Tuesday, October 9, 2012

My article for newspaper: Pamba sakafu ya nyumba yako kwa zulia




Pamba sakafu ya nyumba yako kwa zulia

Leo hii kuna aina nyingi za kisasa za mionekano ya sakafu za ndani ya nyumba. Zipo sakafu zilizopambwa kwa marumaru, mawe (mfano mawe ya Tanga), mbao na hata mazulia. Kwa hiyo sakafu ya aina yoyote unayotaka inapatikana. Hata hivyo kitu kimoja kinabakia kuwa kweli kuwa sakafu za ndani ya nyumba zilizofunikwa kwa zulia ndio maarufu zaidi duniani.

Zulia ni urembo wa sakafu unaoonekana kupendwa na wa kisasa zaidi majumbani, maofsini na hata mahotelini .Bila shaka, mazulia madogo na hata yale yakufunika kufikia ukuta kwa ukuta yanaongeza uzuri wa nyumba. Ingawa zulia la kufunika ukuta hadi ukuta linaleta muonekano wa mvuto zaidi lakini laweza kuwa ghali kwa sababu kadhaa kama uwekaji, usafishaji na utunzaji.

Zulia linasaidia kuleta hali ya joto na ulaini miguuni, hasa kwenye vyumba vya kulala na sebuleni. Sakafu ngumu kwa mfano marumaru zinateleza zikilowa wakati za zulia linasaidia kuzuia utelezi. Zulia la ukuta kwa ukuta halitelezi wala kusogea kwani limeweka likajishikilia ukilishangisha na zile zulia ndogo ndogo. Sakafu ya kutoteleza inathamani sana kwa nyumba zenye wazee na watoto wadogo.

Zulia linarahisisha mapambo ya ndani kwa ajili zinapatikana kwa rangi na michoro mbalimbali. Ukilinganisha na mionekano mingine ya sakafu kama marumaru na mawe; sakafu za zulia zinaweza kuwa za bei nafuu zaidi ingawaje utunzaji na usafi wake ni gharama zaidi.

Kati ya sakafu zote sakafu iliyofunikwa kwa zulia ni nzuri zaidi kumaliza kelele za miguu na pia ni kizuizi kizuri cha sauti. Kuna tafiti zimeonyesha kuwa zulia zinasaidia kusafisha hewa kwa kudaka vumbi kwa hivyo kwa kulisafisha mara kwa mara inasaidia kuweka hewa safi ndani ya nyumba. Zulia pia zinadumu muda mrefu kwa kuwa nyingi zinatengenezwa imara. Kwa mfano zulia la kufunika ukuta kwa ukuta laweza kudumu kati ya miaka 5 hadi 30.

Zulia sahihi ni zaidi ya staili na rangi. Kabla hujaweka zulia kwanza jiangalie aina ya maisha unayoishi, ni nini kinachofanyika hapo mahali unapotaka kuweka. Wakati wa kununua jiulize maswali machache kama ni kwa kiasi gani chumba au mahali husika  panatembelewa. Je chumba hicho kinapata mwanga wa jua wa kutosha ? Je hapo mahali au hicho chumba ni cha ndani kwa ndani au ni cha kwanza ukitokea nje?  Mazingira ya nje kabla hujaingia ndani ya nyumba yakoje na ni mara ngapi kwa wiki utakuwa unatumia mashine kusafisha zulia husika.

Kutokana na aina mbalimbali ya mazulia zilizopo, unaweza kuamua yapi ni sahihi kutokana na wewe na familia yako. Mazulia madogo yanafanya chumba kiwe cha ukaribisho zaidi na ndio maana watu wengi wanayanunua kwa ajili ya sebule zao na yanapatikana kwa saizi, michoro na rangi mbalimbali wakati yale ya ukuta kwa ukuta mengi ni ya rangi moja.

Chagua zulia ambalo hautajutia hela yako kwa miaka mingi ijayo. Hakuna uamuzi utakaoathiri upambaji wako kama rangi ya zulia utakayochagua. Rangi zisizokolea zinafanya chumba kionekane kikubwa na pia doa huonekana zaidi. Kama unataka chumba chako cha kulia chakula kionekane kikubwa, au hata sebule yako kuwa wazi zaidi, zulia lenye rangi zisizokolea linaleta matokeo haya.
Rangi zilizokolea hufanya chumba kionekane kidogo hivyo kama unataka chumba cha kulala kikubwa kionekane kidogo basi weka zulia la rangi iliyokolea. Pia wataalamu wanashauri kuweka zulia lenye rangi kama ya udongo wa eneo lako. Hata hivyo hiki kisiwe kibali cha uchafu! Kwenye mapambo mengine ya ndani chagua rangi za familia moja na za zulia.

Elewa umuhimu wa mwanga. Mianga ya aina tofauti inafanya rangi za zulia kubadilika kwa kila mwanga. Mwanga wa asili toka dirishani utaleta matokeo tofauti na mwanga wa taa ya juu ya kichwa au ya kivuli. Kabla ya kununua jaribu sampo yako kuona inabadilika vipi na mianga mbalimbali.  

Matumizi ya rangi za kuwaka au zilizopoa hutegemea na upendeleo binafsi, hali ya tabia nchi na mazingira mazima ya nyumbani kwako. Mazulia ya rangi ya bluu na kijani yanafaa zaidi kwenye vyumba vinavyopata mwanga wa jua kwa kiasi kikubwa. Rangi za kuwaka kama chungwa na karoti zinafaa vyumba vya mwanga hafifu.

Zulia ndogo ndogo zina urembo wa maua, michoro, rangi na saizi mbalimbali hivyo chagua kuendana na bajeti yako dhidi ya yale makubwa ya ukuta kwa ukuta ambayo mara nyingi ni ya rangi moja na huuzwa kwa mita. Usiweke zulia la ukuta kwa ukuta kama makazi yako sio ya kudumu. Weka yale madogo madogo. Mbali na kuwa na chaguzi mbalimbali za haya madogo pia ni rahisi kutoa kuweka jipya au kuhamisha toka eneo moja hadi nyingine hata utakapohama nyumba.

Ni sahihi kusema kuwa mazulia yawe madogo au ya kufunika kote yana chagamoto zake ingawa yanasaidia sana kuboresha nyumba yako. Hata hivyo ukilinganisha na hali ya uchumi nchi hii inayopitia ya wananchi walio wengi kuwa na mlo mmoja tu kwa siku, mambo haya ya mazulia yamewekwa pembeni. Ingawa, bado kuna wenye nyumba wengi wanaothamini mapambo ya ndani kwa kuwa yanahuisha mwili, nafsi na akili ya mwonaji.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23

1 comment:

  1. Habri Vivi mimi natafuta sakafu ya mbao kwa bei nafuu lkn imekuwa vigumu kutakana na bei eneo ni dogo tu la mita za mraba 80, je naweza pata kwa bei nafuu watu unafahamu?

    ReplyDelete