MGOMBEA Urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)
atajulikana Julai 12 mwaka huu baada ya kukamilisha mchakato mzima wa kuomba
kuwania nafasi hiyo, kutafuta wadhamini na kujadiliwa katika chama hicho.
Alisema mchakato wa kupata wagombea wa CCM katika vyombo
vya dola yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar,
wabunge, wawakilishi na madiwani kwa uchukuaji wa fomu utafanyika kuanzia Juni
3 hadi Julai 15 mwaka huu.
Gharama za fomu hizo hazijapanda zimebaki vile vile kama
zilivyokuwa mwaka 2010 na katika kanuni, yaani shilingi milioni 1 kwa urais,
shilingi laki moja kwa ubunge na elfu hamsini kwa diwani.
Akifafanua zaidi alisema kwamba, wagombea Urais
wataanzania kuchukua fomu,bila mbwembwe kuanzia Juni 3 na kutakiwa kurejesha
fomu hiyo mwisho saa 10 ya Julai 2 mwaka huu katika mazingira hayo hayo ya
kutokuwepo na shamrashamra.
Aidha alisema kuanzia tarehe hiyo ya uchukuaji fomu hadi
marejesho yake, wagombea watakuwa wanatafuta wadhamini 450 kutoka mikoa 15
nchini huku mikoa mitatu ikiwa ni kutoka Zanzibar na angalau mkoa mmoja uwe wa
Unguja au kisiwa cha Pemba.
Ongezeko hilo la mikoa na wadhamini linatokana na haja ya
kutafuta sampuli inayooana na idadi ya watu na mikoa kwa sasa. Tanzania ina
mikoa 31.
Uchaguzi uliopita wagombea walitakiwa kutafuta wadhamini
250 katika mikoa 10, minane ikiwa ni kutoka Bara. Alisema wagombea urais hao
wanapokwenda kutafuta wadhamini, wajumbe wote wa mkutano mkuu wa taifa
hawataruhusiwa kuwa wadhamini, huku mwanachama atakayekuwa mdhamini akizuiwa
kufanya udhamini wa zaidi ya mtu mmoja.
Kwa anayewania Urais wa Zanzibar tarehe za kuchukua na
kurejesha ni zile zile za Jamhuri, huku akitakiwa kupata wadhamini 250 kutoka
mikoa mitatu, mmoja ukiwa ama Unguja au Pemba.
Alisema vikao vya kuchuja wagombea Urais Zanzibar vitafanyika
kuanzia Julai 4 hadi 10 ambapo Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM itamtaja
Mgombea Urais wa Zanzibar.
Aidha wajumbe wote wa NEC hawaruhusiwi kumdhamini mgombea
Urais wa Zanzibar. Akizungumzia fomu za wagombea Ubunge, alisema kwamba
wanachama watachukua fomu hizo Julai 15 na kuzirejesha Julai 19 na mikutano ya
kampeni itafanyika kuanzia Julai 20-31 ili kuomba kura.
Kura ya maoni ya kuwapata wanaowania nafasi ya Ubunge
kupitia CCM itafanyika Agosti 1, mwaka huu. Kwa wanaowania Viti Maalumu ratiba
ni ile ile, lakini safari hii mchujo wa mwisho utafanywa na Baraza kuu la UWT
ambao kimsingi ndio wanaomiliki viti hivyo maalumu, ingawa mchujo wa awali
utafanyika katika jumuiya husika.
Viti maalumu safari hii vitawaniwa pia na jumuiya ya
wazazi ambao wamepewa viti viwili.Jumuiya nyingine ni jumuiya ya vijana, UWT
yenyewe,jumuiya ya wasomi, wafanyakazi na wenye ulemavu.
Ratiba ya kuwania udiwani nayo ni Julai 15 hadi 19 na
kura za maoni zitafanyika Agosti Mosi. Katibu huyo wa NEC hata hivyo
aliwatahadharisha wanaowania nafasi hizo za dola kupitia CCM, kuangalia kwa
makini kanuni za uchaguzi za chama hicho, kuzisoma na kuzielewa kwa kuwa kama
watafanya kosa litawagharimu ,huku akisisitiza ‘kosa moja goli moja’.
Akizungumzia namna ya kufanikisha kura ya maoni alisema
chama chake kitafunga daftari la wanachama Julai 15 na wapiga kura wa chama
hicho watalazimika kuwa na zaidi ya kadi ya chama kwa utambulisho ikiwamo kadi
ya kupiga kura ili kushiriki kura ya maoni.
Alisema nia ya kuweka vitambulisho viwili ni kuzuia
wapiga kura bandia ambao safari iliyopita walionekana kuwa chanzo cha matatizo.
Aidha, wanafanya hivyo ili kuzuia wasioitakia mema CCM kula njama ya kuiangusha
kupitia matumizi ya kadi bandia.
Aidha alisema ipo mikakati ambayo tayari inafanyiwa kazi
kuhakikisha mchakato mzima hadi kura wa maoni unafanikiwa kuwapa Watanzania
kile wanachokihitaji.
Pia alisema wagombea wote watakuwa pamoja katika mikutano
ya kuomba kura. Akijibu swali maana ya maelekezo ya sasa kama ni hakikisho
Katiba mpya haitakuwepo, Nape alisema CCM inafanya utaratibu wake kwa
kuzingatia Katiba iliyopo sasa na kama katiba mpya itakuja watakutana kufanya
mabadiliko yanayohitajika.
Mpaka gazeti hili linaenda mtamboni jana Kikao cha
halmshauri Kuu ya CCM kilikuwa kinaendelea.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment