Mlango wa mbele wa nyumba yako ni kielelezo chako.
Mlango huu zaidi ya kuleta mvuto wa nyumba pia unakuhuisha mara uingiapo
nyumbani.
Mlango wa mbele ni moja ya vitu vya mwanzo watu
wanavyoona kuhusu nyumba. Rangi, staili na hali yake ni sehemu kubwa ya jinsi
nyumba inavyoonekana kwa nje. Mlango huu una kazi ngumu ya kufanya nje kuwe nje
na ndani kuwe ndani. Unapata adha ya unyevu, jua, upepo na hata vumbi na kama
umetengenezwa kwa mbao kuna uwezekano wa kusinyaa na kuvimba kuendana na hali
ya hewa ya majira ya mwaka. Hali hii inafanya mlango kuwa mgumu kufunguka
nyakati nyingine au kupiga kelele. Njia nzuri ya kuzuia ni kuhakikisha mlango
umepakwa dawa sahihi za kuzuia hali hii kabla ya kuujengea kwenye nyumba.
Mlango wa mbele wa nyumba unaweza kuwa wa mbao,
chuma ama glasi. Vyovyote uwavyo uangalizi wa mara kwa mara unahitajika ili
kuufanya uonekane maridadi kila wakati. Kama mlango unapigwa na jua la moja kwa
moja hakikisha unaupaka rangi au finishi
inayonyonya miale ya jua ili kufanya rangi yake idumu muda mrefu.
Kaya nyingi zimefanya mlango wa mbele kuwa rasmi kwa
maana ya kwamba unatumika zaidi na wageni. Kutokana na kuwa hautumiwi mara kwa
mara ni muhimu kuhakikisha kuwa unafanya kazi jinsi inavyotakiwa. Swali ni kuwa
ni kwanini watu wengi hawatumii mlango wa mbele mara kwa mara? Ni kama vile
mlango huu umewekwa kwa ajili ya wengine na wanafamilia hawastahili kuutumia
wao wenyewe ambapo wengine hao huja na kuutumia mara chache kwa mwaka. Wakati mwingine
hata marafiki na majirani wakija nyumbani, wanatumia mlango wa nyuma au wa
pembeni ila sio wa mbele. Matokeo yake mlango wa mbele unakaa tu bila kutumika.
Watu wengi wanaingia ndani mwao kwa kupitia mlango
wa nyuma ambao labda umeunganika na varanda iliyojazwa vitu vingi ama hata
pengine umeunganika na gereji. Ule usemi wa unachokiona mwanzo kinadumu zaidi
ni muhimu sana hapa. Kama unaingia ndani ya nyumba kupitia mlango wa nyuma uliojaa
makorokoro na vifaa vya miradi ambayo haijakamilika au hata vifaa vya bustani moja
kwa moja utajisikia kuchoka hata kabla hujafika ndani. Nyumbani kwako
panatakiwa kuwa himaya yako. Jipe raha kwa kupitia mlango wa mbele, hata kama
inamaanisha kuegesha gari yako kwanza halafu unazunguka mbele. Utashangaa ni vip
utakavyohuisha nafsi yako!
Mlango wa mbele unasema mengi kuhusu watu wanaoishi
kwenye nyumba husika. Kuna watu eneo la ndani la mlango huu linatumika kama
stoo. Mlango wa mbele uliozibwa kwa ndani ni alama kuwa wenye nyumba hawataki
mtu apitie mlango huo.
Kwa kawaida kitu kinachokuvutia kinakuhamasisha na
hivyo kukuongezea nguvu mwilini. Kama mlango wa mbele unakuhamasisha ina maana
nguvu inazalishwa. Kama huo mlango huupitii hata mara moja kwa mwezi basi hamna
nguvu.
Mazingira
ya mlango wa mbele kwa nje ni muhimu sana. Je ni rahisi kuuona mlango uko wapi
na kuna njia nyepesi ya kuufikia? Je maua na mimea ya eneo lile imepunguzwa
kuufanya mlango uonekane? Jicho linavutwa kuutazama na ni nini hasa
kinachokuvutia ukitazama maeneo ya nje ya mlango wa mbele wa nyumba yako? Mlango
wako huo unavutia vile ambavyo unasema unapenda katika maisha? Njia ya kueleweka kupitia mlango wa mbele, rangi za kuvutia
au mapambo, ni hatua za kwanza kukuwezesha kutumia mlango huo na hivyo
kujiongezea nguvu ya kusonga mbele na maisha. Weka eneo la mlango safi na huru,
kwa ndani pasiwe stoo na mwisho utumie mlango huu. Kama bado unashawishika kuwa
ni usumbufu kutumia mlango wa mbele kwa kila siku basi amua kuutumia japo mara
moja kwa wiki. Ukiwa unajua kuwa unajiongezea nguvu kwa kutumia mlango huo.
Kwavile imeonekana kuwa kaya nyingi hazitumii mlango
wa mbele kila siku, basi ni vyema kuhakikisha na kucheki mara kwa mara kuwa
mlango unafanya kazi vyema na hata eneo lake ni safi kwa ajili ya ukaribisho
rasmi wa wageni. Usianze kuondoa buibui, vumbi na mavi ya mijusi kwenye mlango
wako huo mbele ya mgeni wakati wa kumfungulia. Fanya hatua ya mwanzo ya mgeni
anayekutembelea kuwa ya kumbukumbu. Pia hakikisha kuwa kile kizulia cha
mlangoni ni kisafi.
Macho yanafurahia kuona vitu vizuri, mlango wako wa
mbele ni moja ya pambo la kwanza kabisa wageni wanaloona wanapofika nyumbani.
Mlango wako uvutie na uoane na mapambo yako mengine ya nje ya nyumba. Mlango
huu pia unakulinda unapokuwa ndani, kwa hiyo unatakiwa kuwa imara.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023
No comments:
Post a Comment