MWANAFUNZI wa darasa la saba wa Shule ya Msingi
Mwagiligili, iliyopo Misungwi, mkoani Mwanza, Rahel Emmanuel (13), amekutwa
amekufa baada ya kujinyonga ndani ya nyumba ya Mwalimu wake Mkuu, John Msusa.
Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Msusa alisema tukio hilo
lilitokea juzi, saa sita mchana.
Alisema kabla ya kifo hicho, mwanafunzi huyo ambaye ni
mtoto wa shemeji yake, aliyeanza kuishi naye tangu akiwa mdogo alikutwa na
karatasi katika madaftari yake iliyokuwa na maneno ya mapenzi na alihojiwa
ofisini na kuruhusiwa kwenda nyumbani kumpikia mtoto chakula, ndipo
akajinyonga.
“Huyu mwanafunzi alikamatwa na kipande cha karatasi
katika madaftari yake kilichokuwa na maneno ya mapenzi, tulimhoji ofisini na
kumruhusu kwenda nyumbani kumpikia uji mtoto aliyekuwa analia, sasa alipofika
nyumbani kwangu alifanya uamuzi wa kujinyonga kwa kutumia kamba ndani ya nyumba
tunayoishi.
“Hatujui alifikiria nini hadi kuchukua uamuzi wa namna
hiyo, hili suala tunawaachia vyombo vya dola ili kuchunguza zaidi,” alisema
Msusa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwagiligili, Herman Paulo,
alikiri kutokea tukio hilo na alisema alichukua uamuzi wa kutoa taarifa Kituo
cha Polisi cha Misasi na walifika na kufanya uchunguzi na kuruhusu mwanafunzi
huyo kuzikwa jana katika Kijiji cha Kanyerere.
Pia Ofisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Misungwi, Efram
Maginge, alisema wamepata taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo, aliyekuwa
miongoni mwa waliotarajiwa kuhitimu mwaka huu.
Polisi wilayani Misungwi nao wamethibitisha kuwepo kwa
tukio hilo na walisema hakuna wanayemshikilia.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment