea. Mabinti wanaokua wanakipenda kukalia wakati wa kusoma kitabu cha hadithi, gazeti au jarida. Kwa ajili miaka imeenda kile kizulia cha rangirangi ulichotupia juu ya lile zulia la rangi moja unaweza ukakibadilisha kwa  kumnunulia kingine. Maadam sasa ni mkubwa ataweza kuchagua rangi anazopenda ambazo zitaoana na zingine hapo chumbani.

Baada ya hapo unaweza ukaenda na bintiyo kweye maduka ya mapambo ya ndani akachagua vitu vidogodogo vya kuongezea kama taa za vivuli fremu za picha, kifungashio cha kalamu na penseli kwenye deski lake, mishumaa na kibox cha kuweka hereni na mikufu na vitu vyake vingine vya urembo. Na pia kama atapenda waweza mwekea vioo vya ukutani. Sasa kitu pekee anachohitaji kwenye lile deski ni kompyuta. Mzazi usione bintiyo anataka kutumia kompyuta yako ukamfukuza. Ni muda wake nae kuwa na yake kwake.

Kwa majumuisho, pamba kwa jinsi ambayo chumba kinakuwa na mwanga wa kutosha na sehemu kubwa ya kuhifadhi vitu ili asitupetupe vitu chini kwa madai ya kuwa hakuna nafasi ya kuweka. Mwanga wa kutosha na deski ni kwa ajili ya kujifanyia kazi zake za shuleni. Na kama unapenda binti yako ajenge tabia ya kujisomea basi usidharau umuhimu wa kumwekea shelfu la vitabu kwenye chumba chake kuweka vitabu vyake vya zamani na vipya mahali pamoja.

Hongera! Umefanikiwa kupamba chumba cha binti yako toka akiwa bebi hadi miaka 18 bila usumbufu mkubwa, muda au pesa nyingi!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment