Tuesday, October 16, 2012

My article for newspaper: Miwani ya jua




Miwani ya jua ni zaidi ya kitupio cha mitindo
Ingawa umeshavaa tayari kuelekea kwenye mkutano au mtoko wako mwingine, unajisikia kuna kitu umekosa. Ni nini hicho? Ni hiyo miwani ya jua ambayo itakinga macho yako na jua na pia inaongeza mvuto wa muonekano wako.

Miwani ya jua inaimarisha afya na usalama wa jicho. Ni muhimu kuyapa macho yetu kipaumbele leo ili kuwa na uhakika wa ubora ule ule hapo uzeeni. Usitoke nyumbani bila ya  miwani yako ya jua hasa kwa siku ambayo jua ni kali. Kwa majira yote ya mwaka miwani ya jua inatakiwa kuwa sehemu ya kila siku ya maisha yako. Malaka hii itakujuza umuhimu wa miwani ya jua zaidi ya kuwa kitupio maarufu cha mitindo.

Miwani ya jua ina historia ndefu toka enzi za himaya ya Roma. Kutokana na kukua kwa teknolojia miwani hii nayo inabadilika kuendana na wakati.

Wavaaji leo wanajua miwani hii sio tu kitupio cha mitindo bali ni muhimu kwa afya ya macho yao kuyakinga na mionzi hatari ya jua ijulikanayo kama UV (Ultraviolet rays). Wengi wetu tunajua kuwa mionzi hii inaweza kusababisha saratani ya ngozi na matatizo mengine ya kiafya. Binadamu anaweza kuzuia yote hii kirahisi tu kwa kuvaa miwani sahihi ya jua ambayo inazuia mionzi ya UV hadi 100%. Tatizo ni kuwa huwezi kuona zuio hili kwa macho kwa kuwa ama limechanganywa au kuwekwa kama kingozi chembamba sana kwenye lensi. Njia ya kujua miwani ina zuio hili ni kwa kupima kwa kifaa maalumu au kusoma maelekezo yanayosema miwani ina zuio la UV kwa 100% au mingine imeandikwa UV 400.

Mitindo ndio inaamua ni miwani gani inaendana na wakati husika. Kutokana na kuwa na bei, staili na aina nyingi za miwani hii inaweza kuwa ngumu kwa mvaaji kuamua ni ipi anunue kutimiza kiu ya mitindo na kulinda afya ya macho yake. Wakati wa kununua zingatia vitu vikubwa vitatu ambavyo ni kinga ya jicho, ukivaa ujisikie huru na mtindo utakaokupendeza. Usidanganyike na rangi za lensi, ziwe kijani, nyekundu, kijivu na hata rangi ya udongo; zote zinaweza kufanya kazi kama ile ya lensi nyeusi. Zuio la UV liwe ni kigezo kikuu.

Chagua miwani kuendana na umbo la uso wako.  Kwa mfano kama umejaaliwa uso mnene, jitahidi kuepuka miwani itakayoonekana mikubwa sana au midogo sana. Vaa saizi ya kati na kama una uso wa pembe nne na hasa mataya makubwa epuka miwani yenye fremu nyembamba kwa ajili itafanya uonekane mpana sana. Kuna miwani inayowapendeza wenye sura ndefu na pia kuna inayowapendeza wenye sura pana ama za duara.

 Kama unavaa miwani ya jua wakati wa kuendesha chombo cha moto au kwenye kazi kama za bustani kwa mfano fikiria kununua yenye lensi imara zaidi na ambayo haivunjiki kurusha vipande vipande. Lensi inaweza kuwa ya kioo au plastiki au za kubadilika rangi kuendana na kiwango cha mwanga ni sawa tu ili mradi ziwe na zuio la UV. Fremu za rangi nyeusi na udongo zinampendeza walau kila mtu wakati zile za rangi rangi hazimpendezi kila mtu. Maelekezo ya uimara wa lensi utayapata kwenye duka ya muuzaji aliye mtaalamu na sio hiyo ya kununua mitaani. Hakikisha unajaribu miwani kabla hujainunua.
Wanawake wengi hawana uhakika jinsi ya kupaka vipodozi na miwani ya jua. Hii wala isiwe taabu. Oanisha rangi ya fremu za miwani yako na vipodozi utakavyotumia. Pia lensi nene zinafanya macho yawe makubwa kwa hiyo ukipaka wanja wa kope itasaidia kupunguza ukubwa wa jicho hivyo kuleta uwiano. Kwa vile miwani inalala maeneo ya nyusi hakikisha zimetindwa vyema na ukitaka zionekane zaidi basi ongezea wanja. Kope za kubandika zinaweza kugusa miwani na kuacha rangi ya maskara. Weka kope fupi na maskara isiwe nyingi kiasi cha kuweza kuchafua lensi za miwani. Usihisi kuwa unatakiwa kujaza vipodozi ili vionekane nje ya miwani. Wacha uzuri wa asili wa macho yako kwa kutumia vipodozi vichache.

Kuvaa miwani ya jua ndani ya majengo ni sawa kwa vile mvaaji ama anataka kuwa na mvuto au hataki kujulikana kwa sana kwa kila anayemfahamu.
Miwani ya wabunifu ni mizuri sana kimuonekano lakini sio kwamba ni ya kimuujiza kulinganisha na mingine. Kama chaguo lako la kuvaa miwani ya jua ni kwa ajili ya mitindo au ni kwa kukinga macho kutokana na jua, kumbuka kuwa haitakiwi kuwa ghali ili kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kucheza salama, nunua miwani ya jua toka kwenye maduka yenye wataalam  ambayo unaweza kupata kwa bei ya kati ya elfu 20 hadi 50 na epuka kununua ya barabarani ambayo inaweza kuwa na zuio la UV lakini isiwe imara ya kudumu tuseme mwaka mzima. Kwa kawaida mtu anahitaji miwani ya jua moja tu. Usisahau watoto pia wanahitajika kuzuiwa macho yao yasiharibiwe na hii mionzi hatari ya jua.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.

No comments:

Post a Comment