Saturday, October 20, 2012

nikumbuke kwenye ufalme wako wa kuosha gari

tunapenda usafi. hutajutia hela yako. hatuna presha wala papara tunakusafishia gari yako tukiwa tumetuliza akili...karibu Ian CAR WASH survey karibia kabisa na pub le maarufu sana BRAJEC. tuonane weekend hii...xo

Friday, October 19, 2012

ukifanya haya utakuwa kwenye mahusiano yenye afya



Njia 3 za kufanya kuwa mahusiano mazuri zaidi
Mimi sio expati wa mahusiano. Ila nimegundua kuwa japo kila mahusiano ni ya kipekee na yanatofautiana ya kati ya  mtu na mtu kuna vitu vitatu ambavyo mahusiano yoyote yakivifuata vitaboresha uhusiano wa mtu na mwenzie.  Nakualika kujua hivi vitu vitatu tu: Kuwa mkweli. Kuwa tayari kukubaliana kutokubaliana . Kuwa tayari kukimbia.

Kuwa mkweli

Kutokuwa mkweli katika mahusiano ni sumu. Ni ngumu sana kukumbuka uongo wote uliowahi sema na ni nani ulimwambia. Kudanyanywa kunaumiza, Kuna faida nyingi ukiwa mkweli kwa patna wako. Kuna uhuru unaokuwa  ndani yake na ulinzi wa kujiamaini kuwa unaambiwa ukweli daima.


Kuwa tayari kukubali kutokubaliana


Inapokuwa ulikuwa singo kwa muda, una maono fulani kichwani kwako juu ya mambo fulani kuwa ndivyo unavyotaka yawe. Mara anakuja huyu mtu ambaye umempenda lakini ana mawazo tofauti na yako kwa labda kila unachotaka. Unajikuta inabidi ulegeze msimamo wako kiasi. Na unaona ni sawa tu. Lakini vinakuja vile vitu ambavyo unajisikia kabisa lazma viwe hivi na sio vile, unatakiwa kuwa na uhakika kuwa patna wako amekubaliana na wewe. Kwa hiyo ukiweza kulegeza msimamo kidogo na kuweka wazi kwa patna wako mnaweza kuja na solution ambayo itakuwa bora zaidi na wote mkaifurahia.


Kuwa tayari kukimbia


Fuata moyo wako. Unajua wakati mambo hayaendi sawa au jambo fulani patna wako alilofanya halileti heshima kwako. Ujue nini, unatakiwa ujipe raha mwenyewe. Kama unahisi kuwa hufurahii mahusiano yako ni sawa kukimbia hata kama ni kwa muda ili utulize kichwa uamue ni nini hasa unataka. Usijali watu watasema nini: chukua maisha yako mikononi mwako. Saa nyingine kujiondoa kwenye uhusiano ni kitu chema zaidi unachoweza kufanya kwako na kwa huyo mtu mwingine.

Thursday, October 18, 2012

eye catcher..


Njia mbalimbali za kuulamba polka dots





kama una picha yako umeulamba polka dots nitumie nami nitairusha

pata somo hapa

na hiki ndio alichosema "Fashion is all about experimenting to try and find your style and you have some hits and misses along the way."

Tuesday, October 16, 2012

My article for newspaper: Miwani ya jua




Miwani ya jua ni zaidi ya kitupio cha mitindo
Ingawa umeshavaa tayari kuelekea kwenye mkutano au mtoko wako mwingine, unajisikia kuna kitu umekosa. Ni nini hicho? Ni hiyo miwani ya jua ambayo itakinga macho yako na jua na pia inaongeza mvuto wa muonekano wako.

Miwani ya jua inaimarisha afya na usalama wa jicho. Ni muhimu kuyapa macho yetu kipaumbele leo ili kuwa na uhakika wa ubora ule ule hapo uzeeni. Usitoke nyumbani bila ya  miwani yako ya jua hasa kwa siku ambayo jua ni kali. Kwa majira yote ya mwaka miwani ya jua inatakiwa kuwa sehemu ya kila siku ya maisha yako. Malaka hii itakujuza umuhimu wa miwani ya jua zaidi ya kuwa kitupio maarufu cha mitindo.

Miwani ya jua ina historia ndefu toka enzi za himaya ya Roma. Kutokana na kukua kwa teknolojia miwani hii nayo inabadilika kuendana na wakati.

Wavaaji leo wanajua miwani hii sio tu kitupio cha mitindo bali ni muhimu kwa afya ya macho yao kuyakinga na mionzi hatari ya jua ijulikanayo kama UV (Ultraviolet rays). Wengi wetu tunajua kuwa mionzi hii inaweza kusababisha saratani ya ngozi na matatizo mengine ya kiafya. Binadamu anaweza kuzuia yote hii kirahisi tu kwa kuvaa miwani sahihi ya jua ambayo inazuia mionzi ya UV hadi 100%. Tatizo ni kuwa huwezi kuona zuio hili kwa macho kwa kuwa ama limechanganywa au kuwekwa kama kingozi chembamba sana kwenye lensi. Njia ya kujua miwani ina zuio hili ni kwa kupima kwa kifaa maalumu au kusoma maelekezo yanayosema miwani ina zuio la UV kwa 100% au mingine imeandikwa UV 400.

Mitindo ndio inaamua ni miwani gani inaendana na wakati husika. Kutokana na kuwa na bei, staili na aina nyingi za miwani hii inaweza kuwa ngumu kwa mvaaji kuamua ni ipi anunue kutimiza kiu ya mitindo na kulinda afya ya macho yake. Wakati wa kununua zingatia vitu vikubwa vitatu ambavyo ni kinga ya jicho, ukivaa ujisikie huru na mtindo utakaokupendeza. Usidanganyike na rangi za lensi, ziwe kijani, nyekundu, kijivu na hata rangi ya udongo; zote zinaweza kufanya kazi kama ile ya lensi nyeusi. Zuio la UV liwe ni kigezo kikuu.

Chagua miwani kuendana na umbo la uso wako.  Kwa mfano kama umejaaliwa uso mnene, jitahidi kuepuka miwani itakayoonekana mikubwa sana au midogo sana. Vaa saizi ya kati na kama una uso wa pembe nne na hasa mataya makubwa epuka miwani yenye fremu nyembamba kwa ajili itafanya uonekane mpana sana. Kuna miwani inayowapendeza wenye sura ndefu na pia kuna inayowapendeza wenye sura pana ama za duara.

 Kama unavaa miwani ya jua wakati wa kuendesha chombo cha moto au kwenye kazi kama za bustani kwa mfano fikiria kununua yenye lensi imara zaidi na ambayo haivunjiki kurusha vipande vipande. Lensi inaweza kuwa ya kioo au plastiki au za kubadilika rangi kuendana na kiwango cha mwanga ni sawa tu ili mradi ziwe na zuio la UV. Fremu za rangi nyeusi na udongo zinampendeza walau kila mtu wakati zile za rangi rangi hazimpendezi kila mtu. Maelekezo ya uimara wa lensi utayapata kwenye duka ya muuzaji aliye mtaalamu na sio hiyo ya kununua mitaani. Hakikisha unajaribu miwani kabla hujainunua.
Wanawake wengi hawana uhakika jinsi ya kupaka vipodozi na miwani ya jua. Hii wala isiwe taabu. Oanisha rangi ya fremu za miwani yako na vipodozi utakavyotumia. Pia lensi nene zinafanya macho yawe makubwa kwa hiyo ukipaka wanja wa kope itasaidia kupunguza ukubwa wa jicho hivyo kuleta uwiano. Kwa vile miwani inalala maeneo ya nyusi hakikisha zimetindwa vyema na ukitaka zionekane zaidi basi ongezea wanja. Kope za kubandika zinaweza kugusa miwani na kuacha rangi ya maskara. Weka kope fupi na maskara isiwe nyingi kiasi cha kuweza kuchafua lensi za miwani. Usihisi kuwa unatakiwa kujaza vipodozi ili vionekane nje ya miwani. Wacha uzuri wa asili wa macho yako kwa kutumia vipodozi vichache.

Kuvaa miwani ya jua ndani ya majengo ni sawa kwa vile mvaaji ama anataka kuwa na mvuto au hataki kujulikana kwa sana kwa kila anayemfahamu.
Miwani ya wabunifu ni mizuri sana kimuonekano lakini sio kwamba ni ya kimuujiza kulinganisha na mingine. Kama chaguo lako la kuvaa miwani ya jua ni kwa ajili ya mitindo au ni kwa kukinga macho kutokana na jua, kumbuka kuwa haitakiwi kuwa ghali ili kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kucheza salama, nunua miwani ya jua toka kwenye maduka yenye wataalam  ambayo unaweza kupata kwa bei ya kati ya elfu 20 hadi 50 na epuka kununua ya barabarani ambayo inaweza kuwa na zuio la UV lakini isiwe imara ya kudumu tuseme mwaka mzima. Kwa kawaida mtu anahitaji miwani ya jua moja tu. Usisahau watoto pia wanahitajika kuzuiwa macho yao yasiharibiwe na hii mionzi hatari ya jua.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.

Tuesday, October 9, 2012

My article for newspaper: Pamba sakafu ya nyumba yako kwa zulia




Pamba sakafu ya nyumba yako kwa zulia

Leo hii kuna aina nyingi za kisasa za mionekano ya sakafu za ndani ya nyumba. Zipo sakafu zilizopambwa kwa marumaru, mawe (mfano mawe ya Tanga), mbao na hata mazulia. Kwa hiyo sakafu ya aina yoyote unayotaka inapatikana. Hata hivyo kitu kimoja kinabakia kuwa kweli kuwa sakafu za ndani ya nyumba zilizofunikwa kwa zulia ndio maarufu zaidi duniani.

Zulia ni urembo wa sakafu unaoonekana kupendwa na wa kisasa zaidi majumbani, maofsini na hata mahotelini .Bila shaka, mazulia madogo na hata yale yakufunika kufikia ukuta kwa ukuta yanaongeza uzuri wa nyumba. Ingawa zulia la kufunika ukuta hadi ukuta linaleta muonekano wa mvuto zaidi lakini laweza kuwa ghali kwa sababu kadhaa kama uwekaji, usafishaji na utunzaji.

Zulia linasaidia kuleta hali ya joto na ulaini miguuni, hasa kwenye vyumba vya kulala na sebuleni. Sakafu ngumu kwa mfano marumaru zinateleza zikilowa wakati za zulia linasaidia kuzuia utelezi. Zulia la ukuta kwa ukuta halitelezi wala kusogea kwani limeweka likajishikilia ukilishangisha na zile zulia ndogo ndogo. Sakafu ya kutoteleza inathamani sana kwa nyumba zenye wazee na watoto wadogo.

Zulia linarahisisha mapambo ya ndani kwa ajili zinapatikana kwa rangi na michoro mbalimbali. Ukilinganisha na mionekano mingine ya sakafu kama marumaru na mawe; sakafu za zulia zinaweza kuwa za bei nafuu zaidi ingawaje utunzaji na usafi wake ni gharama zaidi.

Kati ya sakafu zote sakafu iliyofunikwa kwa zulia ni nzuri zaidi kumaliza kelele za miguu na pia ni kizuizi kizuri cha sauti. Kuna tafiti zimeonyesha kuwa zulia zinasaidia kusafisha hewa kwa kudaka vumbi kwa hivyo kwa kulisafisha mara kwa mara inasaidia kuweka hewa safi ndani ya nyumba. Zulia pia zinadumu muda mrefu kwa kuwa nyingi zinatengenezwa imara. Kwa mfano zulia la kufunika ukuta kwa ukuta laweza kudumu kati ya miaka 5 hadi 30.

Zulia sahihi ni zaidi ya staili na rangi. Kabla hujaweka zulia kwanza jiangalie aina ya maisha unayoishi, ni nini kinachofanyika hapo mahali unapotaka kuweka. Wakati wa kununua jiulize maswali machache kama ni kwa kiasi gani chumba au mahali husika  panatembelewa. Je chumba hicho kinapata mwanga wa jua wa kutosha ? Je hapo mahali au hicho chumba ni cha ndani kwa ndani au ni cha kwanza ukitokea nje?  Mazingira ya nje kabla hujaingia ndani ya nyumba yakoje na ni mara ngapi kwa wiki utakuwa unatumia mashine kusafisha zulia husika.

Kutokana na aina mbalimbali ya mazulia zilizopo, unaweza kuamua yapi ni sahihi kutokana na wewe na familia yako. Mazulia madogo yanafanya chumba kiwe cha ukaribisho zaidi na ndio maana watu wengi wanayanunua kwa ajili ya sebule zao na yanapatikana kwa saizi, michoro na rangi mbalimbali wakati yale ya ukuta kwa ukuta mengi ni ya rangi moja.

Chagua zulia ambalo hautajutia hela yako kwa miaka mingi ijayo. Hakuna uamuzi utakaoathiri upambaji wako kama rangi ya zulia utakayochagua. Rangi zisizokolea zinafanya chumba kionekane kikubwa na pia doa huonekana zaidi. Kama unataka chumba chako cha kulia chakula kionekane kikubwa, au hata sebule yako kuwa wazi zaidi, zulia lenye rangi zisizokolea linaleta matokeo haya.
Rangi zilizokolea hufanya chumba kionekane kidogo hivyo kama unataka chumba cha kulala kikubwa kionekane kidogo basi weka zulia la rangi iliyokolea. Pia wataalamu wanashauri kuweka zulia lenye rangi kama ya udongo wa eneo lako. Hata hivyo hiki kisiwe kibali cha uchafu! Kwenye mapambo mengine ya ndani chagua rangi za familia moja na za zulia.

Elewa umuhimu wa mwanga. Mianga ya aina tofauti inafanya rangi za zulia kubadilika kwa kila mwanga. Mwanga wa asili toka dirishani utaleta matokeo tofauti na mwanga wa taa ya juu ya kichwa au ya kivuli. Kabla ya kununua jaribu sampo yako kuona inabadilika vipi na mianga mbalimbali.  

Matumizi ya rangi za kuwaka au zilizopoa hutegemea na upendeleo binafsi, hali ya tabia nchi na mazingira mazima ya nyumbani kwako. Mazulia ya rangi ya bluu na kijani yanafaa zaidi kwenye vyumba vinavyopata mwanga wa jua kwa kiasi kikubwa. Rangi za kuwaka kama chungwa na karoti zinafaa vyumba vya mwanga hafifu.

Zulia ndogo ndogo zina urembo wa maua, michoro, rangi na saizi mbalimbali hivyo chagua kuendana na bajeti yako dhidi ya yale makubwa ya ukuta kwa ukuta ambayo mara nyingi ni ya rangi moja na huuzwa kwa mita. Usiweke zulia la ukuta kwa ukuta kama makazi yako sio ya kudumu. Weka yale madogo madogo. Mbali na kuwa na chaguzi mbalimbali za haya madogo pia ni rahisi kutoa kuweka jipya au kuhamisha toka eneo moja hadi nyingine hata utakapohama nyumba.

Ni sahihi kusema kuwa mazulia yawe madogo au ya kufunika kote yana chagamoto zake ingawa yanasaidia sana kuboresha nyumba yako. Hata hivyo ukilinganisha na hali ya uchumi nchi hii inayopitia ya wananchi walio wengi kuwa na mlo mmoja tu kwa siku, mambo haya ya mazulia yamewekwa pembeni. Ingawa, bado kuna wenye nyumba wengi wanaothamini mapambo ya ndani kwa kuwa yanahuisha mwili, nafsi na akili ya mwonaji.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23