Chumba
cha kulala cha wakuu wa familia ni kama mahali patakatifu
Chumba hiki ni kile cha baba na mama wa familia – ni koloni lao hapo
nyumbani kama wengine wanavyoweza kusema. Wazazi mkiwa ndio nguzo ya familia basi
mnahitaji chumba cha kipekee. Mnaokaa kwenye chumba hiki ndio mnaolipa bili na
kufanya kazi kwa bidii ili mfanikiwe kwenye hilo. Kwa nini chumba chenu kisiwe
maalumu? Wakuu wa familia mnastahili chumba hiki!
Je wewe mkuu wa familia unakipenda chumba chako cha
kulala? Chumba hiki kiwe kama mahali patakatifu kwa wanandoa au yeyote
anayelala mle. Ni nini cha kwanza unachokiona mara baada ya kufungua mlango wa
chumba hiki, na ni nini unachokiona cha kwanza mara baada ya kufungua macho
asubuhi. Chumba hiki kiwe ni sehemu huru pasipo na usumbufu kama wa kufua,
kompyuta au midoli ya watoto. Midoli imekuwa ni tatizo kwenye chumba cha kulala
hasa kwa wazazi wanaokimbia mchakamchaka wa maisha ya kila siku. Midoli
inaishia chumba cha wazazi na hata kitandani.
Kuwa wazi na kuweka mipaka juu ya
chumba hiki na hata midoli ya watoto isijazane chumbani kwako na kitandani. Kwa
ujumla watoto wawe na sehemu ya kucheza na kuweka midoli yao. Chumba cha kulala
cha wakuu wa familia ni cha watu wazima ndani ya familia.
Fenicha kuu kwenye chumba hiki ni kitanda. Kimsingi, kitanda kina lengo moja kuu: ni
kufagilia usingizi wenye afya. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia
kinahitaji kitanda chenye kukidhi vigezo vya usingizi bora. Kama matangazo
tuseme ya magodoro yanavyoonyesha ni kuwa tunatumia theluthi moja ya maisha
yetu kulala. Sasa kwa nini godoro, malazi na fremu ya kitanda visiwe maalumu. Kuna
njia nyingi ya kupata kitanda bora kwa bajeti yeyote. Kitanda chenye fremu ya
chuma tuu kilichosogezwa karibia na ukuta hakikidhi vigezo. Kila kitanda
kinahitaji bodi la kichwani (makala zijazo tutaongelea umuhimu wa bodi hili) ambayo
yanapatikana kwa saizi na mitindo mbalimbali.
Kwakuwa msisitizo wa chumba hiki ni kwa
wanandoa kama kuna sehemu kubwa weka sofa au viti viwili vya kukalia badala ya
kimoja. Mara zote fikiria vitu kwenye seti. Kama wewe ni mwanaume au mwanamke uliye
singo lakini ndio mkuu wa familia weka picha ya peke yako kusisitiza
utambulisho wako kuwa huna mtu. Kama mnaolala humo mko kwenye mahusiano basi
mambo ni kwa seti kama vile taa za vivuli mbili, vimeza vya kando viwili na
hata kama mishumaa basi miwili. Kumbuka unatengeneza mandhari ya
kupumzika na kuondoa msongo wa mawazo wa siku nzima.
Chagua sanaa inayoelezea uhusiano wenu iwe ni picha
ya ngalawa, ndege au hata maneno ya kimahaba. Sio sawa kuweka picha za
marafiki, mababu na hata wanafamilia wengine kwenye chumba hiki. Tatizo ni kuwa
chumba kinaanza kuonekana kinguvu kimezidiwa na vitu. Watu wote hawa wana haja
gani chumbani kwako. Pambeni chumba cha kulala kwa picha zenu nyie wanandoa mnaolala
humo.
Epuka rangi za kukolea sana kwa mfano kama ukiweka
pazia za damu ya mzee au bluu ya weusi inaweza kuwa tabu kuamka asubuhi kuwahi
kutafuta rizki. Kanuni inasema kuwa mlango usiwe mstari mmoja na kitanda, kwa
maana ya kuwa ukiwa umelala kitandani uuone mkango lakini ukifungua mlango
macho yasione kitanda moja kwa moja. Mlango ukiwa namna hii unawapa walalaji
kujiamini zaidi kuwa wanamiliki chumba na usingizi unakuwa mwororo.
Vifaa vya umeme leo hii ni changamoto kwenye chumba
cha kulala. Kompyuta, luninga na vifaa vingine vya umeme vinatuzunguka na
kutunyonya nguvu kwa kuleta nguvu ya
uvutano mithili ya sumaku ambayo baadaye inaleta msongo wa mawazo. Ili
kupumzisha mwili na kuuweka katika afya njema basi ni vyema kuwa mbali na vifaa
vya umeme chumba cha kulala. Kama hamna jinsi kuwa ni lazima vifaa hivi viwepo
chumbani basi sio tu vizime na kuacha vijitaa vinawaka bali chomoa kabisa
kwenye umeme wakati wa kulala.
Kumbuka
kuwa kila kitu kwenye nyumba tunazoishi kinatupa ujumbe. Chumba chako cha kulala
wewe mkuu wa familia kinakupa ujumbe gani? Je kinakukumbusha majukumu yote unayohitajika
kukamilisha au kinakupa hisia za utulivu na kukukaribisha kupumzika? Je kinakushawishi
kuwasha luninga au kinakuleta kwenye faragha? Je kinaongeza msongo wa mawazo kwenye
maisha yako? Au kinakupa pumziko la nafsi hata kama uko singo? Kama ndio basi
umetengeneza chumba cha kulala ambacho ni kama mahali patakatifu.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O.
Machange. Kwa maoni tuwasiliane kwa barua pepe viviobed@yahoo.co.uk
au kwa simu 0755 2000 23
No comments:
Post a Comment