Kama itathibitika ni kweli, unadhani adhabu ya miaka 30 jela inamtosha mbakaji huyu? Mkazi mmoja wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani
amekamatwa na polisi akituhumiwa kuwabaka watoto wake wawili wadogo kwa zaidi
ya miaka miwili sasa.
Habari zilizolifikia Mwananchi, zilisema kuwa katika
tukio hilo ambalo limethibitishwa na polisi na watoto wenyewe, baba huyo
alianza kuwafanyia binti zake vitendo hivyo mwaka 2013 kwa siku ambazo mkewe
ambaye ni mama wa wasichana hao hakuwapo hadi usiku wa Machi 19, mwaka huu. Kwa
sasa tunayahifadhi majina ya familia hiyo.
Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 15 anayesoma darasa
la saba na mdogo wake mwenye umri wa miaka 11 aliyeanza kubakwa akiwa darasa la
tatu.
Kwa mujibu wa watoto hao, baba huyo alikuwa anamuita
mmoja wa watoto wake chumbani kwake na kumtaka alale na mdogo wao wa kiume
wakati huo akiwa na mwaka mmoja na binti akipitiwa na usingizi humvua nguo za
ndani na kumwingilia huku akimtaka kukaa kimya na kuvumilia maumivu.
Mke wa mtuhumiwa huyo, ambaye amekuwa akizimia mara kwa
mara kutokana na kulia baada ya kubaini mchezo huo, alisema aligundua watoto
wake wanabakwa Ijumaa iliyopita baada ya mmoja wa mabinti zake hao kumweleza
kuwa baba yake alikuwa amembaka Machi 19, mwaka huu.
Alisema kabla ya binti huyo kumweleza hivyo, alimwomba
asimpige kwani kuna kitu anataka amweleze, japo ni kibaya lakini yeye
amechoshwa na kimekuwa kikimuumiza kichwa.
“Alisema kila ninapokwenda katika biashara zangu,
anatamani nisiwe ninawaacha hapo, nikamwahidi sitamfanya kitu ili mradi aseme
ukweli tu,” alisema mama huyo.
Baada ya kuhakikishiwa kulindwa, ndipo binti huyo
aliposimulia jinsi ambavyo baba yake amekuwa akiwafanyia na kuwatishia wakipiga
kelele atawaua.
“Niliposikia mwili ulisisimka na ghafla binti yangu
mwingine naye akatokea akilia na kuniambia, ‘hata mimi baba ananifanyiaga
hivyohivyo kila siku unapokuwa umepeleka mboga sokoni Kariakoo,” alisema mama
huyo.
Mwanamke huyo ameomba sheria ichukue nafasi yake katika
tukio hilo kwa kuwa ni la kinyama na pia wataalamu wa saikolojia wamsaidie
binti yake mdogo wa darasa la tano kwani yeye ameathirika zaidi.
Daktari aliyewapima watoto hao, ameshauri binti huyo
mdogo apate ushauri zaidi ili kurudisha akili yake katika hali ya kawaida.
Simulizi za watoto
Wakizungumza nyumbani kwao jana watoto hao, walisema baba
yao alikuwa akiwatishia kuwakatakata kwa panga au kuwakaba koo humohumo
chumbani endapo wangethubutu kumweleza mtu yeyote kitendo wanachokifanya.
“Tulikuwa tumeingia kwetu kulala na wadogo zangu,
nikasikia ananiita nikambembeleze mtoto eti anamsumbua, nilikwenda
nikambembeleza akalala, wakati nashuka
kitandani kurudi chumbani kwetu baba akanivuta kwake akanivua, akasema anachokifanya
ni suna kwa hiyo hataki kelele, akisikia atanikaba nife.”
“Niliumia sana na asubuhi mama alirudi nikajitahidi kweli
asijue na hata shule sikwenda, jioni mama aliondoka tena baba hakuniita siku
hiyo lakini baada ya siku tatu aliniita tena ikawa vilevile navumilia. Siku
zilivyozidi unaweza kukuta kwa wiki naitwa hata mara nne siku ambazo mama
hayupo nyumbani,” alisema.
Watoto hao walieleza kuwa baadaye baba huyo alihamia kwa
binti mdogo kwa staili ileile na kila mmoja alikuwa akiitwa kwa zamu na kwa
vile kila mmoja alijua ni siri yake na baba. Kutokana na woga wa kuuawa, hakuna
aliyemweleza mwenzake hadi katikati ya mwaka jana mmoja wao alipomweleza
mwenzake na baadaye kumweleza mama yao.
“Baba alikuwa anasema atatuua bila hata mtu kujua na
tutaozea shambani, hata nikiwa katika siku zangu baba ananiingilia hivyohivyo,
naugua kila mara UTI, mdogo wangu naye kila mara UTI, tukaamua liwalo na liwe
kama kufa basi ila mama ajue,” alisema mtoto huyo huku akibubujikwa na machozi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembe Saba, Hamis
Shomari alisema kabla ya kupelekwa kituo cha polisi Kongowe Jumamosi iliyopita,
watoto hao waliitwa shuleni hapo na kuhojiwa kila mmoja peke yake na wote
walikiri kuanza kubakwa mwaka 2013 na baba yao na kwamba tabia hiyo iliendelea
hadi Machi 19 usiku alipobakwa binti mdogo kwa mara ya mwisho na Machi 20
walipoamua kumweleza mama yao.
Kamanda wa Polisi
mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na kwamba
wasichana hao wamefanyiwa vipimo mbalimbali na majibu ya daktari yamethibitisha
kuwa wamebakwa na sehemu zao za siri
zimeharibiwa, hivyo wanaendelea na matibabu.
No comments:
Post a Comment